Mafanikio ya biashara yoyote yanatokana na falsafa ambayo biashara hiyo inaendeshwa nayo. Ukiangalia wafanyabiashara wengi wanaotokea kwenye nchi ambazo ni za kibepari, wana falsafa tofauti kabisa na wale wanaotokea kwenye nchi za kijamaa.
Nchi za kibepari kama marekani, zina ushindani mkubwa sana wa kibiashara na hivyo watu kujali ubora wa hali ya juu. Katika nchi hizi wafanyabiashara wanahitaji kutoa thamani kubwa sana ili kuweza kuendelea kuwepo kwenye biashara.
Kwenye nchi za kijamaa, watu wanaweza kuridhika na chochote wanachopata, lakini kwenye nchi za kibepari watu wanataka kilicho bora zaidi.
Moja ya falsafa ambazo zimekuwa zinatumika na wafanyabiashara kwenye nchi za kibepari kama marekani katika kuajiri ni hii; AJIRI TARATIBU, FUKUZA HARAKA.
Ili uweze kupata msaidizi bora kwenye biashara yako unahitaji muda. Unahitaji muda kumjua na kuona kama anaendana na biashara yako. unahitaji muda ili kuona ni thamani gani anaweza kuongeza kwenye biashara hiyo. Hili siyo zoezi rahisi na hivyo watu wamekuwa wakijipa muda kuwachunguza watu kabla hawajawaajiri.
Pamoja na kutumia muda huu mwingi kuajiri, wafanyabiashara hawasiti kuchukua hatua haraka pale mfanyakazi anapoleta matatizo kwenye biashara. Iwapo mfanyakazi amekuwa anaumiza biashara badala ya kuisaidia, basi wanawafukuza mara moja. Kwa sababu wanaamini tabia za asili za watu hazibadiliki, na japokuwa kila mtu ana changamoto zake, mwisho wa siku lazima mtu aweze kuongeza thamani kwenye biashara, kama haongezi thamani basi anafukuzwa.
Hii ni falsafa ambayo unaweza pia kuitumia kwenye biashara yako, kwa sababu tatizo la sisi wafanyabiashara tunaotoka kwenye nchi ambazo siyo za kibepari tunakuwa wajamaa sana. Tunaamini watu na kuwaajiri haraka bila ya kufanya uchunguzi wa kutosha. Na tunapowaajiri tunaona kama tunastahili kubeba mizigo yao, hivyo hata kama wanakuwa mzigo kwenye biashara zetu, tunaogopa kuwafukuza kwa sababu tunaona maisha yao yatakuwa magumu.
Tunahitaji kuwa na huruma zaidi kwenye biashara zetu, kwa sababu kumwonea huruma mfanyakazi ambaye atakwenda kuua biashara, ni kujiharibia wewe mwenyewe na wafanyakazi wengine wanaojituma.
Ni muhimu ukajitengenezea vigezo vya kuajiri na kila unayemwajiri ajue anategemewa kutekeleza majukumu gani, kama akishindwa kutekeleza majukumu hayo na akawa hana nia yoyote ya kuweka juhudi basi hastahili kuendelea kuwepo kwenye biashara yako.
Changamoto nyingine ni pale unapoajiri ndugu au watu wa karibu, wanaharibu lakini huthubutu kufukuza.
Kwa biashara yenye mafanikio, tunahitaji kuwa makini sana kwenye kuajiri. Anza sasa KUAJIRI TARATIBU NAKUFUKUZA HARAKA.
Nakutakia kila la kheri katika ukuaji wa biashara yako.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.
Kwa ushauri wa moja kwa moja kuhusu biashara yako kutoka kwangu bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.