Kuna aina tofauti za uongozi, kuna uongozi wa mabavu na kuna uongozi wa hamasa. Uongozi wa mabavu ni pale mtu anapolazimisha watu kufanya kitu fulani ambacho ni muhimu kufanyika. Uongozi wa hamasa ni pale ambapo mtu anawahamasisha watu kuchukua hatua na watu wanafanya hivyo kwa sababu wanaona ni muhimu kwao kufanya hivyo. Hawasubiri kulazimishwa badala yake wanajitoa na kufanya wenyewe.
Uongozi wa mabavu unaweza kuleta matokeo mtu anayotaka ndani ya muda mfupi, lakini ndani ya muda mrefu unaharibu mahusiano ya anayeongoza na anayeongozwa na hivyo kushindwa kupata matokeo ambayo mtu anataka. Uongozi wa hamasa ni uongozi ambao una manufaa makubwa sana kwa baadaye, unahitaji muda kujenga lakini baada ya hapo mambo yanakwenda vizuri.

Mwandishi Simon Sinek kwenye kitabu chake START WITH WHY anatupa mbinu moja muhimu ya kuweza kujijenga na kuwa viongozi wa hamasa. Njia hii ni kujua kwa nini unafanya kile ambacho unakifanya. Wewe ukishajua kwa nini unafanya, unaweza kuwahamasisha wengine na wao wakachukua hatua.
Simon ana falsafa yake moja anayoipa mkazo sana kwamba WATU HAWANUNUI KILE UNACHOUZA BALI WANANUNUA KWA NINI UNAUZA. Akiwa na maana kwamba watu wananunua ile sababu unayouza ambayo inaendana na wao. Na kwa tahadhari tu sababu unayouza siyo kupata fedha, bali ile thamani kubwa unayotoa.

Karibu kwenye makala hii ya uchambuzi wa kitabu hiki, ambapo tutajifunza mbinu za kuwa viongozi wa hamasa. Kila mtu ni kiongozi kwa nafasi fulani, unaweza kuwa kiongozi wa kisiasa, kiongozi wa dini, kiongozi wa kikazi, kiongozi wa kijamii na hata kiongozi wa kifamilia. Katika kila aina ya uongozi misingi ni ile ile, karibu tujifunze leo ili tuweze kuchukua hatua na kuwa viongozi bora.

1. Kwenye kitu chochote kinachofanyika, kuna misingi mikuu mitatu. Misingi hii inafananishwa na miduara mitatu, ambayo inaanzia nje kwenda ndani. Misingi hii ni kama ifuatavyo;

NINI UNAFANYA (WHAT), Hapa mtu anakuwa anajua kile ambacho anakifanya. Kila mtu anajua anachofanya, na hivyo ni rahisi mtu kusema anafanya nini. Kwa bahati mbaya msingi huu hauhamasishi watu wengi.

JINSI UNAVYOFANYA (HOW), Hapa mtu anakuwa anajua jinsi ya kufanya kile anachofanya. Siyo wote wanaojua jinsi ya kufanya, lakini hata wale wachache wanaojua bado hawawezi kuwashawishi wengi.

KWA NINI UNAFANYA (WHY), Hapa mtu anakuwa na sababu inayomsukuma kufanya kile ambacho anafanya. Ni wachache sana wanaojua kwa nini wanafanya kile wanachofanya, na hawa ndio wanaofanikiwa sana. Wale wanaojua kwa nini wanafanya, wanaweza kuwahamasisha wengi zaidi na kuwa viongozi bora.

 

2. Njia mbovu ya kuwahamasisha watu ni kuanza na nini, jinsi na kumalizia na kwa nini. Watu wengi wanapojaribu kuwahamasisha wengine ili waweze kuchukua hatua fulani, iwe ni kununua au kuweka juhudi, huanza na kile wanachofanya. Hapa huwaambia watu kile wanachofanya na kuwataka wachukue hatua, kama tulivyoona kujua unachofanya hakuhamasishi, na hivyo wanashindwa kushawishi wengine.

