Ili uweze kufikia mafanikio makubwa yapo mambo ya lazima ambayo unatakiwa kuyafanya karibu kila siku ili ufanikiwe. Naamini hilo lipo wazi kabisa, hiyo ikiwa na maana kwamba huwezi kufanikiwa bila kufanya mambo hayo.
Wengi hufikiri kwamba ili ufanikiwe ni lazima uwe na akili ya ajabu  na ufanye mambo makubwa sana. kama hayo ndiyo mawazo yako, hapana hiyo haiku hivyo, mafanikio yanahitaji ufanye mambo kadhaa kwa muendelezo bila kuacha hata kama ni madogo.
Bila shaka unaweza ukawa hunielewi vizuri. Kupitia makala haya naomba nikushirikishe mambo machache ambayo ukiyafanya mara kwa mara katika maisha yako, uwe na uhakika hakuna mtu atakaye kuzuia kufanikiwa tena. Mafanikio yatakuwa ni haki yako.  
1. Kuwa mtu wa vitendo.
Siri ya ushindi wa mafanikio yako haipo kwenye kujua vitu peke yake au kuongea. Kuwa mtu wa vitendo. Kama kuna jambo umelikusudia lifanye.  Acha matendo yako yaongee zaidi na hapo ni lazima ufanikiwe.
2. Kutokuridhika mapema.
Sumu kubwa ya mafanikio ni kule kuridhika mapema. Ikiwa unataka kufikia kilele cha mafanikio makubwa, achana na kuridhika na mafanikio madogo yasiyokufikisha popote. Tafuta mafanikio makubwa zaidi ya hayo.
3. kutokuhamasishwa na pesa.
Chagua kufanya kazi bidii zote bila kusukumwa na msukumo wa nje kama vile pesa. pesa iwe ni matokeo na siyo kichocheo cha wewe kufanya kazi. Kama utafanya hivyo bila kusukumwa na pesa uwe na uhakika utafanikiwa.
4. Kujitawala.
Wakati wote jifunze kujitawala kwa mambo yako. jifunze kutawala muda, nidhamu na pesa zako. Ikiwa utaweza kumudu kujitawala wewe mwenyewe ni wazi uatajitengenezea mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
5. Kutokuogopa kushindwa.
Kama kuna kitu umepanga kukifanya, hebu kifanye bila woga. Acha kuwaza ikiwa ikatokea nimeshindwa itakuaje? Jitoe mhanga kufanikisha ndoto zako mpaka zieleweke. Kwa kufanya hivyo utakuwa mshindi.
6. Kuwa wewe kama wewe.
Mafanikio hayaji kwa kuiga vitu sana kwa wengine. Mafanikio yanakuja kwa kujijengea misimamo yako mwenyewe na kusimamia kile unachokiaminikwamba ni lazima kikufanikishe.
7. Kujifunza kila siku.
Ikiwa utakuwa unawekeza kwenye maarifa kila siku tambua ni lazima ufanikiwe. Hakuna maarifa ambayo yanaweza yakakuacha eti ukawa mtupu, ikiwa utafanyia kazi. Amua kujifunza siku zote za maisha yako.
8. Kujiamini.
Huwezi kupata mafanikio bila kujiamini. Msingi mkubwa wa mafanikio unatapatikana kwa kufanya mambo yako kwa kujiamini tena kwa sehemu kubwa. Ukijiamini utafanikisha mambo mengi na makubwa sana.
9. Kujiwekea malengo.
Kujiwekea malengo pia ni silaha mojawapo kubwa ya kukusaidia kufanikiwa. Kama huweki malengo, ni ngumu sana kwako wewe kuweza kufanikiwa kwa kile unachokifanya. Weka malengo na kisha yafuate kila siku mpaka ndoto zako zitimie.
10. Kutokuwa na kinyongo.
Ni lazima ifike mahali ukubali kwamba ili ufanikiwe hutakiwi kuwa na kinyongo na watu waliofanikiwa. Inabidi ujifunze vile vilivyowafanikisha hadi wakafikia hapo. Ukifanya hivyo, hapo utakuwa mshindi na pia utajikuta unatengeneza mafanikio kwa upande wako.
11. Kutunza muda vizuri.
Muda ni pesa. Ni vyema ukajua namna ya kutunza muda wako vizuri ili ukusaidie kufikia mafanikio makubwa. Wengi waliofanikiwa hawapotezi muda wao hovyo hata kidogo.
12. Kutokujiwekea sababu.
Chochote unachopanga kufanya, hakikisha umekifanya. Acha kujiwekea sababu zako zisizo na maana kwamba hujafanya hiki kwa sababu hii au ile. Ukiishi kwa kutojiwekea sbababu ni lazima utafanikiwa kwa viwango vya juu sana.
Kwa ufupi hayo ndiyo mambo ambayo ukiyafanya ni lazima ufanikiwe. Chukua hatua kuelekea kwenye ndoto zako.
Pia kwa makala nyingine za mafanikio na maisha, tembelea dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,