Safari hii ya kuelekea kwenye mafanikio siyo safari rahisi. Imejaa changamoto na vikwazo vya kila aina. Kuna wakati utajikuta upo njia panda na unaelekea kukata tamaa. Huu ni wakati mgumu sana kwa mtu yeyote yule, na usipokuwa makini wakati huo unaweza kuwa ndiyo mwisho wa safari yako ya mafanikio.

Kitu pekee kinachoweza kutuondoa kwenye hizi hali za kukata tamaa ni hamasa. Unapokuwa na hamasa unaweza kujisukuma kufanya zaidi hata pale unapokuwa mzito kufanya hivyo. Hamasa inakuwezesha kufanya kile ambacho wengine hawawezi kufanya. Hamasa inakutoa kitandani asubuhi na mapema na inakuweka kwenye kazi yako hata baada ya kila mtu kuondoka.

Swali ni je tunapata wapi hamasa hii ili tufanikiwe? Ni nani anayepaswa kutupa hamasa hii?

Jibu unaweza usilipende, lakini hamasa hii ni kazi yako mwenyewe. Wewe ndiye wa kujipa hamasa hiyo itakayokusukuma kufanya. Siyo mwajiri wako, siyo wateja wako wala siyo mwenza wako. Ni wewe mwenyewe, kujua ni kipi hasa unachotaka, kujua inawezekana na kufanyika na kujitoa kukifanya. Kadiri unapokuwa na ndoto kubwa, na imani kwamba inawezekana, unakuwa na hamasa kubwa zaidi. Hakuna anayeweza kukuhamasisha kama wewe mwenyewe hujahamasika.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Why Motivating People Doesn’t Work And What Does. (Sayansi Mpya Ya Hamasa Na Uongozi)

Hamasa ni sehemu ya kazi yako, hivyo unapoweka mipango yako, weka na mpango wa hamasa pia. Mpango huu utakuwezesha kuendelea kuweka juhudi hata pale unaposhawishika kwenda kinyume na mipango yako.

Hamasa kutoka kwa wengine itakusaidia kama tayari una hamasa ndani yako, tofauti na hapo utaona kila kitu hakiwezekani. Fanyia kazi hamasa yako, na utaona mwanga wa kule unakotaka kufika.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)