UCHAMBUZI WA KITABU; COACH YOURSELF TO WIN (Hatua Saba Za Kufikia Ufanisi Mkubwa Kwenye Kazi Na Maisha Yako Kwa Kuwa Kocha Wako Mwenyewe)

Kuna siri moja ambayo wachezaji wa michezo mbalimbali wanaijua na kuitumia ambayo wengine hawaijui au wanaijua lakini hawaitumii. Siri hii ni kuwa na mtu wa kukufuatilia kwenye kile unachofanya, na mtu huyo siyo tu anakufuatilia juu juu bali anakufuatilia kwa karibu, kukuonesha hatua muhimu ya kuchukua na kukuonesha ni wapi unapokosea. Mtu huyu anaitwa KOCHA. Karibu kila mchezo mchezaji anakuwa na KOCHA, hata michezo ya mchezaji mmoja mmoja kama masumbwi, watu hawa wanahitaji kuwa na KOCHA.

KOCHA siyo tu mwalimu kwamba anamfundisha mchezaji mbinu za ushindi, bali anamsimamia mpaka aweze kufikia kile anachotaka.
Kila mtu kwenye maisha yake anahitaji kuwa na KOCHA, kwa sababu siyo rahisi kujisimamia mwenyewe. Unaweza kuweka malengo na mipango mizuri lakini ukashindwa kuifikia kutokana na kukosa mtu wa kukusimamia kwa karibu. Unahitaji kuwa na KOCHA kwenye kazi yako, biashara yako na hata maisha yako kwa ujumla. Kocha atakusukuma uchukue hatua hata pale unapokaribia kukata tamaa.

Lakini pia siyo watu wote wanaweza kumudu gharama za kuajiri mtu awe kocha kwenye maisha yao, au hata kama wanamudu huenda hawana muda wa kukutana na kocha. Kuna habari njema kwa watu hawa, kwamba wanaweza kuwa MAKOCHA WAO WENYEWE. Wao wenyewe wanaweza kujisimamia mpaka wakaweza kufikia malengo na mipango yao kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla.
Mwandishi Howard Guttman anatupa hatua saba za kuweza kuongeza ufanisi wetu kwenye kazi na maisha kwa ujumla. Karibu tujifunze mbinu hizi sana kwenye uchambuzi wa kitabu hiki COACH YOURSELF TO WIN.
Karibu tujifunze kwa pamoja.

MAMBO MATATU MUHIMU UNAYOHITAJI KABLA HUJAWA KOCHA WAKO MWENYEWE.

Kabla hatujaingia kwenye hatua saba za kuongeza ufanisi wako kwa kuwa kocha wako mwenyewe, kuna mambo matatu muhimu unahitaji kuwa nayo ili uweze kuwa kocha wako mwenyewe.
MOJA; Unahitaji kuwa na taarifa sahihi za pale ulipo sasa na kule unakotaka kufika. Bila ya kujua ulipo na unapokwenda hutaweza kutoka hapo na hata ukitoka hutajua ni njia hani uchukue.
PILI; Unahitaji kuwa MWONGOZO, hapa unahitaji mtu au watu ambao watakuwa wanakuangalia na kukufatilia.
TATU; Unahitaji kuwa tayari kwenda nje ya mazoea yako, unahitaji kuwa tayari kufanya vitu ambavyo hujawahi kufanya, uchukue hatua ambazo ni hatari na ambazo huna uhakika nazo.

SOMA; KITABU CHA MAY; Biashara Ndani Ya Ajira; Jinsi Ya Kuanzisha Na Kukuza Biashara Yako Ukiwa Bado Umeajiriwa.

Zifuatazo ni hatua saba za kuongeza ufanisi wako kwa kuwa kocha wako mwenyewe;

HATUA YA KWANZA; JE UNAWEZA KUWA KOCHA WAKO MWENYEWE.
Kabla hujaamua kuwa kocha wako mwenyewe ni lazima ujiulize kama unaweza kuwa kocha wako mwenyewe. Ili kujua kama unaweza kuwa kocha wako mwenyewe.

