Habari za leo rafiki yangu?
Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto  zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Kama ambavyo nimekuwa nakuambia mara kwa mara, na utanisamehe kama umeanza kuchoka, lakini lazima nirudie tena na tena kwamba changamoto hazikwepeki. Kwenye safari hii ya mafanikio, changamoto ni lazima, na hivyo hatuwezi kuzikimbia ila kuzitatua. Na muhimu zaidi ni kujua kwamba kama ingekuwa rahisi basi kila mtu angekuwa na mafanikio makubwa. Ni ngumu na changamoto zipo kila hatua ndiyo maana ni wachache pekee wanafikia mafanikio hayo makubwa. Najua wewe rafiki yangu ni mmoja wa wachache hawa, hongera sana.
 

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA HAPA.


Kwenye makala ya leo nitakwenda kukushirikisha ushauri unaoweza kuwapa vijana ambao kwa sasa hawana ajira ila wanataka kutoka kimaisha. Leo nataka utoke na kitu cha kumwambia kijana, kama ni wewe sawa, au kama kuna kijana alishakuomba ushauri wa aina hii basi unaweza kumwambia haya utakayojifunza leo, au kwa kumsaidia zaidi mtumie kabisa makala hii ili asome mwenyewe.
Kabla hatujaona ushauri unaoweza kuwapa vijana hawa wanaotaka kutoka kimaisha ila changamoto kwao ni ukosefu wa ajira, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusiana na changamoto hii;

Nina vijana kama 60 napenda kuwafundisha kupitia mitandao na wakati mwingine tunakutana ana kwa ana. Changamoto kubwa kuna waliosoma kozi mbalimbali na hawana kazi, nifanyeje hata waweze kujianzishia cha kufanya. Nimekuwa nakusoma sana na wakati mwingine natumia masomo yako kuwatumia wasome ila sijajua jinsi ya kuwasaidia watoke kimafanikio. Hata ukitembelea facebook utakutana na group linaitwa Youth Family angalia hata posts zetu tunazowafundisha. Kazi kubwa wanaona pesa ndio jawabu wafanyaje sasa.
Teddy C. A.

Habari Teddy,
Hongera sana kwa moyo wako mzuri wa kupenda kuwafundisha wengine mambo mazuri ya kuwawezesha kuwa na maisha bora. Ni roho ya kipekee kwa sababu kufundisha ni kujali, wapo wengi wenye maarifa lakini hawapo tayari kuyatoa kwa wengine.
Pia asante sana kwa kuwa msomaji na kuwashirikisha vijana masomo ninayotoa, ninaamini kwa njia moja au nyingine nimewezesha kufanya maamuzi bora ya maisha yao.
Sasa kuhusiana na changamoto uliyotuandikia, ni kweli kuna vijana wengi ambao hawana ajira na hii inakuwa changamoto kwao kuweza kufikia ndoto zao. Ukiongeza na kwamba wengi wamesoma na hivyo matarajio yao yalikuwa kutumia elimu waliyoipata kutoa huduma kwa wengine.

Umefanya hatua nzuri kuwa unawafundisha vijana hao maarifa mbalimbali, ila kuna hatua moja ambayo hujawawezesha kupiga, hatua hiyo ni kuchukua hatua. Unajua ni vizuri sana kujifunza, lakini hata ujifunze kiasi gani, hata usome vitabu vizuri kiasi gani, na hata uyaelewe mambo kiasi gani, kama hutachukua hatua, hakuna kitakachobadilika, utabaki pale pale ambapo upo wakati wote.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Vijana Wanaotafuta Ajira. Soma Hapa Uone Fursa Unazoweza Kutumia.

Sasa umefika wakati wa wewe kuwawezesha vijana hao kuchukua hatua, watumie yale ambayo wamekuwa wanajifunza katika kuboresha maisha yako. Lakini hili ni gumu kutokana na mtazamo ambao vijana hao wanaweza kuwa nao. Huenda wengi wanafikiria ajira kama hatua yao ya kuanzia, hivyo wanasubiri mpaka wapate ajira hizo. Lakini kwa kuwa ajira zimekuwa siyo za uhakika, kuna umuhimu wa kuangalia upande wa pili kwenye hili.

Kwa utaratibu ambao mmejiwekea na vijana hawa katika mafundisho yenu, waambie wale ambao wapo tayari kuchukua hatua, wapo tayari kuweka sababu zao pembeni na kuchukua hatua, waanze kwa kufanya kitu. Wachague kitu ambacho wanaweza kufanya kwa pale ambapo wapo, sijajua mazingira yao yapoje, lakini kila mmoja akiangalia pale ambapo yupo, ataweza kuona hatua anazoweza kuchukua.

