Kile ambacho baadhi ya watu watakuchukia nacho, ndiyo hicho hicho ambacho baadhi ya watu watakupenda nacho. Kwa lugha rahisi kwa jinsi ulivyo na kwa vile unavyofanya, kuna watu ambao watakupenda na kuna ambao watakuchukia.
Ukiwa mwaminifu kunwa watu ambao watakupenda kwa uaminifu wako, vile vile wapo watakaokuchukia kwa uaminifu wako, hasa pale utakapowakatalia kile wanachotaka, ambacho siyo cha uaminifu.
Ukiwa mwongo wapo watakaokupenda kwa uongo wako, na pia wapo watakaokuchukia kwa uongo wako. Wale ambao wananufaika na uongo wako watakupenda, ila wale wasionufaika watakuchukia.
Ukiwa mchapa kazi wapo ambao watakupenda kwa uchapakazi wako, hasa pale unapowasaidia moja kwa moja. Lakini pia wapo ambao watakuchukia kwa uchapakazi wako, kwa kuwa unawaonesha wao siyo wachapa kazi.
Funzo tunaloondoka nalo hapa ni lipi?
Kwamba watu watakupenda au kukuchukia kwa sababu zao binafsi, kama wananufaika au wanaumia kupitia kile unachofanya.
Kwa kuwa tunajua huwezi kumridhisha kila mtu, hivyo siyo vyema kuangalia nani atakupenda au kukuchukia kwa kile unachofanya, badala yake angalia ni kipi sahihi kwako kufanya na kifanye. Chochote utakachochagua kufanya, utapata watakaokupenda na watakaokuchukia.
FALSAFA MPYA YA MAISHA; Njia Ya Uhakika Ya Kuwafanya Watu Wakupe Kile Unachotaka.
Mara zote fanya kile kilicho sahihi, na wanakuelewa mtakwenda pamoja, wasiokuelewa wataendelea kukuchukia, usijali, hiyo siyo juu yako, ni juu yao wenyewe. Wewe fanya kilicho sahihi na kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana. Na unapofanya kwa ubora wa hali ya juu sana, wanaokupenda wanazidi kukupenda, na wanaokuchukia wanazidi kukuchukua, lakini kumbuka hiyo siyo juu yako, ni juu yao wenyewe.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)