Wote tunajua ya kwamba ili kufanikiwa kwenye jambo lolote, juhudi zinahitajika. Na tena siyo juhudi tu, bali juhudi kubwa. Hili halina ubishi.

Lakini kuna watu wengi ambao wamekuwa wanaweka juhudi kubwa sana na hawayafikii mafanikio waliyokuwa wanayatazamia. Wapo watu wamefanya kazi siku saba za wiki, miezi 12 ya mwaka kwa zaidi ya miaka 20 lakini hakuna kikubwa wanachoweza kuonesha na kujivunia nacho kwenye maisha yao. Wapo watu ambao wamelima kwa muda mrefu, kila msimu wanalima kwa juhudi lakini maisha yao bado ni magumu sana.

Ni kwa mifano kama hii ambapo watu wamekuwa wakijiridhisha kwamba huhitaji kuweka juhudi kubwa kwenye kazi bali unahitaji kuweka akili kubwa kwenye kazi. Kwa kiingereza wanasema DON’T WORK HARD, WORK SMART.

Upo pia usemi, wa kuchekesha lakini, ya kwamba punda anafanya kazi sana lakini hakuna kikubwa anachopata kwenye amisha yake, simba ni mvivu sana, anapenda kulala lakini ndiye mfalme wa pori.

Ninachoamini ni kimoja, juhudi kubwa inahitajika, kwenye jambo lolote lile, na siyo DON’T WORK HARD BUT WORK SMART, bali WORK HARD AND SMART, unahitaji vyote viwili.

SOMA; Ukiacha Kuweka Juhudi Utajiharibia Hivi…

Hivyo kama unaweka juhudi kubwa lakini bado hupati matokeo uliyotarajia, huenda tatizo siyo juhudi bali unakoelekeza juhudi hizo, au mtazamo wako kwenye hilo unalofanya.

Ni muhimu mara kwa mara kutafakari kile unachofanya, kuona umetoka wapi, uko wapi na unakwenda wapi. Pia kuangalia kama kuna njia bora zaidi ya kufanya. Ni muhimu kila siku, nirudie tena KILA SIKU, uboreshe sehemu ya kile unachofanya. Usifanye tu kwa mazoea, kwa sababu jana ulifanya, bali jiulize leo ni kipi unaweza kuboresha zaidi, hata kama ni kidogo sana, kadiri unavyofanya kila siku ndivyo unavyojijengea mabadiliko makubwa ya baadaye.

Weka juhudi kubwa na maarifa kwenye kila unachofanya, na kila siku boresha zaidi kile unachofanya. Kwa juhudi na maarifa sahihi, ukiwa na mtazamo sahihi, hakuna kinachoweza kukuzuia kupata kile unachotaka.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)