Ni kweli kabisa tunahitaji kupata hamasa kutoka kwa wengine. Tunapojua ya kwamba kuna watu ambao waliweza kufika pale ambapo tunataka kufika, basi tunakuwa na hamasa kubwa sana kwamba hata sisi tunaweza. Hii ni nzuri.

Lakini kumekuwa na upendeleo mkubwa sana kwenye kutoa na kutafuta taarifa za watu hawa ambao wameweza kufanya makubwa kwenye maisha yao. Tumekuwa tunawaangalia kama vile wao pekee ndiyo waliojaribu na kushinda, hakukuwa na wengine.

Ukweli ni kwamba, katika kila mtu mmoja unayemwona amefanikiwa sana, kuna wengine zaidi ya 100 ambao walianza naye, na walifanya kama yeye lakini hawajafanikiwa. Sisi tunakazana kumwangalia huyu mmoja na kusahau hao wengine wengi walioshinda.

Tunapenda kutumia mifano michache, kwa mfano;

Bill Gates aliacha shule lakini amefanikiwa kuliko hata walimaliza shule. Ni kweli, lakini je umeangalia maisha ya wengi walioacha shule yako vipi?

Bakhresa alianza biashara kwa kuuza nyanya na sasa anamiliki viwanda, ni kweli, lakini umeangalia wauza nyanya wengine walioanza na yeye kipindi hiko wako wapi?

Dimond alikua mtoto wa manzese, kaanza kuimbaimba sasa hivi ni mwanamuziki mkubwa Afrika, ni kweli lakini umeangalia watoto wengine wa pale manzese ambao walikuwa wanaimba na Dimond? Wamefika wapi kimuziki na kimaisha?

Kwa wanafunzi; mtu fulani alisoma kozi kama tunayosoma sisi, ona amepata kazi nzuri na ni tajiri sana. Ni kweli, lakini je umeangalia wenzake ambao walisoma kozi moja na kuhitimu pamoja? Je nao wana kazi na utajiri kama wa huyo mmoja mnayemwangalia?

Kwenye kamari na bahati nasibu; utaona mtu mmoja anashangiliwa kubahatika kupata mamilioni, lakini hutaambiwa kuhusu maelfu ambao walishiriki na hakuna hata mmoja ambaye amepata hayo mamilioni.

SOMA; UKURASA WA 370; Tabia Za Walioshindwa Unazotakiwa Kuepuka.

Ukweli ni kwamba, mafanikio siyo rahisi kama ambavyo tumekuwa tunahubiriwa, hasa pale tunapowaangalia wengine. Kuna mambo mengi ya ndani ya mtu mwenyewe na nje yake ambayo yakikutana sawasawa mtu anafanikiwa sana.

Sisemi uwaangalie wengi walishindwa ili ukate tamaa, bali uwaangalie ili uwe na taarifa sahihi, kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa, na sababu za kushindwa uzijue, kabla hujajipa imani kubwa ya kushindwa.

Hivyo unapochagua kujifunza mafanikio kupitia wengine, usiangalie wale walishinda pekee, itakunufaisha kama utaangalia na upande wa pili.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)