Ni ukweli uliowaza kila mwanadamu aliye chini ya jua anahitaji kuwa na furaha ya kweli nay a kudumu maishani mwake. Hakuna mtu ambaye haitaki furaha  ya kweli kila mtu huitafuta kwa udi na uvumba na kwa njia anazojua yeye ili mradi zimfikishe kwenye furaha hiyo ya kweli.
Hata pamoja na shughuli nyingi ambazo binadamu anazifanya kila siku za kiuchumi, lakini shughuli hizo ukiziangalia huwa zinalengo jambo moja muhimu sana la kuitafuta furaha ya kweli. Mpaka hapo unaona furaha ya kweli ni kitu cha muhimu na kinatakiwa kulindwa wakati wote pale unapoipata.
Lakini kwa bahati mbaya, wengi huwa wanapotea kwa kufikiri sana kwamba ili uwe na furaha ya kweli ni lazima uwe na pesa nyingi kwanza. Kama ulikuwa unawaza hivyo umepotea. Furaha ya kweli haiji eti mpaka uwe na pesa na mali nyingi. Hilo linatokea vipi? Fuatana na mimi katika makala haya, nikupe njia za uhakika za kulinda furaha yako wakati wote.
1. Ishi sasa.
Njia pekee na nzuri ya kulinda furaha yako wakati wote ni kuamua kuishi sasa na wala sio jana au kesho. Watu wengi wanakosa furaha katika maisha yao kwa sababu ya kujibebesha mizigo mingi kwa wakati mmoja na ambayo inawelemea.
Kwa mfano utamkuta mtu anawaza sana jambo ambalo lilimuumiza sana jana au jambo la kesho ambalo hana uwezo wa kulitawala. Kwa mazingira kama haya inakuwa siyo rahisi kupata furaha ya kudumu. Hiyo inaonyesha ili uwe na furaha lazima uishi sasa kwanza kama vile hakuna changamoto inayokusumbua.
2. Jipende zaidi.
Siri nyingine ambayo unaweza kuitumia na ikakupa furaha ya kudumu ni wewe kuamua kujipenda. Hili unaweza ukalifanya hivi, kwa kuamua kujali afya yako wewe mwenyewe binafsi, lakini hiyo haitoshi hata kwa kupenda pia yale mambo unayoyafanya.
Mara nyingi wengi tunajikosesha furaha halisi kwa sababu ya kutokjipenda wenyewe. Usishangae sana na kujiuliza kivipi mtu anakuwa hajipendi? Hili linaweza kutokea kutokana na jinsi unavyoilinda afya yako. kama unaona afya yako huilindi vizuri, basi ni dalili tosha hujipendi.
3. Kuwa mkweli wakati wote.
Ukweli siku zote unauwezo mkubwa wa kukulinda na kukupa furaha wakati wote. Unapojijengea hulka au tabia ya kuwa mkweli, mara nyingi huo ukweli ni lazima ukupe furaha na uongo unakuwa kinyume chake lazima ukupotezee furaha .
Pengne unajiuliza kwa nini? Subiri kidogo nikwambie. Mara nyingi unapokuwa mwongo kila wakati utajikuta ule uongo unakufunga. Utajikuta ni mtu unaingia migogoro na watu wengi kwa sababu ya uongo. Kwa hali kama hiyo huwezi kuwa na furaha, tofauti na kama ungekuwa mkweli ungejenga furaha ya kudumu sana.
4. Penda familia yako.
Hakuna ubishi katika hili pia furaha ya kweli  inapatikana kutokana na wewe kujali na kupenda familia yako. Huwezi kuwa na furaha ya kweli kama nyumbani kuna mgogoro mkubwa. Kila wakati utakapokuwa ukiwaza familia kama kuna mgogiro litakuumiza sana.
Kwa hiyo iri kubwa hapa ilikudumisha furaha yako, tenga muda wa kufurahia maisha na familia yako. Hakikisha unajenga kila siku upendo kwa mke na watoto wako na kudumisha pia mahusiano na ndugu wengine. Kwa hilo litakusaidia kukupa furaha ya kweli maishani mwako.
5. Tekeleza majukumu yako.
Siku zote jifunze kuwa mtu wa kutekeleza majukumu yako mapema. Kama kuna kuna kazi unaifanya itekeleze mapema. Kwa kifupi, unatakiwa kuwajibika kwa kile unachokifanya bila kuacha. Ukifanya hivyo litakusaidia kuepuka lawama nyingi ambazo utapewa sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yako.
Na kwa sababu ya hilo utake usitake ni lazima litakunyima furaha yako ambayo ungetakiwa kuwa nayo. Kwa hiyo mpaka hapo unaona kumbe siri nyingine ya furaha ya kweli ni kutekeleza majukumu yako kila wakati. kinyume cha hapo ni kujitakia mgogoro wa nafsi na kujikuta kukosa furaha.
Kwa kuzingatia mambo hayo ni msingi mkubwa sana wa kukusaidia kukupa furaha ya kudumu kwenye maisha yako wakati wote.
Endelea kutembelea www.amkamtanzania.comkujifunza na kuhamasika kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,