Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Unayaonaje maisha yako kadiri unavyojijengea falsafa hii mpya ya maisha? Je unaona yanakuwa bora au yanazidi kuwa hovyo? Kwa sababu lengo kuu la falsafa hii mpya ya maisha ni kutuwezesha kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa. Na kumbuka haya yote yanaanza na wewe mwenyewe, kama utafanya yale ambayo ni sahihi kwako. Tafadhali niambie kuhusu falsafa hii mpya ya maisha kwenye maisha yako.

Karibu kwenye makala yetu ya falsafa mpya ya maisha leo, ambapo tutakwenda kuangalia moja ya maeneo ambayo yamewagusa wengi. Eneo hili ni kuumizwa.

Watu wamekuwa wakilalamika kwamba wameumizwa na wengine, au wamesalitiwa kwa namna ambavyo wengine wamewatendea mambo mbalimbali. Hizi ni hali za kusikitisha kwa sababu kuna watu ambao wameishia kuharibu maisha yao kwa sababu ya kile ambacho wengine wamekifanya.

Huenda hapo ulipo unaamini kabisa ya kwamba makosa ya mtu mwingine yameharibu maisha yako. Au kwa sababu mtu fulani hakutimiza kile ambacho alipaswa kutimiza basi anastahili kubeba lawama zote za maisha yako. utakuta mtu mzima anawalaumu wazazi wake kwamba ndiyo wamesababisha maisha yake yawe hovyo. Wengine wanawalaumu wenza wao, iwe ni wapenzi au wanandoa, watakuambia wamewasababishia kuwa na maisha magumu. Wengine wanawabebesha ndugu zao mizigo ya maisha yao.

Kama ambavyo tumekuwa tunajifunza kupitia kipengele hiki cha FALSAFA MPYA YA MAISHA, maisha yako yako chini yako, kama unataka furaha kwenye maisha basi itaanza na wewe, na kama unataka mafanikio, wewe ndiye wa kuyafanyia kazi ili uyafikie. Hakuna anayeweza kukupa furaha au kukupa mafanikio. Unaweza ukapewa lakini havitadumu kwa muda mrefu, juhudi zako ndiyo zitakazokuletea furaha na mafanikio kwenye maisha yako.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kuumizwa, hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kukuumiza wewe bila ya wewe mwenyewe kutoa ruhusu. Kwa maneno mengine ili uumie unahitaji kutoa ruhusa mtu mwingine aweze kukuumiza. Ubaya ni kwamba hujui kama unatoa ruhusa, ila wewe ndiye unayeruhusu.

Wacha nikupe mfano mmoja mzuri, umewahi kuwa una mahusiano mazuri na mtu, mnakwenda vizuri tu halafu akaja mtu akakuambia mtu yule siku za nyuma alikuwa anakusema vibaya kwa wengine, alisema hivi na hivi (maneno ambayo siyo mazuri). Baada ya kusikia hivyo ukakasirika na kwenda kumvaa mtu yule, au ukaacha kuwa naye karibu? Sasa hebu niambie, hapo ni nani kamuumiza mwenzake? Huyu mtu ulikuwa naye vizuri mpaka siku moja kala hujasikia maneno aliyozungumza siku nyingi zilizopita. Hii ina maana kwamba japo alizungumza maneno hayo ambayo siyo mazuri kwako, hayakukuumiza. Ila umekuja kuumia baada ya kusikia kwamba alisema maneno hayo. Unaona nani kamuumiza mwenzake? Wewe ndiye umejiumiza, kwa kuyachukua maneno na kuyatengenezea njia ya kukuumiza.

Tumekuwa tunatoa ruhusa sisi wenyewe kuumizwa na wengine, halafu wengine wanapofanya kile ambacho wanapenda kufanya, sisi tunaumia. Kitu ambacho wote tunapaswa kujua ni kwamba kila mtu anafanya kile ambacho anaona ni sahihi kwake kufanya. Na kwa kuwa wote hatuko sawa, na pia kwa kuwa kila mtu ana ujinga wake, basi ujinga umekuwa unafanyika pia. Kama watu wanafanya kile ambacho wao wanaona ni sahihi kwao kufanya, na pia kama watu wana ujinga wao, kwa nini kila kitu kikuumize wewe?

Jinsi ambavyo tumekuwa tunatoa ruhusa kwa wengine kutuumiza.

Kama tumeshakubaliana kwamba sisi wenyewe ndio tunawaruhusu wengine watuumize, swali muhimu linakuja tunatoaje ruhusa hii. Kama nilivyosema awali, wengi tunatoa ruhusa tukiwa hatujui kama tumetoa ruhusa. Sisi tutaona tunaishi maisha yetu kama kawaida, lakini tunakuwa tumewapa watu nafasi kubwa ya kutuumiza.

