Kabla ya kujenga nyumba, tunajenga kwanza msingi.

Ukitaka kujua uimara wa nyumba, hata kama bado haijakamilika, angalia uimara wa msingi.

Msingi unatupa picha kubwa sana kuhusu nyumba. Msingi ukiwa siyo imara tunajua kabisa ya kwamba nyumba inayojengwa siyo imara, labda ni banda tu.

Kadiri msingi unavyokuwa imara, unavyokwenda chini tuna uhakika nyumba inayojengwa pale itakuwa imara na itadumu kwa muda mrefu.

Misingi pia inatofautiana, msingi wa nyumba ya kawaida hauwezi kuwa sawa na msingi wa ghorofa. Pia msingi wa ghorofa moja hauwezi kuwa sawa na msingi wa ghorofa kumi.

Katika sehemu ambazo mjenzi anapaswa kuwa makini ni kwenye msingi, akiharibu msingi hawezi kurekebisha baadaye ni bila ya kubomoa nyumba nzima. Kama msingi upo imara, akikosea kwingine anaweza kuparekebisha.

Sasa turudi kwenye maisha yetu,

Je ni msingi gani umejenga kwenye maisha yako?

Watu wengi wamekuwa wanakazana kupata mafanikio, wamekuwa wakitamani kufika mbali, lakini hawafiki. Watalalamika kwamba wanajitahidi sana lakini kila wanapofika hatua fulani mambo yanaharibika. Ukiwaangalia watu hawa vizuri unaona kitu kimoja kipo wazi, kukosa msingi.

Hata uwe mchapakazi kiasi gani, kama huna msingi imara hutafika mbali. Hata uwe na malengo makubwa na mipango mizuri kiasi gani, kama huna msingi mzuri uliojijengea kwenye maisha yako, juhudi zote unazoweka zinapotea bure.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Ni Kiasi Gani Cha Fedha Unahitaji Kuwa Nacho Ili Kuwa Na Maisha Bora Na Yenye Furaha?

Tuangalie kwanza msingi ambao tumejijengea kwenye maisha yetu. Je msingi huu unaendana na kule ambapo tunataka kufika?

Unataka kuwa na biashara kubwa na yenye mafanikio, je biashara hiyo umeianzisha kwenye misingi ipi?

Unataka kuwa bilionea, je ubilionea wako unaujenga kwenye misingi ipi?

Misingi ni muhimu sana. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa na misingi ambayo ataisimamia kwenye maisha yake, ambayo itamwezesha kuvuka nyakati za changamoto na aweze kufika kule ambapo amepanga kufika. Bila msingi imara, utapotezwa, kama nyumba isiyo na msingi imara inavyoweza kubomolewa na upepo au maji.

Leo tufanye zoezi la kuangalia misingi yetu kwenye maisha. Kwa chochote tunachopigania, tumekijenga kwenye misingi ipi?

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)