Katika safari hii ya maisha ya mafanikio, kuna vitu vingi sana ambavyo unahitaji kujifunza. Hii ni kwa sababu hukupata nafasi ya kufundishwa ulipokuwa shuleni, na wala hujapata nafasi hiyo kwenye malezi yako. hivyo hili linabaki kuwa jukumu lako mwenyewe kwa sababu wewe ndiye unayetaka kufanikiwa.
Baadhi ya vitu muhimu sana unavyopaswa kujifunza na kuvijua vizuri kwenye maisha ya mafanikio ni uongozi (leadership), jinsi ya kuuza (sales), namna ya kutangaza kitu (marketing), usimamizi wa fedha (financial management).
Njia bora kabisa ya kujifunza vitu hivi muhimu ni kwa kufanya. Kusoma ni muhimu lakini huwezi kusoma kila kitu unachopaswa kujua ndipo uingie kwenye kufanya, badala yake fanya huku ukiendelea kujifunza zaidi. Unapokutana na changamoto rudi kwenye vitabu na pia ongea na wale waliofanikiwa kwenye hicho unachofanya.
Kama unataka kujifunza uongozi anza kuchukua nafasi za uongozi pale unapozipata, utapata nafasi nzuri ya kujifunza kwa kufanya. Chukua uongozi kwenye taasisi za kijamii na hata kwenye jamii kwa ujumla. Labda kanisani kwenu anahitajika mwenyekiti wa kamati fulani, jitokeze kwenye nafasi kama hizo, au mtaani kwenu anahitajika kiongozi, chukua nafasi hiyo. Faida ya kujifunza uongozi kwa kufanya ni kwamba unakutana na changamoto moja kwa moja na hivyo unaanza kujifunza namna ya kuzitatua.
Kama unataka kujifunza namna ya kuuza kitu au kutangaza kitu, basi tafuta bidhaa au huduma ambayo unaona inaweza kuwanufaisha watu lakini haijawafikia wengi. Angalia namna unavyoweza kuitangaza na kuuza bidhaa hiyo na hapo anza kuitangaza na kuiuza. Wakati unafanya hivi utakuwa unajifunza mengi sana kuhusu kuuza na kutangaza. Kila unapokutana na changamoto ndiyo wakati wa kurudi na kujifunza namna ya kuondokana na changamoto hiyo.
SOMA; RICH DAD; Jifunze Kuifanya Fedha Ikufanyie Wewe Kazi.
Kama unataka kujifunza kuhusu usimamizi na udhibiti wa fedha, anza na fedha zako mwenyewe. Hakikisha unazisimamia na kudhibiti vizuri, utajifunza mengi.
Njia moja ya uhakika kabisa ambapo utajifunza yote hayo kwa pamoja ni kuanzisha biashara yako mwenyewe. Hapa lazima utajifunza uongozi, utajifunza namna ya kutangaza na namna ya kuuza. Pia lazima ujifunze kuhusu usimamizi wa fedha. Biashara itakulazimisha ujifunze hata kama hutaki, na hivyo utakuwa bora sana. Muhimu ni usikate tu tamaa, hasa pale unapokutana na changamoto, bali jua ndiyo wakati wako wa kujifunza.
Anza biashara yako, anza hata kidogo na kila siku ifanyie kazi ili kuikuza zaidi, utajifunza mengi kuhusu maisha na mafanikio, na wakati huo unaelekea kufanikiwa.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)