3. Njia sahihi ya kuwahamasisha wengine ni kuanza na KWA NINI, unapoanza na kwa nini unafanya unachofanya, unaingia ndani ya mioyo ya watu, wanaelewa kile unachofanya na wanachagua kuwa upande mmoja na wewe. Kwa nini inawahamasisha watu na kuweza kuchukua hatua.

4. Hakuna bidhaa au huduma yoyote iliyopo sokoni sasa ambayo haina upinzani. Biashara yoyote unayofanya au utakayopanga kufanya, watakuja watu wengine wataifanya vizuri kuliko wewe au wanatoa kwa bei ya chini kuliko unavyotoa wewe. Hivyo bila ya kuwa na kitu kinachowahamasisha na kuwavutia watu kufanya biashara na wewe, huwezi kuendelea kuwa nao, wataenda kwa wengine wanaofanya vizuri kuliko wewe.

5. Biashara yoyote unayoifanya, jua ni kwa nini unafanya kile unachofanya. Nisisitize tena, kupata fedha au faida siyo sababu inayoweza kuwahamasisha wengine. Fikiria kama fedha isingekuwa changamoto kwako, ni thamani ipi kubwa unayoitoa kwenye maisha ya wengine. Hii ndiyo sababu kuu na itumie kujenga uhusiano mzuri na wateja wako.

SOMA; MIMI NI MSHINDI, Ahadi Yangu Na Nafsi Yangu.

6. Kuna njia mbili pekee mtu anaweza kuzitumia kuathiri tabia ya binadamu. Yaani kama unataka kumfanya mtu yeyote afanye kile unachotaka afanye, awe ni mteja, mtoto, mwenza, mfanyakazi, unaweza kutumia njia hizi mbili;
Njia ya kwanza ni kudanganya na kutishia. Hapa unaweza kutumia hofu kumfanya mtu achukue hatua unayotaka achukue. Unaweza kumdanganya kwamba kwa kuchukua hatua hiyo atanufaika zaidi. Au unaweza kumtishia kwamba kama asipochukua hatua basi mambo yatakuwa mabaya sana kwake. Njia hii inaleta majibu ya muda mfupi, ila baadaye inaharibu sana.
Njia ya pili ni kuhamasisha. Hapa unampa mtu sababu kwa nini ni muhimu kwake kufanya kile ambacho unamtaka afanye. Na yeye mwenyewe anaamua kuchukua hatua kwa sababu ni muhimu kwake. Aina hii inajenga mahusiano mazuri baina ya wale wanaohusika.

7. Dunia ya sasa inaendeshwa kwa udanganyifu, hofu na vitisho. Hii ni kuanzia kwenye biashara, jamii, familia mpaka kwenye siasa. Watu wanatafuta njia ya mkato ya kuwahamasisha wengine kuchukua hatua na hivyo kutumia udanganyifu, hofu na vitisho. Viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitumia udanganyifu kupata kuungwa mkono. Wafanyabiashara wamekuwa wakitumia hofu kuwasukuma watu wanunue. Na viongozi wa kikazi, kijamii, kidini na kifamilia wamekuwa wanatumia vitisho kuwafanya watu wachukue hatua fulani wanayotaka wachukue.

8. Hakuna mchezo mbaya kufanya kwenye biashara kama kutumia bei kama kigezo cha kupata wateja. Wafanyabiashara wengi hufikiri kushusha bei au kupunguza bei kutavutia wateja wengi. Kweli kunawavutia kwa muda mfupi, lakini mshindani wako anapojua hilo na yeye akashusha bei basi wateja watahamia kwake. Unahitaji kuwa na sababu ambayo wateja wako wanaiamini na wanaendelea kufanya biashara na wewe hata kama kuna mwingine ana bei ndogo kuliko wewe.

