Hizi Ndizo Sehemu Nne (4) Muhimu Za Kuchota Baraka Katika Maisha Yako.

Habari mpendwa Rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? Natumaini hujambo na karibu katika makala yetu ya leo tuweze kujifunza pamoja na hatimaye kuongeza maarifa.
Tukiishi katika maisha ya visasi hatutafika bali tutazaa mauti. Ni vema kusamehe kwa faida yako na kisasi mwachie Mungu apambane na watesi wako. Mtesi wako mwekee kaa la moto kichwani, atembee nalo mwishowe litamchoma. Katika maisha kuna watu ambao wamekuwa miiba katika miili ya watu. Wamekuwa vikwazo kwako, wamekusababishia majeraha ya moyo, wamejeruhi nafsi yako kwa namna moja au nyingine. Hivyo basi, kila mtu atakua amepitia mateso fulani katika maisha yake na kuumizwa sana nafsi yake.

Ili upate furaha ya moyo yakupasa kuondoa uchungu ulioumbika ndani ya moyo wako. Unaondoa uchungu ulioumbika katika moyo wako kwa kusamehe na kuanza maisha mapya. Samehe ili uweze kusamehewa na wala usilipe kisasi kwa mtu aliyekufanyia ubaya bali njia pekee ni kumwachia Mungu apambane na watesi wako. Samehe kwa faida yako wewe mwenyewe.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA

Ndugu mpenzi msomaji, karibu katika makala yetu ya leo tujifunze sehemu za kuchota Baraka katika maisha yako. Kuna mambo mengine huwa unayafanya katika maisha bila kujua kama unajitengenezea mazingira ya Laana au Baraka. Maisha ya laana au baraka unayatengeneza wewe mwenyewe kwa kujua au kutokujua. Zifuatazo ni sehemu nne (4) muhimu za kuchota Baraka katika maisha yako.

1. Mungu; kila mtu ana imani yake ya dini lakini dini ni kiunganishi cha wewe kukutana au kuwasiliana na Mungu.’’ Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu, dunia na watu wote wakaao ndani yake ‘’hakuna mtu aliyejitoa kwa Mungu wake na akakosa kumpa Baraka katika maisha yake. Ukijitoa kwa Mungu kuna faida kubwa maisha yako yatakuwa na Baraka tele na wala sio laana. Kwahiyo, ukitaka kujichotea Baraka jitoe kwa Mungu wako , fanya kwa moyo kazi zake wala hutapungukiwa bali utazidi kuongezewa. Watu wanajisahau kwa kuhangaikia mambo ya kidunia na kumsahau Mungu. Mrudishie Mungu shukurani kwa yale aliyokujalia nawe utabarikiwa.

2. Wazazi; wazazi ni zawadi kutoka kwa Mungu. Hakuna aliyeandika barua azaliwe na mzazi Fulani katika maisha yake. Ukweli ni kwamba wote tumejikuta tumezaliwa na wazazi ambao leo tunao. Unatakiwa kuwaheshimu wazazi wako. Wapokee na wapende kama walivyo hata kama wana udhaifu wapokee kwani ni wazazi wako waliokuzaa. Kuna baadhi ya wazazi ambao kweli walikuwa ni mwiba katika maisha yako lakini huna budi kuwasamehe. Mzazi amepewa mamlaka ya kukubariki au kukulaani hivyo ni vema kuwapenda wazazi wako. Mfano, kuna watu ambao wamewatelekeza wazazi wao bila hata ya kuwasaidia wakiwaacha wakiteseka katika shida wakati wana uwezo wa kuwasaidia.

Watunze wazazi wako, jitoe kwa wazazi na tumia muda na nguvu zako kuwatunza na kuwasaidia wazazi wako ili ujichotee Baraka. Kama usipojitoa kwa wazazi wako na mtoto wako naye hatakuja kujitoa kwako ukiwa mzee kwani atajifunza kupitia wewe kipindi ulikuwa huwathamini wazazi wako. Watunze na wapende wazazi wako wote bila kuwa bagua bila mama usingeweza kupatikana na bila baba usingeweza kupatikana. Kama wazazi wako wamekukosea waombee na mwachie Mungu apambane nao. Tekeleza wajibu wako wote kama mtoto kama ni kufanya kazi basi fanya kwa moyo na kufurahia kazi unazopewa. Kwa hiyo, kwa kujitoa kwa wazazi wako ni njia ya kujichotea Baraka katika maisha yako. Maisha yako yanaweza yasiende kama unakosa kuwatii na kuwaheshimu wazazi wako.

3. Watu Wengine; mwanafalsafa mmoja Zig Ziglar aliwahi kusema hivi ‘’ ukitaka kufanikiwa katika maisha yako saidia watu wengine kupata kile wanachokitaka na wewe utapata kile unachokitaka katika maisha yako’’ hii ni falsafa ya kweli kabisa katika maisha. Kama ulikuwa hujui basi anza leo kuifanyia kazi. Watu wengine ndio wanakusaidia wewe kufikia malengo yako. Huwezi kufanikiwa bila ya watu hivyo basi ni muhimu sana wewe kujenga mahusiano mazuri na watu ili uweze kufanikiwa.
Kumsaidia mtu siyo pesa tu kuna njia nyingi za kusaidia watu. Unatakiwa kuishi maisha ambayo yana msaada kwa watu wengine. Wasaidie watu kupata kile wanachokitaka na wewe unajichotea Baraka tele katika maisha yako. Toa maisha yako kwa ajili ya watu wengine hakika hutapata hasara wala laana bali utajichotea Baraka nyingi katika maisha yako.

4. Familia Yako; kama una familia basi jitoe kwa moyo katika familia yako ili uweze kujichotea Baraka na kufanikiwa katika kazi zako. Hudumia familia yako kwa moyo na kwa upendo. Jitoe kwa familia yako bila kujibakiza kuwa na upendo wa kujitoa kwa ajili ya familia yako. Wasaidie watoto wako, mke au mume wako katika kutatua matatizo yao. Usigeuke kuwa mwiba katika familia yako. Kuna wazazi wengine wanatelekeza familia zao kwa kukwepa majukumu. Ni rahisi kukwepa majukumu yako lakini ni ngumu kukwepa matokeo ya majukumu yako. Kama katika familia yako mnaishi maisha ya paka na panya hakuna amani wala upendo siyo maisha hayo kabisa.
Waswahili wanasema tembo wakipigana nyasi hulia au huumia hivyo basi, wazazi wakigombana na kuwa na magomvi kila siku wahanga wakubwa wa matatizo katika familia ni watoto. Wazazi wakiwa na ugomvi katika familia wahanga wakubwa ni watoto. 

Wazazi wanageuka kuwa kero na vikwazo kwa watoto kwa kujeruhi mioyo ya watoto. Fanya watoto wako wafurahie kuwepo duniani na siyo kujihisi siyo sehemu salama ya kuishi. Unatakiwa kujitoa kwa upendo na kuwa tayari kufa kwa ajili ya familia yako.
Kwa kutamatisha, kama unaweza kujitoa kwa mambo ya kidunia basi, usisahau kujitoa kwa Mungu wako, wazazi wako, familia yako na watu wengine pia ili uweze kujichotea Baraka katika maisha yako. Kama umekosana na mwenzako sameheaneni kwani kusamehe ni kurudisha uhusiano wa awali kati ya mkosewa na mkosa.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: