UCHAMBUZI WA KITABU; BRAIN STORM (Jinsi Unavyoweza Kuitumia Akili Yako Kupata Mawazo Bora Na Ya Kibunifu).

Kila mmoja wetu ni mbunifu, tofauti ya wale wanaoonekana ni wabunifu na wale ambao wanaonekana siyo wabunifu ni jinsi wanavyotumia akili zao. Wale ambao wanazitumia akili zako kupata mawazo tofauti na yale yaliyozoeleka wanaonekana kuwa wabunifu. Hakuna ambaye anazaliwa akiwa mbunifu, bali tunatofautiana kwa jinsi tunavyotumia akili ambazo tunazo.

Kila mmoja wetu anahitaji ubunifu kwenye maisha yake. Kuanzia kwenye kazi, biashara na hata maisha ya kawaida, ubunifu ni hitaji muhimu la kuwa na maisha bora na yenye mafanikio. Moja ya njia ya uhakika ya kushindwa kwenye jambo lolote lile ni kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, na kwa mtindo ule ule. Unapokuwa mbunifu unaweza kuja na njia tofauti na bora za kufanya mambo yako, kitu ambacho kitaongeza ufanisi wako.

Mwandishi Jason Rich, mwandishi wa kitabu; BRAINSTORM TAP YOUR CREATIVITY TO GENERATE AWESOME IDEAS AND REMARKABLE RESULTS anatupa mbinu za kuweza kutumia akili zetu kupata mawazo bora na ya tofauti ambayo yatatuwezesha kufikia mafanikio tunayotaka.
Karibu tujifunze pamoja kupitia uchambuzi huu wa kitabu hiki;

1. Ubunifu siyo tabia ya kuzaliwa nayo, yaani hakuna mtu amezaliwa akiwa mbunifu, kama ilivyo hakuna mtu amezaliwa akiwa anajua kusoma. Lakini kila mtu amezaliwa na zana moja muhimu sana katika ubunifu. Zana hii ni akili ambayo kila mmoja wetu anayo. Sasa kama ambavyo ulijifunza kusoma na kuandika, unahitaji kuifundisha akili yako jinsi ya kuja na mawazo ya kibunifu. Hivyo usikate tamaa na kuona wewe siyo mbunifu, bali jua namna ya kujifunza ubunifu.

2. Haijalishi unafanya kitu gani kukuingizia kipato kwenye maisha yako, unaweza kufanikiwa zaidi ya hapo ulipofikia sasa kama utaweza kuitumia akili yako vizuri. Akili yako ni kama mgodi ambao bado hajachimbwa kabisa. Kuna hazina kubwa sana ipi ndani yako. Unachohitaji ni kuiwezesha akili yako kuja na mawazo ya kibunifu, na kinachobaki ni wewe kutumia mawazo hayo kufika kule unakotaka kufika.

3. Ubunifu ni kujiruhusu kufanya makosa. Wengi wetu siyo wabunifu kwa sababu tunaogopa sana kukosea, tunaona tukijaribu kitu tukakosea watu watatucheka. Ubunifu ni kujipa ruhusa ya kufanya makosa mengi, na kisha kujua makosa yapi unaweza kuyatumia vizuri zaidi. Kila kitu unachokiona ni bora, jua kuna mtu alikuja na wazo la kitu hiko, na huenda wazo hilo lilikuwa la hovyo, lakini kwa kuliboresha waliweza kuleta kitu bora.

4. Hakuna mtu ambaye umri wake umempita kwa kuwa mbunifu. Kila mtu anaweza kuwa mbunifu bila ya kujali ana miaka mingapi. Watu wengi wamekuwa wanafikiri ubunifu ni kwa ajili ya vijana. Na hawa ni wale ambao kwa ukubwa wao wanaogopa kukosea na hivyo kufanya mambo kwa mazoea. Watoto wadogo ni wabunifu kuliko watu wazima kwa sababu watoto hawaogopi kuchekwa, hawaogopi kukosea.

5. Mawazo unayohitaji ili kuboresha kazi yako, kukuza biashara yako, kuimarisha familia yako, yote yapo ndani ya akili yako. Mawazo haya kuna mahali umeyafungia na hujaweza kuifikia. Ubunifu ndio utakaokuwezesha kufikia mawazo hayo ambayo tayari unayo.

SOMA; KILA MTU NI MBUNIFU, JE UNAUTUMIA UBUNIFU WAKO KUFIKIA MALENGO YAKO?

6. Kama wewe ni mwajiriwa, hakuna sehemu ambayo mawazo ya kibunifu yanahitajika kama ndani ya makampuni na mashirika. Makampuni na mashirika mengi huwa yanapoteza ubunifu kutokana na ukubwa wake na watu kufanya vitu kwa mazoea. Wewe ukiwa mbunifu unaweza kuja na mawazo ambayo yataboresha zaidi na wewe kunufaika zaidi pia.

7. Kama upo kwenye biashara, hakuna kitu unaweza kufanya kuepuka ubunifu. Unahitaji ubunifu kuwavutia wateja wako, unahitaji ubunifu kuwafanya wateja wanunue zaidi, unahitaji ubunifu kuwafikia watu wengi zaidi. Unahitaji ubunifu kupunguza gharama, unahitaji ubunifu kuongeza ufanisi. Kila siku kwenye biashara yako, ni siku ambayo unahitaji kuwa mbunifu zaidi. Na mawazo haya ya kibunifu yapo ndani yako, siyo kuangalia wengine wanafanya nini uige, bali tumia akili yako na wale wanaokuzunguka kupata mawazo bora.

8. Hatua ya kwanza ya kuwa mbunifu ni kufikiria nje ya boksi. Umekuwa unasikia hili neno FIKIRIA NJE YA BOKSI, lakini maana yake ni nini hasa. Maana halisi ya kufikiria nje ya boksi, ni kufikiria kile ambacho hujawahi kufikiria, kufikiria kama ile hali uliyopo sasa hujaingia bado. Kwa mfano kwenye biashara, ukiwa unafikiria kuongeza wateja, unaanza kufikiria kwa zile njia ulizotumia karibuni. Hapa unafikiria ndani ya boksi. Kufikiria nje ya boksi ni kufikiria kama ungekuwa huna mteja hata mmoja ungetumia njia gani kupata wateja, au kama ungekuwa unafanya biashara nyingine tofauti ungepataje wateja. Hapa unafikiria nje ya boksi na ni rahisi kuja na mawazo ya kibunifu.

9. Ubongo wetu umegawanyika kwenye sehemu kuu mbili, ubongo wa kulia na ubongo wa kushoto. Ubongo wa kushoto unahusika na vitu vya kufikiri vitu kama lugha, mahesabu na mengine yanayohusisha kufikiri, yanafanyiwa kazi kwenye ubongo wa kushoto. Ubongo wa kulia unahusika zaidi na mambo ya burudani na ubunifu. Mambo kama muziki, uchoraji, yanahusika zaidi kwenye ubongo wa kulia. Ili uwe mbunifu, ni muhimu uweze kutumia sehemu hizi mbili za ubongo wako vizuri.

10. Njia ya kwanza ya kuwa mbunifu ni kukataa vitu kama vilivyo. Hakuna kitu kinaua ubunifu kama kukubali kila kitu kama kilivyo na kufanya kwa mazoea. Unahitaji kuwa mpinzani, unahitaji kujikatalia hata wewe mwenyewe mara kwa mara. Unapojikuta unafanya kitu leo kwa sababu jana ulifanya, ni wakati mzuri wa kujiuliza kwa nini unafanya hivyo, je hakuna njia nyingine za kufanya?

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kutoka Kwenye Kitabu Cha The Truth About Innovation (Ukweli Kuhusu Uvumbuzi)

11. Ili kuwa mbunifu, mazingira yanahusika sana. Ni vigumu kuwa mbunifu kama upo kwenye eneo ambalo linakuletea msongo wa mawazo. Hivyo pale unapotaka kufanya zoezi la kupata mawazo ya kibunifu, tafuta eneo ambalo lina utulivu na linakufanya ujisikie vizuri. Inawezekana unapendelea eneo tulivu kabisa, au unapendelea muziki wa sauti ya chini. Jua mazingira yanayoendana na wewe na yatengeneza ili uyatumie kuwa mbunifu.

12. Unahitaji kuujua mwili wako mwenyewe, watu tunatofautiana kwenye nguvu za miili yetu kulingana na muda wa siku. kuna watu ambao wanakuwa wabunifu sana wakati wa asubuhi, wengine jioni wengine usiku wa manene. Wale wa asubuhi watadamka mapema wakati wale wa usiku wa manane watakesha. Jua ni wakati gani bora kwako na upange shughuli zako katika muda ule. Pia uzuie usumbufu kwenye muda huo.

13. Unaweza kufanya zoezi la kuja na mawazo ya kibunifu ukiwa mwenyewe au ukiwa na kikundi cha watu. Kila njia ina faida na hasara zake. Unapofanya mwenyewe unakuwa na uhuru zaidi lakini pia unakosa mawazo ya tofauti, unaweza kuishia na mawazo ambayo siyo tofauti sana na yale uliyonayo sasa. Unapofanya zoezi hili na kikundi cha watu, unapata faida ya kupata mawazo tofauti tofauti lakini una hasara ya kutumia muda mwingi na wakati mwingine kukatishana tamaa baina ya wale wanaohusika na kuja na mawazo ya kibunifu.

14. Unapofanya zoezi la kuja na mawazo ya kibunifu, kwanza jua ni kitu gani unataka kutatua, anza na tatizo. Kisha jipe muda wa kuja na mawazo hayo, usijiwekee ukomo wa muda, bali jiwekee ukomo wa mawazo. Usiseme nataka baada ya saa moja niwe nimepata wazo bora, badala yake jiwekee kwamba unahitaji kuondoka na wazo bora. Wakati unatoa mawazo au wengine wanatoa mawazo, usianze kuhukumu mawazo. Hata kama wazo linaonekana ni la kijinga kabisa, wacha mawazo yabubujike, baadaye mtachambua wazo moja moja.

