Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Karibu tena kwenye falsafa yetu mpya ya maisha, ambapo tunakwenda kujifunza njia bora za kuyafanya maisha yetu kuwa bora, yenye furaha na mafanikio makubwa. kama ambavyo nimekuwa nasema kila mara, maisha bila ya falsafa ni maisha ambayo hayana ramani wala mwelekeo, ni maisha ambayo yanaweza kuyumbishwa na chochote na ni vigumu sana kuwa na furaha na mafanikio kwa maisha ya aina hiyo.

Kitu kikubwa ambacho tumekuwa tunagusia kwenye falsafa mpya ya maisha ni ukweli na kuishi maisha yenye maana kwetu na wale wanaotuzunguka. Lakini imekuwa vigumu kwa wengi kuweza kufikia maisha haya kwa sababu moja kubwa sana. Sababu hii imekuwa kikwazo kwa wengi kuwa na maisha bora na wanayoyafurahia. Leo katika makala hii ya falsafa mpya ya maisha tunakwenda kuangalia sababu hii na jinsi ya kuondokana nayo.

SOMA; UKURASA WA 497; Watu Ambao Hawawezi Kukuelewa….

Sababu kuu inayofanya maisha ya wengi yasiwe bora ni UNAFIKI. Watu wengi wamekuwa na unafiki mkubwa kwenye maisha yao wenyewe na hii imekuwa inawaathiri wao wenyewe na kuwazuia kuwa na maisha bora. Kuna watu wanasema kabisa kwamba maisha bila ya unafiki hayawezi kwenda, huenda kuna ukweli, inapokuja kwenye baadhi ya mambo ya kijamii, lakini unapoleta unafiki kwenye maisha yako mwenyewe, hapa unajiharibia kabisa maisha yako.

Kabla hatujaangalia jinsi tunavyotengeneza unafiki kwenye maisha yetu, na jinsi ya kuondokana nao, kwanza tuangalie unafiki ni nini.

Unafiki ni pale mtu anapofanya kitu ili tu aonekane na wengine, lakini anavyoamini na nia yake ni tofauti kabisa. Mtu anachagua kufanya kitu ambacho hakiamini kabisa, au hajali kabisa, lakini tu anataka kuwapendeza wengine na kupata kile ambacho anataka kupata kwa wakati huo. Tumekuwa tunaona unafiki kwenye siasa, ambapo wanasiana waliokuwa wanaonekana mahasimu wakija pamoja kwa sababu ya kupata kitu fulani. Unafiki pia umekuwepo kwenye imani za kidini, ambapo watu wanakwenda kwenye nyumba za ibada kusali, lakini wakitoka pale wanafanya kinyume kabisa na mafundisho ya dini zao. Wanapokuwa kwenye nyumba zao za ibada, au wanapoonekana na waumini wenzao, wanajionesha kama watakatifu.

Unafiki umekuwepo kwenye maeneo karibu yote ya maisha yetu, na umekuwepo tangu kuwepo kwa maisha ya binadamu. Kwa sababu kila mtu kuna wakai ambapo anahitaji kupata kitu fulani, sasa wale wanaotaka njia ya mkato ya kupata chochote wanachotaka, unafiki ni njia rahisi kwao.

Unafiki ni mbaya, lakini unafiki mbaya kabisa ni ule unafiki kwenye maisha yetu wenyewe.

Je unafiki kwenye maisha yetu wenyewe ndiyo upi?

Unafiki kwenye maisha yetu wenyewe, ni pale ambapo tunajifanya kuna kitu hatukioni, wakati kipo wazi kabisa mbele yetu. Hapa mtu anachagua kuenda na maisha yake kama vile kila kitu kipo sawa, wakati anajua kabisa kuna mambo hayapo sawa. Mtu anaingia kwenye unafiki huu kwa kuogopa kuweka mambo sawa, kwa kutokutaka kusumbuana na wengine. Mtu anapoanza unafiki inaonekana ni njia rahisi ya kuenda na maisha yake, lakini baadaye unageuka kuwa mzigo mzito kwenye maisha yake na unamzuia kuwa na maisha bora na yenye mafanikio.

SOMA; UKURASA WA 572; Misingi Mitatu Ya Kujenga Ushirikiano Bora Na Wengine.

Maeneo ambayo watu wengi wamekuwa na unafiki kwenye maisha yao ni haya;

Kwenye kazi; watu wengi hawafurahii kazi wanazozifanya, wapo pale kwa sababu tu ya kupata fedha. Cha kushangaza zaidi ni kwamba hata kipato wanachopata kwenye kazi hizi bado hakiwatoshi. Hivyo watu hawa wanakuwa na mizigo miwili, mzigo kwa kwanza ni kuchukia ile kazi wanayoifanya, na mzigo wa pili ni kipato kutokutosheleza. Pamoja na mizigo hii bado wengi wamekuwa wakijifanya kama vile mambo yako safi tu. Wataendelea kufanya kazi zao kama wanavyozifanya, na wataendelea kulalamikia kipato kila siku.

Kulainisha hali hizo wanajikuta wameingia kwenye mikopo, hivyo unaanza mzunguko mwingine, wa kukopa kisha kulipa anapopata fedha, na kuanza kukopa tena. Wakati wote huu anajisahaulisha tatizo lake la msingi, kwamba kazi aliyonayo haipendi, na kipato hakimtoshi. Anaendelea kwenda na unafiki, akifikiri labda ipo siku mambo yatabadilika yenyewe, japo anajua kabisa mambo hayabadiliki. Unafiki wa aina hii umewafanya watu wengi kuwa na maisha magumu licha ya kuwa na uwezo wa kufanya maisha yao kuwa bora zaidi.