Kaa chini na kila ambaye yupo tayari kuchukua hatua na siyo sababu, mwambie aangalie mazingira yanayomzunguka, aangalie vitu ambavyo amekuwa anapendelea kufanya au kufuatilia, kisha aangalie elimu ambayo ameipata sasa. Akae chini na kufikiri kwa kina, kwa msaada wako kama inawezekana, aangalie ni namna gani anaweza kutumia kila kinachomzunguka kujiajiri au hata kuajiriwa.

Baadhi ya hatua ambazo mtu anaweza kuchukua, kulingana na mazingira aliyopo zinaweza kuwa;
Kuomba kazi ya kujitolea kulingana na ujuzi alionao kwenye maeneo ambayo yanaendana na taaluma yake. Aweze kuona maeneo yanayoendana na taaluma aliyosomea, na aombe kazi ya kujitolea, asitake malipo badala yake kupata uzoefu na pia kujua mambo mengi zaidi kuhusiana na kazi hizo.

SOMA; USHAURI; Biashara Nzuri, Inayolipa Na Unayoweza Kuifanya.

Kijana pia anaweza kujikusanya na wenzake, wakachangishana fedha ndogo ndogo na kuwaomba watu wao wa karibu wawaongezee mchango kidogo na wakaanza mradi wowote wanaoweza kuweka juhudi zao. Wanaweza kufanya kilimo kama wapo kwenye eneo lililopo karibu na mashamba, hapa wanaweza kuanza na hatua ndogo na kisha kukua. Wanaweza kufikiria miradi mingine inayoendana na maeneo waliyopo na kiasi cha fedha wanachoweza kuanzia. Mfano wanaweza kuanzisha mradi wa kuosha magari kama wapo maeneo ya mjini, mradi huu wanaweza kuanza na kiasi kidogo cha fedha, na wakaweka juhudi kubwa kuukuza. 

Miradi ipo mingi, ni uwezo wa vijana kufikiri na utayari wa kuweka juhudi.
Kitu kingine ambacho vijana wanaweza kufanya ni kuingia kwenye ujasiriamali wa biashara taarifa. Hapa kijana anatoa taarifa za kitaalamu kulingana na uzoefu alionao, elimu aliyopata na taaluma aliyosomea. Kijana anaweza kufungua blog yake, ambayo ni bure kabisa au kwa gharama ndogo, na kuitumia kutoa taarifa sahihi kwa watu. Hapa anaweza kuweka juhudi kubwa na akawa mtu wa kutegemewa katika utoaji wake wa taarifa, baadaye akageuza blog yake kuwa sehemu ya kipato chake. Na hapa kwenye ujasiriamali wa taarifa itabidi uwashauri wanunue kitabu changu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG ukibonyeza hayo maandishi utapata utaratibu wa kupata kitabu hiko.
Yote haya ambayo nimependekeza na mengine yanayofanana na hayo, ni mambo yanayoweza kufanywa na yeyote ambaye amejitoa kweli na anataka kubadilika. Lakini tatizo ni moja, inatakiwa mtu aweke juhudi kubwa, mtu aache uvivu, aache sababu, aache maisha aliyozoea kuishi ili kuweza kufanya hayo. Vinginevyo atakuwa na kila sababu kwa nini kila mradi niliopendekeza hauwezi kufanikiwa kwake.

Baada ya kuwashauri hayo vijana, chagua kubaki na wale ambao wanachukua hatua pekee, kama kuna ambao hawataki kuchukua hatua, ni vyema ukawaacha wakafanya kile ambacho wanaona ni sahihi kwao kufanya. Kwa sababu kukaa nao watawarudisha nyuma hata wale ambao wanafanya. Nina uhakika kwa asilimia mia moja kijana atakayechukua hatua yoyote, hawezi kubaki pale ambapo yupo sasa. Tatizo siyo fedha wala fursa, bali tatizo ni utayari wa mtu kuchukua hatua, kuweka sababu pembeni na kufanya jambo la tofauti kwenye maisha yako.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

Teddy nikutakie kila la kheri katika kazi hii kubwa uliyochagua kuifanya, usichoke kuifanya, ila ifanye na wale ambao wapo tayari kuchukua hatua. Usifurahie tu kuwa na watu ambao wanapenda mafunzo, badala yake wawe tayari kufanyia kazi mafunzo hayo.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.