9. Biashara inayofanikiwa ni ile ambayo ina wateja waaminifu, wateja ambao wanaichukulia biashara hiyo kama sehemu ya maisha yao. Wateja hawa ndio wanaoendelea kuwa kwenye biashara na kuwaleta wengine wengi kwenye biashara hiyo. Ili biashara iweze kuwa na wateja waaminifu, lazima kuwe na kitu ambacho kinawahamasisha wateja kuendelea kuwepo kwenye biashara hiyo. Na hamasa hiyo inahitaji kutokana na manufaa makubwa wanayoyapata.

10. Watu hawanunui kile unachouza (WHAT) bali wananunua ile sababu unayouza (WHY). Kile unachouza kila mtu anaweza kuuza, lakini ile sababu unayouza wengine hawawezi kuiiga. Unachohitaji ni kuijua sababu hii, na kuitumia kama njia ya kutengeneza wateja waaminifu kwa biashara yako. unapotoa sababu ya kwa nini unauza unachouza, unakutana na watu ambao wanaamini kile ambacho unaamini wewe na mtakwenda pamoja. Ukishawapata watu hawa huhitaji tena kutumia nguvu nyingi kuwafanya wanunue, badala yake wataona kununua ni wajibu wao, kwa sababu wote mpo pamoja. Ijenge biashara yako kwenye msingi huu na utakuwa na biashara bora sana kwako.

11. Ni hitaji letu sisi binadamu kuona kwamba tupo sehemu ya jamii fulani ambayo inaendana na sisi. Ndiyo maana watu wapo tayari kufanya mambo ambayo siyo muhimu kwao ili tu wawe pamoja na wale wanaofanya mambo hayo. Pia binadamu tunapenda kuwa sehemu ya kitu kikubwa, ambacho tunakiamini na kuona kinahusiana na sisi. Unaweza kutumia hitaji hili la binadamu kuwahamasisha wale unaowasimamia au wateja wako. Kwa kujua ni kitu gani wanachoamini na ukajiweka kwenye kile unachotaka wafanye.

12.Watu wanapokuwa na sababu ya kufanya kitu ambayo inaendana na kile wanachoamini, wapo tayari kufanya maamuzi hata kama hawajapata taarifa za kutosha. Hii ndiyo sababu kuna ambao huwa wanaonekana wanafanya maamuzi hatari lakini wanapata matokeo bora. Watu hawa wanakuwa wanaamini sana kile wanachofanya na kuwa wanakielewa vizuri. Kwa njia hii kuna baadhi ya hisia huwa zinawajia na kuona maamuzi wanayofanya ni sahihi. Amini kwenye kile unachofanya na utaweza kuwaaminisha wengine wengi zaidi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Sign-Posts On The Road To Success (Alama Muhimu Kwenye Safari Ya Mafanikio).

13. Wakati mwingine watu wanafanya kitu ili kuonekana kuwa nao wao wanafanya. Lakini kutaka huku kuonekana kunaanza na kuamini kile ambacho wanakwenda kufanya. Kuna watu wananunua bidhaa au huduma fulani ili wengine wawaone na wao ni watu wa aina fulani. Pia kuna watu ambao wanakubali kufanya kazi fulani kwa sababu wanataka waonekane ni sehemu ya mchango kwenye kazi hiyo. Jua mahitaji ya watu ni yapi na watimizie, utawahamasisha kuchukua hatua.

14. Ukishajua kwa nini unafanya unachofanya, unahitaji kujua unakifanyaje. Hapa kwenye kujua jinsi ya kufanya ndipo penye misingi muhimu ambayo mtu anaisimamia katika kutekeleza kile anachofanya. Bila ya misingi ile sababu ya kufanya haitaweza kufikiwa. Na watu wanapohamasika kwa ile sababu ya kufanya, wanapenda kuona misingi iliyopo kwenye ufanyaji. Kwenye jinsi ya kufanya ndipo penye nidhamu na utamaduni unaotumika, iwe ni kwenye kazi, biashara au jamii.

15. Kila unachosema na kila unachofanya kinatakiwa kuendana na kile unachoamini. Ile sababu ya kwa nini unafanya unachofanya ndicho unachoamini, jinsi unavyofanya ndivyo unavyotekeleza ile imani yako. Na nini unachofanya ni matokeo ya mwisho. Unapokuwa na sababu ya kufanya, lakini huna misingi unayosimamia kwenye ufanyaji, huwezi kupata matokeo unayotarajia kupata. Maneno yako na matendo yako ni lazima yaendane kama kweli unataka kupata unachotaka kupata.

