Watu wengi wamekuwa wanafikiri kwamba kuweza na kufanya ni kitu kimoja, na hivyo kuona kama wanaweza basi hata kufanya siyo shida.
Utawasikia watu wakiwaangalia wale waliofanikiwa na kusema hata mimi naweza kufanya kama yeye. Sasa swali linakujia kama unaweza kufanya kwa nini na wewe hujawa kama yeye ambaye amefanikiwa?
Hapa ndipo unapopata majibu kwamba kuweza tu siyo kitu, mafanikio yapo kwenye kufanya, na siyo kufanya mara moja pekee, bali kufanya tena na tena na tena na tena. Siyo kwamba kufanya huku kuna mteremko, bali unafanya tena na tena hata pale unapokuwa umeshindwa kila unapofanya.
Kabla hujamwangalia anayefanya vizuri na kusema hata mimi naweza kama yeye, jiulize je upo tayari kufanya? Upo tayari kuweka juhudi za ziada kwa muda ambao ungekuwa unapumzika? Upo tayari kufanya tena hata baada ya kushindwa? Haya ndiyo maswali yatakayokupa dalili kama kweli na wewe utafanikiwa au la.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; DEEP WORK (Mbinu Za Kufanya Kazi Yenye Maana Kwenye Zama Hizi Za Usumbufu).
Kuweza pekee hakuna maada mkubwa, mafanikio yapo kwenye kufanya, kwenye kuweka juhudi kubwa na kutokukata tamaa.
Kufanya kunahitaji utayari na msukumo kutoka ndani ya mtu mwenyewe. Kunahitaji uvumilivu na kutokata tamaa, hakuhitaji maneno mengi bali vitendo. Kuwa mtu wa kufanya, na siyo mtu wa kusema unaweza kufanya. Kila mtu anaweza kusema anaweza kufanya, lakini ni wachache ambao wapo tayari kufanya, na hawa ndiyo wanaofanikiwa. Kuwa mmoja wa hawa wachache ili na wewe ufanikiwe.
Kipi kikubwa unafanya leo?
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)