Tunaishi kwenye zama za tofauti kabisa ukilinganisha na zama zilizopita. Kwa sasa kila kitu ni haraka. Tunataka vitu haraka na tunavitaka sasa, subira imekuwa kitu adimu mno.

Kasi ndiyo kipimo cha ubora kwa sasa, tunataka kusafiri kwa kasi, tunataka mtandao uwe na kasi kubwa, kusubiri dakika chache ni mtihani mgumu kwenye dunia ya sasa.

Ni kitu kizuri, mabadiliko ya kiteknolojia yamerahisisha maisha, sasa unaweza kuwasiliana na mtu popote alipo kwa urahisi kabisa, na kwa gharama nafuu mno.

Lakini inapokuja kwenye MAISHA YA MAFANIKIO, kasi na haraka hazikufikishi kwenye mafanikio, badala yake zinakupoteza. Zinakufanya uchelewe kufika kwa sababu utafanya makosa mengi mno kama utayaendea mafanikio kwa kasi na haraka.

Pamoja na kubadilika kwa nyakati na teknolojia, bado kanuni za mafanikio zipo vile vile, mafanikio ya kweli yanatokana na kazi ambayo inaongeza thamani kwenye maisha ya wengine. Pia yanahitaji uvumilivu kwa sababu hayatokei haraka.

Lakini kwa kuwa tunaishi kwenye dunia inayotukuza kasi na haraka, basi kuna wenzetu ambao wameyatoa maisha yao kutafuta njia za kasi na haraka za kufanikiwa. Na wamepata njia nyingi ambazo zimewaumiza watu badala ya kuwafanya wafanikiwe.

Wapo waliodanganya na kudanganywa kwamba unaweza kuwa na maisha ya mafanikio, hasa kifedha kama utacheza kamari au bahati na sibu, wamecheza na kuishia kupoteza fedha zaidi ya kuzipata.

Wapo ambao wamedanganyika biashara ya aina fulani ina faida kubwa na ya haraka, wakapewa mahesabu mazuri namna gani wanaweza kuanza na mtaji kidogo na baadaye wakawa mamilionea, wakaingia kwenye biashara hizo na kuishia kuumia.

Wengi wamedanganywa kilimo cha aina fulani ndiyo kitawatoa, wakapewa mahesabu mazuri ya fedha kidogo na muda, wakapewa mahesabu makubwa ya mavuno na faida kubwa. Wakahamasika, wakaingia kwenye kilimo, mwishowe wakaumia vibaya sana, kwa kupata matokeo tofauti na waliyotegemea.

SOMA; Sababu tatu kwa nini biashara nyingi zinakufa haraka.

Ninachotaka kukuambia mwana mafanikio mwenzangu ni hiki; usiingie kwenye kazi, biashara au kilimo kwa sababu umeambiwa kinalipa sana, badala yake ingia kwa sababu umeshajifunza vya kutosha kuhusu kitu hiko, na upo tayari kuweka kila tone la jasho lako, chozi lako na damu yako ikibidi kuhakikisha unafanikiwa kupitia hicho unachofanya.

Safari haitakuwa rahisi, mipango haitakwenda kama ulivyopanga, hasa kwenye fedha na muda. Hivyo kuwa mvumilivu na weka juhudi. Hakuna kitakachokuzuia kupata unachotaka, ila wewe mwenyewe kama utataka kuleta kasi na haraka kwenye mafanikio.

Linapokuja swala la maisha ya mafanikio, kasi na haraka weka pembeni, kanuni ni zile zile, hazijabadilika.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)