Zifuatazo ni njia ambazo tumekuwa tunawapa watu ruhusa ya kutuumiza.

  1. Kumtegemea mtu au watu kwa kila kitu kwenye maisha yako.

Hii ni hatari kubwa sana na unajiweka kwenye nafasi kubwa sana ya kuumizwa. Kama unawategemea wengine kwa kila kitu kwenye maisha, watu hawa wanapoondoa kile unachotegemea, ni lazima utaumia. Kama umeshayaweka maisha yako kwamba hayawezi kwenda bila wengine kufanya vitu fulani, utaishia kuwa mtumwa wa watu hao.

Utegemezi ninaozungumzia hapa siyo ule wa ushirikiano, bali ule ambao wewe unahitaji zaidi kutoka kwa wengine. Wewe unakuwa mpokeaji zaidi kutoka kwa wengine, na hivyo wanapoacha kutoa, maisha yako yanaathirika.

Kitu cha msingi sana unachotakiwa kufanya kwenye maisha yako ni kujijengea uwezo wa kujitegemea. Hii ndiyo njia kuu unayoweza kutumia kununua uhuru wa maisha yako. ukishaweza kujitegemea hakuna anayeweza kukuumiza, kwa sababu hutakuwa mpokeaji pekee, bali utakuwa mtoaji pia. Hivyo yule anayekupa anapoacha, na wewe unaacha kumpa na kutafuta mwingine anayehitaji, unampa na yeye anakupa. Hivyo ndivyo unavyojenga thamani kwenye maisha yako na kujiepusha na kuumizwa.

  1. Kuwa na matarajio makubwa kutoka kwa wengine.

Njia nyingine ambayo unaweza kuwaruhusu wengine wakuumize ni  kuweka matarajio makubwa sana kwao. Ni kweli tunahitaji kuwa na matarajio kwa wengine, lakini kadiri matarajio haya yanavyokuwa makubwa, ndivyo tunavyowapa nafasi ya kutuumiza, hasa pale wanaposhindwa kutimiza kile ambacho tulitarajia watimize. Pale ambapo ulitegemea mtu afanye kitu fulani, lakini yeye asifanye, au akafanya kinyume unaweza kujikuta unaumia sana. Inapotokea matarajio haya makubwa umeyaweka kwa mtu ambaye unamtegemea kwa kila kitu, ni lazima utaumia sana.

Unachohitaji kufanya hapa ni kutokuweka matarajio makubwa sana kwa watu. Jua kwamba watu wanaweza kufanya au wasifanye kile wanachotakiwa kufanya. Hivyo mara zote kuwa na njia mbadala, iwapo kile unachotegemea hakitakwenda ulivyotegemea basi uwe na njia nyingine ya kufanya. Wape watu nafasi ya kutokufanya kile walichoahidi kufanya. Sisemi kwamba uwaache hata kama ni wazembe, unaweza kuwachukulia hatua, lakini wasikuvuruge wewe na kukuumiza.

  1. Kuwaamini wengine kupita kiasi.

Haijalishi mtu ni nani kwenye maisha yako, kumwamini mtu kupita kiasi ni kujiweka kwenye nafasi ya kuumizwa. Ukweli ni kwamba hatuwezi kuwajua watu kwa undani, hata kama ni watu wa karibu kwetu. Kuna vitu kuhusu watu hatuwezi kuvijua. Mtu anaweza kuonekana hivi akiwa kwenye hali fulani, lakini akabadilika sana akiwa kwenye hali nyingine. Watu watasema mtu amebadilika, ila kiukweli hajabadilika, anaonesha kile kilichopo ndani yake. Na vitu viwili vinavyofanya watu wanaonesha tabia zao halisi ni fedha na mamlaka. Mtu akipata fedha zaidi ya alizokuwa nazo awali, au akipata mamlaka makubwa utaona vitu ambavyo hukuwahi kuviona hapo awali. Unapomwamini mtu kupita kiasi, mpaka unafika hatua ya kumkatalia kwamba hawezi kufanya kitu fulani, kuna siku atafanya na utaumia sana.

Unachohitaji kufanya ni kuwaamini watu lakini siyo kupita kiasi. Mpe kila mtu nafasi ya kukosea au ya kufanya kitu ambacho hukutegemea afanye. Kwa namna hii utaepusha kuumizwa. Hapa sisemi ukubaliane na kile mtu anachofanya hata kama siyo kwa uaminifu, ninachosema ni usishangazwe pale mtu anapofanya tofauti na ulivyotegemea, na hapo unaweza kuamua kuchukua hatua ambayo ni sahihi kwako.

