Kufanya makosa ni kitu ambacho kimekuwa kinapewa taswira hasi kwenye ulimwengu tunaoishi sasa. Kufanya makosa kunaonekana kama ni kitu kibaya na anayefanya makosa hayo ni mtu mwenye uwezo mdogo.

Mtazamo huu juu ya makosa umewafanya wengi kuogopa kuchukua hatua. Wengi wameshindwa kuchukua hatua kwa kuhofia kufanya makosa na kuonekana kama watu ambao hawawezi.

Kuna vitu viwili tunavyovisahau hapa;

Cha kwanza ni kwamba hakuna anayejua kila kitu, hayupo mtu wa aina hiyo. Yule unayemwona ni mtaalamu kwenye kitu fulani leo, kuna siku alikuwa hajui kabisa. Yule unayemwona ni injinia leo, kuna siku alikuwa hajui kama mbili ukijumlisha na mbili jibu lake ni nne, ilibidi akae chini na kufundishwa hilo.

Hivi ndivyo safari ya maisha yetu inavyokwenda kila siku, kuna vingi ambavyo hatuvijui, na hivyo kila siku kwetu ni kujifunza.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Don’t Go Back To School (Usirudi Tena Darasani).

Kitu cha pili ni kwamba kukosea ni sehemu ya kujifunza. Ukisoma kitabu chochote, unaweza kuelewa vizuri sana, na kuona sasa upo tayari kuchukua hatua. Lakini unapochukua hatua ndipo unapokutana na ukweli wenyewe, kwamba kuna vingi ulikuwa hujajua bado. Kwenye kufanya njia pekee ya kujifunza ni kufanya makosa, unapokosea ndiyo unajua kwamba ulichofanya siyo na hivyo kurekebisha.

Tufute hii dhana kwamba kufanya makosa ni kitu kibaya, tuwe tayari kujifunza na tusiogope kufanya makosa kwenye kujifunza, hii ndiyo njia ya kujifunza kupitia kufanya.

Mtu pekee asiyekosea ni yule ambaye hajaribu mambo mapya na makubwa, je mara ya mwisho wewe kukosea ilikuwa lini? Hiki ni kipimo kizuri cha kujua kama unafanya mapya na makubwa au unafanya kwa mazoea.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)