SOMA; HII NDIO SABABU KUU YA WEWE KUTOFURAHIA MAISHA YAKO.

15. Angalia vitu kwa jicho la tofauti, hii ni njia moja muhimu ya kutumia wakati unafanya zoezi la kupata mawazo ya kibunifu. Angalia vitu kwa upande tofauti, jiulize kama ungekuwa upande mwingine ungeteka nini. Kwa mfano kama unataka kuongeza wateja wa biashara yako, jiulize kama wewe ungekuwa mteja ungetaka kupata nini? Je kama ungekuwa mshindani wa biashara yako, ungefanya nini ili kupata wateja wengi zaidi. Fikiria kwa njia hizo na utakuja na mawazo mengi.

16. Tumia milango yako yote mitano ya fahamu kuja na mawazo tofauti, tumia kuonja, kunusa, kusikia, kuona na kuhisi kuna na mawazo tofauti kwenye kile ambacho unataka kuongeza ubunifu wako. Kadiri unavyotumia milango yako ya fahamu, ndivyo unavyoona njia tofauti za kufanya kitu. Jiulize unataka watu waone nini, wasikie nini, wahisi nini, wapate ladha gani.

17. Uliza maswali, hoji sana. Hii ni njia ambayo itakuwezesha kupata mawazo ya kibunifu kutoka kwako na kwa wengine. Unapokutana na watu waulize maswali mengi ambayo yatakuwezesha kujifunza kupitia wao. Jihoji wewe mwenyewe kwenye kila unachofanya na utaona mawazo ya tofauti yanakujia. Kama hujui wapi uanzie kuuliza maswali kwa wengine, anza na maswali haya sita ya msingi sana.
Swali la kwanza ni NANI (WHO), anza swali lolote na nani….
Swali la pili ni NINI (WHAT), unaweza kuanza swali na nini….
Swali la tatu ni KWA NINI (WHY), uliza kwa nini kitu kipo kama kilivyo.
Swali la nne ni WAPI (WHERE), anza kuuliza wapi….
Swali la tano ni VIPI (HOW), uliza ni jinsi gani kitu kinafanyika.
Swali la sita ni LINI (WHEN), anza kwa kuuliza lini…

18. Anza na VIPI KAMA (WHAT IF). Moja ya njia unazoweza kutumia kupata mawazo ya kibunifu ni kujiuliza swali VIPI KAMA kwenye kile ambacho unakiona au kukifanya. Kama umemwona mbwa jiulize vipi kama mbwa angekuwa na miguu mitano, vipi kama angekuwa anataga, vipi kama asingekuwa na manyoya, jiulize maswali kama haya na jipe majibu, utaona akili yako unaanza kupata mawazo ambayo hujawahi kupata awali. Uzuri wa njia hii ni kwamba unaweza kuitumia popote. Hebu anza kuitumia hapa unaposoma hivi, jiulize vipi kama mimi ndiyo ningekuwa nimeandika haya, ningewezaje kuyatumia kwenye kazi yangu au biashara yangu, na je ni njia gani nyingine naweza kutumia kupata matokeo unayotaka kupata. Iruhusu akili yako ije na mawazo mengi uwezavyo.

SOMA; Mbinu 5 Zitakazokufanya Uwe Mbunifu Zaidi.

19. Ukishapata mawazo mengi kwa njia hii ya kuruhusu akili yako ibubujike na mawazo, sasa unahitaji kuyachambua mawazo hayo ili uone ni wazo lipi unaweza kulitekeleza. Katika kuchambua mawazo uliyopata, tumia njia hii ya utatu kuchambua kila wazo. Andika wazo kwenye karatasi kisha gawa safu tatu, safu ya kwanza andika faida, safu ya pili andika hasara na safu ya tatu andika madhara. Kisha orodhesha kila kitu kwenye safu yake, andika faida zote za wazo hilo, andika hasara zake na kisha andika madhara ya wazo hilo. Mwisho oanisha safu hizi tatu na ona wazo hilo linafaa kutekelezwa au la.

20. Ukishapata wazo ambalo unaweza kulitekeleza, kinachobaki ni wewe kulifanyia kazi wazo hilo ili uweze kupata kile ambacho unataka kupata. Unahitaji kuweka juhudi kubwa ili kuweza kufanikisha wazo lolote.

21. KITU KIMOJA MUHIMU CHA KUONDOKA NACHO KWENYE KITABU HIKI; Kama utasahau kila kitu kwenye kitabu hiki basi ondoka na kitu hiki muhimu na kitumie kwenye maisha yako ya kila siku; wewe ni mbunifu, kiungo kikuu cha ubunifu ulichonacho ni akili yako, kama unataka kuwa mbunifu, usiogope kukosea. Mwisho kabisa, tumia maisha yako ya kila siku kupata mawazo mapya na ya kibunifu, kila unachopitia, jifunze.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.
Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s