1. Ili uweze kuwa kocha wako mwenyewe unahitaji vitu vitatu; unahitaji kuwa na uwezo wa kubadilika, uwe tayari kubadilika na uwe na nia ya kubadilika. Unahitaji kujua kwamba zoezi la kubadilika linahitaji muda, siyo kitu cha haraka hivyo unahitaji kujipanga ili kufikia mabadiliko ya kweli.

2. Ili kuwa kocha wako mwenyewe unahitaji kubadili tabia zako na kufanya mabadiliko ya kudumu. Watu wengi hubadili tabia zao lakini baada ya muda mfupi hujikuta wamerudi tena kwenye tabia hizo. Hii ni kwa sababu wanakuwa hawajafanya mabadiliko ya kudumu kwenye tabia zao, bali wanakuwa wamebadili mbinu zao.

SOMA; USHAURI; Biashara Nzuri, Inayolipa Na Unayoweza Kuifanya.

3. Ili uweze kuwa kocha wako mwenyewe, lazima uwe na maelezo sahihi kwa tabia zako. Kwa ile tabia uliyonayo, usijichukulie wewe kama ndiyo ile tabia, badala yake jichukulie wewe ni wewe na tabia ni tabia, kwa njia hii inakuwa rahisi kubadilika. Kwa mfano usijiite mlevi, bali jiite mtu ambaye anakunywa pombe mara nyingi au kupita kiasi. Ukijiita mlevi maana yake umejipa utambulisho ambao utaendelea kuwa nao. Ila ukijiita mtu anayekunywa pombe mara nyingi au kwa wingi, unaweza kuanza kupunguza kiasi unachokunywa na hatimaye kuondokana kabisa na tabia ya kutumia pombe.

4. Tatizo lolote unalokutana nalo kwenye maisha yako, kuna namna ambavyo umechangia tatizo hilo, hivyo katika kuwa kocha wako mwenyewe, jiulize mchango wako ni upi kwenye kila unachopitia, hii inakupa nafasi ya kujua kipi hasa cha kubadili. Kama utawalaumu wengine pekee, hutaweza kutoka hapo ulipo sasa.

HATUA YA PILI; PANGA NIA YAKO (KUSUDI LAKO).
Ili kuwa kocha wako mwenyewe kwenye kubadili tabia zako, ni lazima uwe na NIA au KUSUDI kwa nini unataka kufanya mabadiliko kwenye maisha yako. nia ndiyo itakayokusukuma kuchukua hatua na kukufanya uendelee kuweka juhudi hata pale mambo yanapokuwa magumu.

5. Weka nia yako kwa nini unahitaji kufanya mabadiliko kwenye maisha yako, nia hii iwe inakuvutia kuchukua hatua. Kwa nini unataka kupunguza uzito? Kwa nini unataka kuacha kuvuta sigara? Kwa nini unataka kuongeza ufanisi wako kwenye kazi? Fikiria jinsi utakavyonufaika na mabadiliko utakayoleta kwenye maisha yako.

6. Ni hadithi gani ulizonazo sasa kuhusu maisha yako na kile unachofanya. Kila mmoja wetu ana hadithi ya maisha yake, kwa vile anavyofikiri yapo na vile wengine wanavyomchukulia. Huwa tunaishi kadiri ya hadithi za maisha yetu. Jua ni hadithi gani unayoishi sasa na jinsi inavyokuzuia kubadilika.

7. Tengeneza hadithi mpya ya maisha yako. Hapa tengeneza hadithi itakayoendana na mabadiliko unayoleta kwenye maisha yako. Tengeneza hadithi ambayo itaendana na mabadiliko unayotaka kwenye maisha yako, itumie hadithi hiyo katika kukupa hamasa ya kuweka juhudi zaidi kwenye maisha yako.

