Ni saikolojia ya binadamu kwamba, kile ambacho kinapatikana kwa urahisi, huwa hatukipi thamani kubwa. Na hivyo kutokukijali, au kutokitunza na hivyo kukipoteza haraka.
Kwa mfano, watu wanaopata fedha nyingi kwa haraka, bila ya kuweka kazi kubwa, hujikuta wakipoteza fedha hizo zote ndani ya muda mfupi, au wakizitumia hovyo na kurudi kwenye hali waliyokuwa nayo mwanzo.
Hata watu ambao wanapata vitu vya bure, huwa hawavipi thamani kubwa kama vile ambavyo wamevifanyia kazi.
Hii inatufundisha mambo mawili makubwa;
Moja; chochote tunachotaka kwenye maisha yetu, tuhakikishe tumeweka juhudi zetu katika kukipata. Tusipende kukimbilia vitu rahisi kwa sababu vinaweza visiridhishe nafsi zetu.
Ipo hivi, moja ya mahitaji yetu ya msingi kabisa sisi binadamu, ni kuona tunatoa mchango bora kwenye maisha ya wengine. Kuona tumefanya kitu ambacho kimeboresha maisha ya wengine. Na siyo kupata fedha au matokeo mazuri pekee. Hivyo angalia sana ni mchango gani unatoa kwa wengine, kabla hujaangalia unapata nini.
Mbili; inapotokea umepata kitu chochote kwa urahisi, basi usikimbilie kutumia, badala yake kaa na tafakari ili uone ni namna gani unaweza kutumia kitu hicho kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.
Kwa mfano kama umepata fedha nyingi kwa wakati mmoja, labda ni urithi au bahati nasibu, usikimbilie kutumia fedha hizo kutimiza mahitaji yako, zitaisha haraka na mahitaji yako hayatatimia. Badala yake angalia ni jinsi gani unaweza kuboresha maisha ya wengine kupitia fedha ulizopata. Hapa utaona huduma nyingi za kutoa, ambazo zitakufanya uendelee kunufaika na kile ulichopata.
Lakini kama utaanza kujifikiria wewe mwenyewe, kama utaanza kuangalia kipi ulikuwa unataka muda mrefu hujapata, utamaliza fedha zote na mahitaji yako hayawezi kuisha.
Rahisi kupata, ngumu kutunza, ngumu kupata, rahisi kutunza. Jifunze kuitumia vizuri saikolojia yako kuhakikisha kila unachopata, kiwe rahisi au kigumu, kinaleta mabadiliko kwenye maisha yako na ya wale wanaokuzunguka.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)