  1. Kuwa na shauku kubwa ya kupata kitu.

Watu wote ambao wamewahi kutapeliwa, wanaonesha kitu kimoja, wanataka sana kile ambacho wametapeliwa nacho. Utasikia mtu ametapeliwa kwa kuambiwa atapewa ajira, kwa sababu alikuwa anataka ajira kwa hamu sana. Au utasikia mtu kadanganywa atapata utajiri kwa njia fulani, kwa sababu alionesha anataka sana utajiri. Kile ambacho unaonesha unakitaka kwa shauku kubwa, ndiyo watu wanachotumia kukuumiza nacho. Na watu wa karibu yako wanajua hili na wamekuwa wakitumia kukunyanyasa. Mtu anapojua kile ambacho unakitaka sana, atakitumia hiko kuhakikisha unafanya anachotaka yeye.

Hapa unahitaji kuwa makini sana na vile vitu ambavyo unavitaka. Usijioneshe kwa wengine kama una uchu sana wa kitu fulani, kwa njia hii watu hawatakuwa na kitu cha kukuumiza au kukunyanyasa.

  1. Kuweka kila kitu chako hadharani.

Siku hizi hakuna kitu ambacho ni siri kwenye maisha ya watu. Hasa ujio wa hii mitandao ya kijamii, watu wanaanika kila kitu kuhusu maisha yao. Wanaweka taarifa zao binafsi kila mahali. Watu wanaweza kutumia taarifa hizi kuwaumiza. Wapo watu wengi wametapeliwa na watu wasiowafahamu lakini wakawa na taarifa zao za kutosha. Hii yote imewezekana kwa sababu mtu mwenyewe anakuwa ameweka mambo yake wazi. Wakati mwingine unaweza kuwa unawaambia watu kuhusu mafanikio yako, kumbe unawaumiza kwa kile unachowaambia, badala ya kukusifia wakajenga chuki na wakatumia mafanikio hayo kukuumiza zaidi.

Kuondokana na hili, jua ni taarifa zipi ambazo unaweza kuwashirikisha watu kuhusu wewe, na zipi ambazo hupaswi kabisa kuwashirikisha watu. Ni lazima uwe na mambo kuhusu wewe ambayo watu wasiohusika hawawezi kuyajua kabisa. Watu wanapokuwa hawana taarifa za kutosha kuhusu wewe, hawawezi kukuumiza. Kwa kuanzia hakikisha taarifa za mahusiano yako, maisha yako ya kifamilia, kipato chako na afya yako siyo taarifa za umma. Usijadili taarifa hizi na watu ambao haziwahusu, hakuna chochote wanachoweza kukusaidia zaidi ya kuwapa nafasi ya kutumia taarifa hizi kukuumiza zaidi. Una matatizo kwenye maeneo hayo jadili na watu wanaohusika au wanaoweza kukusaidia, siyo kuanika kwenye mitandao au kumwambia kila mtu. Watu wanavyojua mengi kuhusu wewe, ndivyo wanavyoweza kutumia vile wanavyojua kukuumiza.

  1. SIRI.

Kitu kingine ambacho kinaweza kutumika kukuumiza ni siri ambazo umewekeana na wengine. Kama kuna kitu ambacho unataka wengine wakifanye kuwa siri, wanaweza kukitumia kukuumiza. Wakati wewe unategemea wasitoe siri hiyo, wanaitoa kwenye nyakati ambazo hata hukuzitegemea.

Ili kuondokana na hili, hakikisha huna siri yoyote. Na kama ni siri hakikisha ni yako mwenyewe, yaani kitu hiko uwe unajua wewe mwenyewe tu. Akishajua mtu mwingine hiyo siyo siri tena, hata kama mtu huyo unamwamini kwa kiasi gani, huwezi kujua ni kwa wakati gani atapitiwa na kutoa siri hiyo. Kama kuna jambo lolote umewahi kufanya na wengine na unahitaji liwe siri, anza kujiandaa jinsi ya kukabiliana nalo litakapokuwa siyo siri tena, au anza kutoa siri hiyo wewe mwenyewe kwa njia ambayo ni rahisi kwako.

Hakuna mtu anayeweza kukuumiza wewe kama wewe mwenyewe hutampa ruhusa ya kufanya hivyo. Wewe ndiye unayewapa watu ruhusa ya kukuumiza, hivyo kama hutaki kuumizwa, ondoa ruhusa hii unayotoa kwa wengine. Fanyia kazi haya tuliyojifunza hapa ili kuwa na maisha ambayo ni bora. Endelea kufanyia kazi falsafa yako mpya ya maisha ili uwe na maisha yenye maana kwako na kwa wengine.

TUPO PAMOJA.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kupata vitabu vya kusoma tembelea(BOFYA) www.mobileuniversity.ac.tz

Kwa ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu tembelea(BOFYA) www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita