Huu ndiyo ule wakati wa mwaka ambapo wahitimu wa elimu ya sekondari kidato cha sita wamepata matokeo ya mitihani ambayo wameifanya. Na katika wakati kama huu kuna makundi makubwa mawili ya watu. Kundi la kwanza ni wale ambao wamefaulu vizuri mitihani yao na hivyo kuwa na sifa za kuendelea na elimu ya juu. Kundi la pili ni wale ambao wamefeli mitihani yao na hivyo kukosa sifa za moja kwa moja kuendelea na elimu ya juu. Nawakaribisha wote kwenye makala hii ya leo kwani kuna mengi muhimu ya kujifunza.

Kwa kuanza nipende kuwapongeza wahitimu wote kwa hatua hiyo kubwa mliyofikia kwenye maisha yetu. Haijalishi kama umefaulu mtihani au umefeli, kuweza kuhitimu kidato cha sita ni hatua kubwa umepiga kwenye maisha yako. kwa hesabu za miaka saba ya elimu ya msingi na miaka sita ya elimu ya sekondari, siyo chini ya miaka 13 umekuwa kwenye mfumo wa elimu. Ni safari ndefu, hongera kwa kuwa mvumilivu mpaka kufikia hatua hii.

Ushauri kwa wale waliofaulu mitihani yao juu ya kozi bora kusoma.
Maswali yanayoulizwa na wahitimu wengi ambao wamefaulu vizuri ni wasome kozi gani ambayo ni nzuri, ambayo itawawezesha kuwa na maisha mazuri. Swali hili kwa sasa lina majibu tofauti na ilivyokuwa miaka mitano iliyopita. Miaka ya zamani kozi za sayansi kama uinjinia na udaktari zilionekana kuwa kozi bora kusoma kutokana na upatikanaji wa uhakika wa ajira na kipato kizuri. Lakini kwa sasa mambo yamebadilika, hakuna tena kozi ambayo mtu akimaliza ajira ni uhakika na hata kipato siyo cha uhakika kama ilivyokuwa ikionekana hapo zamani.

Kujibu swali la kozi ipi bora mtu asome, ni kugumu kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda mambo yanazidi kubadilika.

Mimi Makirita nina ushauri huu muhimu kuhusu kozi bora ambayo wewe mhitimu wa elimu ya sekondari unaweza kusoma. Kozi hiyo ni ile inayoendana na kile unachopenda kwenye maisha yako. chagua kozi ambayo inaendana na vipaji vyako. Hii ndiyo itakuwa kozi bora kwako, kwa sababu utaziona fursa nyingi na nzuri pale utakapohitimu.
Changamoto kubwa inaweza kuwa kwamba mpaka sasa hujajua kipaji chako ni nini. Na hii inatokana na jamii zetu kutokuweka mkazo mkubwa wa mtu kujua na kutumia kipaji chake. Umekuwa unakazana kusoma ili ufaulu, hivyo mengine yote umeweka pembeni.

Kama mpaka sasa hujajua vipaji vyako ni nini basi soma makala hizi na zitakupa mwanga wa vipaji vyako;
SOMA; Jinsi Ya Kugundua Vipaji Vilivyopo Ndani Yako.
SOMA; Jinsi ya kugeuza kipaji chako kuwa biashara inayokuingizia kipato.

Ushauri kwa wale ambao wamefeli mitihani yao na hivyo kukosa sifa za kuendelea na elimu ya juu.
Pole sana kwako kama umefeli mtihani wa kidato cha sita. Napenda nikuambie kitu kimoja, kufeli shule siyo kufeli maisha, sawa najua umeshaambiwa hili mara nyingi lakini huamini kwa sababu wewe ndiyo unajua ni kwa namna gani kufeli kumekuumiza, hasa kama ulikuwa umejiandaa vizuri. Huu ndiyo wakati ambao unahitaji kufanya maamuzi muhimu sana kuhusu maisha yako. huu ndiyo wakati unaohitaji kuamua ni kitu gani hasa unachotaka kwenye maisha yako, sahau zile hadithi za jamii na jiangalie wewe, unataka kufika wapi kwenye maisha yako.

Kama unataka kuendelea na elimu basi chagua ni njia ipi utatumia mpaka kufikia kile kiwango cha elimu unachotaka. Kama unataka kuanza kujitengenezea kipato basi chagua ni njia ipi utakayotumia, ni elimu ipi ya ziada unayohitaji na ni thamani gani ambayo upo tayari kutoa kwa wengine.
Fanya haya sasa, usiendelee kupoteza muda wako kufikiria kwa nini umefeli mtihani, badala yake shika hatamu ya maisha yako na anza kuweka juhudi kwenye lile eneo ambalo umechagua kuchukua hatua.