16. Ili uweze kuwahamasisha wengine, ili uweze kufikia kile unachotaka kufikia, unahitaji kuwa halisi. Kuwa na sababu ambayo inatokana na wewe kweli na kisha ifanyie kazi . Unapokuwa halisi unafanya kile ambacho unakiamini kweli, na unaweza kupambana hata kama unakutana na changamoto. Kuwa halisi ni hitaji muhimu la kupata mafanikio yakudumu. Unaweza kuiga au kuigiza na ukapata mafanikio, lakini kwa kukosa uhalisia mafanikio hayo hayawezi kudumu.

17. Binadamu tuna uwezo mkubwa wa kujua ni mtu gani yuko halisi na yupi ambaye anaigiza au ambaye ana ajenda nyingine binafsi. Mtu anaweza kuongea kwa hamasa sana, lakini kama hayupo halisi, watu wataona hilo na hawatakuwa tayari kufanya kile ambacho anawataka wafanye. Kuwa halisi kwenye kila unachofanya, utawavutia wale halisi na watakuwa tayari kufanya kile ambacho unawataka wafanye.

18. Kwenye biashara, watu wanaposhawishika kwamba maamuzi wanayofanya ni sahihi kwao, wapo tayari kulipa gharama yoyote ambayo wanaweza kulipa. Hivyo jukumu la mfanyabiashara siyo kumshawishi mtu kuhusu bei ya kitu, bali kumwonesha ni kwa namna gani kitu kile ni muhimu kwake. Mtu anachukua maamuzi ambayo anajua ni muhimu kwake na hivyo kuwa tayari kulipa gharama ili kupata kile wanachotaka.

SOMA; Sehemu Kumi (10) Unazoweza Kupata Muda Wa Kujiongezea Maarifa Kupitia Kusoma Vitabu.

19. Lengo la biashara siyo kumuuzia kila mtu ambaye anataka kununua, bali kumuuzia yule ambaye anaamini kile unachouza, ambaye atanunua na kufaidika na kuja kununua tena na tena na kuwaleta wengine pia. Unapochagua kufanya biashara na watu hawa wanaoamini kile unachoamini, watu hao wanajenga uaminifu mkubwa na wewe na wanakuwa tayari kufanya kile unachowataka wafanye, kwa sababu wanakuamini huwezi kufanya kitu ambacho hakina manufaa kwao.

20. Kuongoza na kuwa kiongozi ni vitu viwili tofauti kabisa, wengi hawajui na hivyo kuchanganya.

Kuwa kiongozi (BEING A LEADER) maana yake unashika madaraka ya juu na unakuwa ndiyo mwamuzi wa mwisho. Una mamlaka ya kuwafanya watu wachukue hatua iwe wanapenda au hawapendi kufanya hivyo.

Kuongoza (LEADING) maana yake watu wanakuwa tayari kukufuata, siyo kwa sababu wanalazimika kufanya hivyo na wala siyo kwa sababu wakikufuata ndiyo wanalipwa, ila kwa sababu wameamua kukufuata. Wanaamua kukufuata kwa sababu wanakuamini kwa kuwa unaamini kile wanachoamini, wanakufuata kwa sababu umewapa sababu ambayo inaendana na kile wanachoamini.
Maisha ya furaha na mafanikio yanatokana na kuongoza na siyo kuwa kiongozi, nenda kaongoze na siyo tu kutaka kuwa kiongozi.

Kila mtu ni kiongozi kwenye nafasi fulani ya maisha yake, kila mtu anahitaji kuwashawishi watu kuchukua hatua fulani, tumia haya uliyojifunza hapa ili kuimarisha ushawishi wako, kujenga mahusiano bora na kuweza kufikia maisha ya ndoto yako, yenye furaha na mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri,
Rafiki Na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz