Kumekuwa na kilio na malalamiko ya wafanyabiashara nchi nzima juu ya hali ngumu ya ufanyaji wa biashara.
Tangu kumetokea mabadiliko ya uongozi kwenye nchi yetu Tanzania, kumekuwa na mabadiliko mengi yanayoendelea nchini. Mabadiliko haya yamebadili sana hali ya uchumi na hivyo kuvuruga mambo mengi ya kibiashara.
Tunashuhudia biashara kubwa zikifungwa kwa kukosa wateja na nyingine kufungwa kwa kutokuendeshwa kwa misingi ya kisheria. Tumeona mahoteli makubwa yanafungwa huku mengine yakibadilishwa na kuwa nyumba za makazi. Tumeona biashara zilizokuwa zinakwepa kodi zikifungiwa. Na pia tunaona biashara zilizokuwa zinaendeshwa bila vibali maalumu zikifungwa.
Sisi kama wafanyabiashara makini, tunaweza kuamua kulalamika kama wengine na kulaumu mabadiliko haya, au tunaweza kufanya kitu na tukaendelea kukuza biashara zetu licha ya mabadiliko haya yanayoendelea kila siku.
Jambo moja muhimu tunalopaswa kufahamu ni kwamba mabadiliko hayakwepeki, mabadiliko yamekuwepo, yapo na yataendelea kuwepo.
Jambo jingine muhimu sana tunalopaswa kuelewa ni kwamba mabadiliko yanaweza kuwa chanya au hasi, lakini kila mabadiliko, hata yawe hasi kiasi gani, yana faida yake kama mtu anaweza kuyatumia vizuri.
Leo nataka tuangalie namna ya kutumia mabadiliko haya yanayoendelea katika hali chanya, ili tuweze kukuza biashara zetu.
Tunatakiwa kuendesha biashara zetu kwenye misingi ya sheria, fanya kile ambacho unatakiwa kufanya kwa mujibu wa sheria, usijaribu kukwepa wala kutafuta njia ya mkato kama kutoa rushwa, itakuja kukuumiza baadaye.
Tunahitaji kujenga uaminifu mkubwa na wateja wetu, kwa sababu wateja ndiyo wanaotufanya tuendelee kuwepo kwenye biashara, hivyo lazima tujenge nao uaminifu mkubwa ili waendelee kufanya biashara na sisi.
Tuzifanye biashara zetu kuwa sehemu ya maisha ya wateja wetu. Hata kama mambo yatakuwa magumu kiasi gani, bado watu wataendelea kuishi na hivyo wataendelea kuwa na mahitaji muhimu kwenye maisha yako. angalia ni namna gani biashara unayofanya inayafanya maisha ya mteja wako kuwa bora zaidi kila siku na tumia sifa hiyo katika kuwavutia wateja kwenye biashara yako.
Huu ndiyo wakati wa kupunguza gharama za biashara, kwa sababu huenda utapata faida kidogo kuliko ulivyokuwa umezoea. Hivyo pitia upya biashara yako, angalia ni gharama kisia gani unatumia kuendesha biashara yako kwa siku, wiki na mwezi. Kisha angalia ni gharama zipi unazoweza kupunguza ili kuweza kuendesha biashara hata kama faida unayopata ni kidogo.
Tunahitaji kuangalia fursa nyingine zilizopo ambazo zinaendana na biashara zetu. Tusiendelee kufanya kwa mazoea, badala yake tuweze kuangalia kwa jicho la tofauti biashara zetu na tuone ni wapi tunaweza kupatumia na kukuza biashara zetu zaidi.
Tunachohitaji kufanya sisi wafanyabiashara makini siyo kulalamika pekee, hiyo haisaidii, tunahitaji kuangalia ni namna gani tunatumia mabadiliko haya kukuza biashara zetu zaidi. Nyakati kama hizi ndipo wafanyabiashara makini wanaposimama na wale wanaojaribu wanapoishia.
Kila siku fikiria njia bora za kuboresha biashara yako, kila siku vaa viatu vya mteja wako na jiulize kama wewe ungekuwa ndiyo mteja ungeteka nini zaidi. Ongea na wateja wako ujue ni nini hasa wanataka na wapatie, pia jua matarajio yao na yafikie.
Ukuaji wa biashara zetu upo mikononi mwetu, tuchukue hatua sahihi na biashara zetu zitakua.
Nakutakia kila la kheri katika ukuaji wa biashara yako.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Kwa ushauri wa moja kwa moja kuhusu biashara yako kutoka kwangu bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.