HATUA YA TATU; CHAGUA WATU WA KUKUONGOZA NA KUKUSAIDIA.
Unapokuwa kocha wako mwenyewe, hatari kubwa ni kurudi nyuma. Pale unapojiwekea malengo na mipango yako mwenyewe, unapoanza kuifanyia kazi na ukakutana na changamoto ni rahisi kukata tamaa. Lakini unapokuwa umewaambia wengine kuhusu mipango yako, watakuwa wanakuuliza umefikia wapi. Hivyo hitaji kubwa la kuwa kocha wako mwenyewe, ni kuwaambia watu unaowaamini yale malengo na mipango yako.

8. Chagua ni watu gani ambao watakuwa kwenye timu yako ya kukufuatilia kwenye utekelezaji wa malengo na mipango yako. Ni lazima uwe na vigezo vya watu unaowaambia kuhusu nia yako. Siyo kila mtu anafaa kuambiwa, wengine wanaweza kukukatisha tamaa. Baadhi ya vigezo vya kuzingatia kwenye kuchagua watu wa kukusimamia ni hivi;
Wawe ni watu unaowaamini na wanakuamini wewe pia.
Wawe ni watu ambao wanajali kuhusu mafanikio ya maisha yako.
Wawe ni watu ambao wana muda wa kukufuatilia.
Wawe ni watu ambao wapo tayari kukuambia ukweli bila ya kuona aibu.

9. Jadili NIA yako ya kubadilika au kufikia malengo yako na wale watu ambao unataka wakufuatilia. Wajulishe ni wapi ambapo unataka kufika, wape mtiririko mzima na wape maeneo ambayo itakuwa rahisi kwao kukufuatilia wewe.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

10. Wakati mwingine unaweza kujiunga na kikundi cha watu ambao wanafanyia kazi mabadiliko kama ambayo unayafanyia kazi wewe. Kwa mfano kuna vikundi vya watu wanaotaka kuacha kutumia pombe, au wanaotaka kuacha matumizi ya madawa ya kulevya. Angalia ni tabia gani unataka kubadili, au malengo gani unataka kufikia kisha angalia kama kuna kikundi cha watu wanaofanya kama unavyotaka kufanya wewe. Faida ya kuwa kwenye vikundi vya aina hii ni kwamba unajifunza moja kwa moja kutoka kwa wengine waliofanikiwa kufanya unachotaka kufanya.

HATUA YA NNE; POKEA MREJESHO.
Ukishakuwa na kikundi cha watu ambao wanakufuatilia kwenye malengo na mipango yako, unahitaji kuwa tayari kupokea mrejesho kutoka kwao. Mrejesho huu ndiyo utakaokupa mwelekeo kama upo kwenye njia sahihi au la.

11. Jifunze kupokea mrejesho hata kama siyo mzuri. Moja ya tabia zetu binadamu ni kupenda kujitetea, hasa pale watu wanapotuambia madhaifu yetu, huwa tunakazana kutoa sababu za kuonesha kwamba siyo madhaifu yetu. Unahitaji kuwa tayari kupokea mrejesho hata kama ni hasi na kuweza kuutumia kuboresha zaidi kile unachofanya.

12. Kuwa msikilizaji zaidi kuliko mwongeaji, unahitaji kusikiliza siyo tu kwa masikio, bali kwa mwili wako wote. Watu wanapoongea wanatoa ishara nyingi unazoweza kujifunza zaidi kutoka kwao. Sikiliza kwa makini.

13. Wafanye watu wakueleze zaidi kuhusiana na wewe na mwisho washukuru kwa kukupa mrejesho huo. Wahoji zaidi ili waweze kujieleza kwa jinsi wanavyokuona wao. Mwishoni washukuru ili waendelee kukupa mrejesho zaidi. Usikasirike wala kuwachukia, badala yake pokea kile wanachokuambua.

HATUA YA TANO; CHAKATA NA JIBU MREJESHO.
Ukishapewa mrejesho na wengine, kuhusu hatua unazochukua na malengo ambayo unayo, unahitaji kuchakata mrejesho huo na kisha kujibu yale ambayo ni muhimu.

