Kuna pengo ambalo unalo, kutoka hapo ulipo sasa mpaka kufika kule unakotaka kufika.
Kuna pengo kubwa kati ya unachofanya sasa na ule uwezo wako halisi uliopo ndani yako. pengo kati ya uhalisia na matarajio yako.
Wengi wamekuwa wakiangalia pengo hili na kuliona ni kubwa sana, na hivyo kukata tamaa na kuona haiwezekani. Wanaacha kupunguza pengo hilo na kuamua kufanya mambo mengine.
Lakini hii siyo njia sahihi ya kushughulikia pengo hilo. Kama unataka kitu kikubwa kwenye maisha yako, lazima pengo pia litakuwa kubwa.
Njia bora ya kushughulikia pengo hili ni kutokuangalia pengo lote, badala yake angalia hatua chache za mbeleni. Angalia pale unapoelekea kwa wakati husika. Ukishakuwa kwenye njia sahihi, pengo linazidi kupungua.
Kwa mfano kama lengo lako ni kuwa bilionea na sasa upo kwenye madeni ya kifedha, pengo lako ni kubwa mno. Ukiliangalia unaweza kusema unajidanganya, kwamba utoke kwenye madeni mpaka kuwa bilionea? Kwa kuangalia hivyo unaweza kusema haiwezekani.
Lakini ukiangalia kwa upande mwingine, wala hutaona pengo hilo ni shida. Kwa mfano ukianza na kupunguza madeni, na hiki ikawa ndiyo unachozingatia kwa sasa, baada ya muda utakuwa umeyalipa. Kisha ukaweka nguvu zako kwenye kuanzisha na kukuza biashara yako. Ukaanza kwa kutengeneza faida kidogo, ukaitumia vizuri kwa kuiwekeza tena kwenye biashara hiyo. Ukaendelea kuwekeza maeneo mengine. Kadiri muda unavyokwenda utazidi kuona unakuwa na uhuru wa kifedha.
Kwa njia hii hutatishwa tena na pengo, na badala yake utaweka juhudi zako kwenye kuvuka kile kilichopo mbele yako.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Usipigane Na Usichokitaka Na Jinsi Ya Kupata Unachotaka.
Muhimu zaidi unahitaji muda katika kufika kule unakotaka kufika. Siyo kitu cha kulala masikini na kuamka tajiri, ni kitu cha kuweka miaka ya kutosha ili kufika pale unapotaka kufika.
Lakini kilicho muhimu zaidi ni uifurahie safari, usisubiri mpaka kufika mwisho ndiyo ufurahie, mwisho wenyewe upo mbali sana. Unahitaji kufurahia kila hatua ya safari na hii itakupa hamasa ya kuendelea japo safari itakuwa ndefu.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)