Ushauri muhimu kwa wote, bila ya kujali umefaulu au umefeli.
Kwa kumaliza kidato cha sita, wewe sasa ni kijana ambaye unaelekea kwenye utu uzima. Kuna mambo muhimu hapa nitakushauri uanze kuyazingatia.

1. Anza kujitegemea wewe mwenyewe kifikra na kimaamuzi. Kama umeshafikisha miaka 21 na kuendelea, jifunze kufanya maamuzi muhimu ya maisha yako wewe mwenyewe. Acha kuangalia wengine wanafanya nini ndiyo na wewe ufanye, badala yake fanya kitu chenye maana kwako.

2. Usifanye kitu chochote kama huna malengo na mipango uliyojiwekea. Usifanye vitu kwa mazoea, au kwa sababu kila mtu anafanya. Fanya kitu unachojua kinakupeleka wapi na jua ni hatua zipi unazotumia kufikia kile unachotaka.

3. Anza kujitengenezea kipato chako mwenyewe. Hata kama unapata kutoka kwa wazazi au kwa njia nyingine kama mkopo wa elimu, jifunze kutoa thamani kwa wengine na uweze kujitengenezea kipato. Kama hujui njia zipi unazoweza kujitengenezea kipato chako soma makala hizi;

SOMA; Biashara Ambazo Mwanafunzi Wa Chuo Kikuu Anaweza Kufanya Bila Kuathiri Masomo Yake.
SOMA; JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG.

4. Chagua sana watu unaohusiana nao, unautumia nao muda wako mwingi. Wanasema ndege wanaofanana huruka pamoja. Na tabia zako ni wastani wa tabia za watu watano wanaokuzunguka. Ni wakati sasa uanze kuangalia ni watu gani unaohusiana nao, marafiki na watu wako wa karibu. Usikae na watu ambao hawajui ni wapi wanakoelekea, usikae na watu wasiojielewa. Chagua sana wale unaotumia nao muda wako. Ni bora uwe na marafiki wachache lakini wenye msaada kwako kuliko kuwa na marafiki wengi ambao wanakupoteza.

5. Jifunze kila siku, KILA SIKU. Iwe utaendelea na masomo au la, kujifunza ndiyo kwanza kumeanza. Unahitaji kujifunza kila siku, kwa kusoma vitabu vizuri, kusoma makala nzuri na kuhudhuria semina na mafunzo mbalimbali. Kusoma habari za udaku na magazeti siyo kujifunza, tenga muda wa kujifunza kila siku. isipite siku bila ya kujifunza kitu kizuri kwenye maisha yako.

6. Chagua falsafa ya maisha yako na ijenge na kuisimamia. Huenda huko ulikotoka ulikuwa unasimamiwa kila kitu na wazazi wako au walimu wako. Sasa hivi umeachiliwa uingie duniani, ambapo kuna kila aina ya changamoto. Huenda hukupata msingi mzuri wa huko duniani unakokwenda. Ili uweze kupona kwenye dunia hii yenye kila aina ya changamoto, unahitaji kuwa na falsafa unayoisimamia kwenye maisha yako. Ni lazima ujiwekee miiko wewe mwenyewe, wa mambo gani utafanya na yapi hutofanya hata iweje. Falsafa yako ndiyo itajenga tabia yako na kuweza kukuvusha kwenye changamoto.

7. Weka juhudi kubwa kwenye chochote unachochagua kufanya. Fanya kama ndiyo kitu pekee unachoweza kufanya. Kwa sasa huna sifa yoyote kwenye dunia hii, sasa ndiyo wakati wa kujijengea sifa. Sifa zinajengwa kwa vitendo, hivyo popote unapopata nafasi ya kufanya kitu, kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana. Watu watakukumbuka kila wakati, na fursa nyingi zitakuja upande wako.

8. Kuhusu kula bata, kuwa makini. Wewe kama kijana unahitaji kupata muda wa kupumzika na kujistarehesha pia. Lakini kuwa makini sana, kuwa makini mno kula kwako bata kusiwe ndiyo kuharibu maisha yako. usipendelee kutumia vileo kama pombe, havina faida kubwa kwenye mwili wako. Usijaribu kabisa kuvuta kitu chochote kile, ni hatari sana kwa afya yako. usithubutu kabisa kutumia madawa ya kulevya, hata udanganywe kwa kiasi gani kwamba unaonja tu, kuna vitu vinaonjwa ila siyo madawa ya kulevya, ni hatari mno.

9. Kuwa mwaminifu, kuwa mwadilifu. Timiza kile ambacho unaahidi, sema ambacho unaweza kusimamia. Mara zote maneno yako na matendo yako viendane.

10. Karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA, ambapo tutakuwa karibu zaidi tukijifunza kila siku kupitia kundi la wasap na makala kwenye blog ya KISIMA CHA MAARIFA. Kujiunga tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 wenye neno KISIMA CHA MAARIFA.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.