Miongoni mwa kitu kinachowatesa watu wengi katika safari ya mafanikio, ni kule kutaka kuona kipato chao kinakuwa siku hadi siku. Wengi huwa wanahamasa kubwa ya namna hii, ya kutaka kuona kipato chao kinakua hali ambayo husababisha hata watafute pesa usiku na mchana.
Pamoja na kiu hiyo kubwa, kitu cha kujiuliza mimi na wewe ni wangapi kati ya watu hawa ambao wanaelewa njia sahihi za kuboresha kipato chao? Inawezekana ni wachache wanaojua na wengi kubaki hawaelewi sana. Lakini kupitia makala hii naomba nikukumbushe njia za kukusaidia kuboresha kipato chako kila siku.
1. Epuka matumizi yasiyo ya lazima.
Kama unaishi maisha ya kuwa na matumizi mabovu ya pesa kila wakati, elewa kabisa itakuwa ngumu sana kwako kuweza kuboresha kipato chako. Hutaweza kujihakikishia kipato cha kudumu kama matumizi yako ni mabovu. Kila wakati kuwa makini sana na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima kwako.
Kumbuka unapokuwa unatumia pesa zako vizuri, hiyo itakusaidia sana katika suala zima la kuboresha kipato chako na kuwa cha kudumu. Kwa nini hiyo iko hivyo? Ni kwa sababu utaokoa pesa nyingi ambazo ungezipoteza. Hivyo kwa vyovyote vile ni lazima itakusaidia kuboresha kipato chako.
Tengeneza vyanzo vingine vya kukuingizia pesa.
2. Tengeneza bajeti ya kukuongoza.
Siri nyingine ya kukusaidia kujihakikishia kipato cha kudumu ni kutengeneza bajeti. Hakikisha unatengeneza bajeti yako ambayo itakuwa inakuongoza katika suala zima la matumizi ya pesa. Usiishi tu kiholela bila kuwa na bajeti yako maalum.
Watu wengi wanashidwa kutengeneza pato lao la kudumu kwa sababu hawana bajeti ya kudumu. Unapokuwa na bajeti inakusaidia sana usitumie pesa zako hovyo. Hiyo ikiwa na maana pesa zako zitatumika kwa utaratibu na zitadumu.
3. Tengeneza  vyanzo vingine vya pesa.
Huwezi kuboreshakipato chako na kikawa cha kudumu kama huna vyanzo vingine vya pesa. Ni lazima uwe na vyanzo vingine vya pesa mbali na hicho ulichonacho. Hiyo itakusaidia sana kuboresha pato lako kila kukicha.
Kwa mfano kama umeajiriwa, tafuta namna ambayo unaweza ukatafuta biashara nyingine ya kukuingizia pesa. Kama umejiajiri na una biashara moja, halikadhalika unatakiwa kutafuta kitu kingine cha kukusaidia kuingiza pesa. Hiyo itakuwa ni njia sahihi sana kwako pia ya kuboresha kipato chako.
4. Weka akiba.
Kujiwekea akiba ni mbinu nyingine ambayo unaweza kuitumia kuboresha kipato chako. Acha kuthubutu kutumia kila pesa uliyonayo mpaka ukabaki huna kitu. Ni lazima uwe na akiba itakayokusaidaia katika kuwekeza na pia katika dharura zingine za kimaisha.
Kwa kiasi chohote cha pesa unachopata tenga nyingine iwe akiba yako. Hata kama pesa hiyo ni ndogo sana usiidharau, baada ya muda itakuwa ni pesa nyingi ambayo itakusaidaia. Kwa kufanya hivyo utajiweka katika mazingira mazuri ya kuboresha kipato chako.
5. Tengeneza nidhamu ya pesa.
Hata kama unaingiza pesa nyingi kiasi gani lakini ikiwa wewe binafsi huna ile nidhamu ya pesa basi hiyo itakuwa ni sawa na kazi bure. Ni vizuri sana kujitengenezea nidhamu ya pesa itakayokuongoza katika kuboresha kipato chako kila kukicha.
Kwa kifupi hayo ndiyo mambo machache yanayoweza kukusaidia kuboresha kipato chako ikiwa uatayafanyia kazi.
Nakutakia siku njema na endelea kujifunza kupitia AMKA MTANZANIA kila siku.
Kwa malaka nyingine nzuri za mafanikio tembelea pia DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi.
Ni wako rafiki katika kusaka mafanikio ya kweli,
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,