Kwenye mahusiano; hili ni eneo jingine ambalo watu wamekuwa na unafiki sana kwenye maisha yao. Na hapa kwenye mahusiano namaanisha mahusiano yetu na wale wanaotuzunguka, kuanzia ndugu zetu, marafiki zetu, watoto wetu, na wenza wetu.  Kuna mambo mengi ambayo huwa yanatokea baina ya watu, ambayo yanamfanya mtu mmoja kukwazika, na kila mtu anajua kwamba jambo lililofanyika limemkwaza mtu, lakini unafiki unachukua hatua yake. Kila mtu anajifanya kama kila kitu kipo vizuri, na hakuna tatizo, hasa pale wanapokutana, lakini kila mtu ndani yake anajua kabisa kwamba kuna mambo hayapo sawa.

Kuna watu ambao wanakuwa wamekosana na wengine, au wamekwazika na kile ambacho wengine wamewafanyia, lakini hawawaambii watu hao, badala yake wanakwenda kuwaambia watu wengine. Yaani wakikutana na wale ambao wamewakwaza hawawaambii chochote, na wanajifanya kila kitu kipo sawa, ila wanapokuwa na wengine wanaanza kuwaambia ni kwa namna gani wamekwazika kupitia wengine.

SOMA; Kama Maisha Ni Vita, Basi Huu Ndio Ukweli Unaotakiwa Kujua.

Kwenye mafanikio; hakuna eneo ambalo watu wamejijengea unafiki kama eneo la mafanikio, hasa wale ambao wameshindwa kufikia mafanikio. Watu wamekuwa wakitafuta sababu za kuwapooza wao kwa ni i hawajafanikiwa ila wengine wamefanikiwa. Na kwa unafiki huu huwa wanakuja na sababu nzuri sana kwao, zinazowafanya wao waonekane ni watakatifu kuliko wale waliofanikiwa.

Inapokuja kwenye mafanikio ya kifedha, yaani utajiri, hakuna watu wanafiki kama watu masikini. Kwa sababu wengi huwa wanaamini kwamba matajiri ni watu ambao wanadhulumu, ni watu ambao wametumia njia zisizo halali kupata utajiri wao. Na wanaposikia tajiri kapata tatizo, basi wanakuwa wa kwanza kushangilia wakijua kwamba sasa na yeye atakoma. Wote huu ni unafiki wa kukataa kukubali uhalisia kwamba wao ni masikini kutokana na aina ya maisha waliyochagua kuishi, na wale ambao ni matajiri, wamechagua kuishi maisha ya tofauti.

Tukiangalia kila eneo la maisha yetu, tunaona ni kwa namna gani tumekuwa wanafiki na kujijengea unafiki, ambao unatupooza tusiumie kwa namna mambo yanavyokwenda.

Je tunawezaje kuondokana na unafiki huu ili kuwa na maisha bora?

Jibu ni moja, penda ukweli, jua ukweli na ukweli utakuweka huru. Hakuna jibu bora zaidi ya hilo, lakini lina changamoto kubwa kwa sababu ukweli ni mchungu, ukweli unauma, ukweli haubembelezi.

Wengi wanapenda kubembelezwa na hivyo hukimbia kuujua ukweli. Huona ni vyema kuweka ukweli pembeni na kujipa matumaini ya uongo, hii imekuwa inawasaidia kwa muda mfupi, lakini haitatui tatizo la kudumu.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Kinachotuzuia Kuujua Ukweli Na Hivyo Kushindwa Kuwa Na Maisha Bora.

Unapojikuta kwenye tatizo au changamoto yoyote kwenye maisha yako, usitake kujidanganya, badala yake jua ukweli, kuwa tayari kupokea ukweli, hata kama utakuumiza. Wakati mwingine ukweli utakuonesha namna ambavyo umekuwa mzembe na mvivu, wakati mwingine ukweli utakuonesha namna gani usivyojali. Pokea ukweli huo na ufanyie kazi, kadiri unavyoupokea ukweli mapema, ndivyo unavyookoa jahazi mapema.

Tatizo la ukweli ni kwamba huwa haupotei, ukweli unaweza kufichwa kwa muda tu, lakini hauwezi kupotezwa, hivyo kubali ukweli na chukua hatua. Kubali kwamba upo kwenye matatizo na anza kutatua matatizo hayo, kubali kwamba kazi uliyonayo sasa huipendi na kipato hakikutoshelezi, na anza kuchukua hatua ya kutengeneza kazi nyingine ambayo ni bora kwako. Anza kuweka juhudi kubwa kwenye kazi hiyo kwa sasa ili kuongeza kipato chako pia. Kubali kwamba una mgogoro na watu wa karibu yako, na kaa nao chini kutatua mgogoro huo, kuukwepa hakuondoi mgogoro huo, bali kunazidi kuharibu mahusiano yenu.

Upende ukweli, achana na unafiki, ona kila kinachokujia mbele yako, acha kujifanya huoni wakati kila dalili zinaonekana.

Ongeza zana hii muhimu ya kuepuka unafiki katika kujijengea falsafa mpya ya maisha, ili kuwa na maisha bora yenye furaha na mafanikio.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)