14. Jiulize kuhusu mrejesho uliopewa na wengine, je unaendana na vile unavyojiona ndani yako? jiulize je ni kwa namna gani umekuwa unafanya mpaka watu wanakuona wanavyokuona. Pia jiulize ni mambo gani unahitaji kubadili ili uweze kuwa kwenye uelekeo sahihi.

15. Waahidi watu ni kipi utakachobadili ili uweze kufika kule unakotaka kufika. Kwa njia hii inakuwa rahisi watu kuona kama kweli una dhamira ya dhati ya kubadilika au kufikia malengo yako.

HATUA YA SITA; TENGENEZA MPANGO KAZI.
Umeshakuwa na nia ya kubadilika au kufikia malengo yako, umeshachagua watu wa kukufuatilia na umeshapata maoni yao, sasa kinachofuata ni kuwa na mpango kazi. Hapa unahitaji mpango ambao utaufanyia kazi ili uweze kufikia malengo yako au kubadili tabia zako.

16. Tengeneza mpango wa maendeleo binafsi (PERSONAL DEVELOPMENT PLAN). Mpango huu unakuwa na hatua utakazochukua ili uweze kufikia NIA yako ya mabadiliko, unakuwa na muda unaohitaji na kipi utafanya kwenye muda wako. Pia unakuwa na changamoto unazoweza kukutana nazo na zikakurudisha nyuma na njia ya kuzitatua.

17. Kutengeneza mpango siyo kujaribu kuitabiri kesho yako au kuitengeneza bali ni kujaribu kuiumba kesho yako. Hakuna awezaye kutabiri nini kitatokea kesho, lakini wote tunajua kuna mambo mengi sana yanayoweza kutokea kesho. Je katika hayo mengi yanayoweza kutokea yapi ambayo ni muhimu kwako kufanyia kazi? Hii ndiyo kazi ya kuweka mipango, kuchagua kipi kitakuwa kipaumbele kwako.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha YOU CAN WIN (UNAWEZA KUSHINDA)

18. Kupanga siyo rahisi, inahitaji ufikiri kwa kina na uwe na ubunifu mkubwa. Na pia mara nyingi mipango yako haitakwenda kama ulivyopanga. Ni muhimu kujua hili ili uwe tayari kuchukua hatua. Kwa vyovyote vile unahitaji kuwa na mpango, kwa sababu KUHINDWA KUPANGA NI KUPANGA KUSHINDWA.

HATUA YA SABA; FANYIA KAZI NA JITATHMINI.
Ukishakuwa na mipango kilichobaki ni utekelezaji wa mipango hiyo. Na siyo tu kutekeleza bali kuendelea kujitathimini ili kuona kama unaendelea kuwa kwenye njia sahihi.

19. Chagua hatua utakazochukua kila siku ili kuweza kubadili maisha yako au kufikia malengo yako. na njia nzuri ya kufanya hivi ni kugawa mambo yako kwenye hatua ndogo ndogo unazoweza kupiga kila siku. Hata kama mabadiliko unayotaka kufanya ni makubwa, usiangalie ukubwa na ukakutisha, badala yake angalia ni hatua hani unayoweza kuchukua kwenye siku yako ili kufikia mabadiliko unayotaka. Kama lengo lako ni kufanya mazoezi basi unaweza kuanza kwa kukimbia hatua chache kila siku, au kupiga pushup kumi kila siku. lengo ni kuanza na kuendele akufanya.

20. Hatari kubwa inayowapata wengi ni kurudi kule walikotoka baada ya kufanikiwa. Watu wengi wanaopanga kupunguza uzito huwa wanafanikiwa kuupunguza lakini baadaye uzito huo unarudi tena maradufu. Au watu wanafanikiwa kukuza baishara zao lakini baadaye zinaporomoka. Hii inatokana na kujisahau na kuanza kurudia zile tabia za zamani ambazo walishaziacha. Unahitaji kujitathmini kila siku kama hatua unazochukua zinaendana na mabadiliko unayotaka au malengo unayoyaendea.
Sasa umeshapata hatua zote saba za kuwa kocha wako mwenyewe, zifanyie kazi hatua hizi na maisha yako yatakuwa bora sana.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.
Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: