Kwenye maisha, kazi na hata biashara, zipo aina mbili za kushindwa.

Lakini kabla hatujaangalia aina hizi, kwanza tuangalie kushindwa. Kushindwa ndiyo kitu ambacho kimekuwa kinawapa wengi hofu pale wanapotaka kufanya mambo makubwa kwenye maisha yao. Lakini hofu hii imekuwa haiwasaidii chochote, badala yake imekuwa inawazuia kufanya yale makubwa kwenye maisha yetu.

Sasa turudi kwenye aina mbili za kushindwa;

Aina ya kwanza ni kushindwa kwa kutokufanya. Yaani hapa ile hofu ya kushindwa inakutawala kiasi kwamba unashindwa hata kufanya, na hivyo unakuwa umeshindwa kabisa. Unataka kuanzisha biashara lakini una hofu kwamba utapata hasara, au hutaweza kuisimamia vizuri, hii inakuzuia kuanza biashara na unakuwa umeshindwa kabisa.

Aina ya pili ya kushindwa ni kushindwa kwa kufanya. Hapa unachagua kufanya kitu, lakini unapata matokeo ambayo ni tofauti na ulivyotegemea. Unapanga kuanzisha biashara, unaweka mipango yako vizuri, kila kitu kinaonekana kiko vizuri, unaanza biashara lakini unaishia kupata hasara kubwa. Hapa unachagua kufanya kitu na unapata matokeo mabaya kabisa, yanayoweza hata kukukatisha tamaa.

Swali la msingi kabisa la kujiuliza katika aina hizi mbili ni je ni aina ipi ya kushindwa ni nzuri kwako?

Na jibu ni kushindwa kwa kufanya ni bora kuliko kushindwa kwa kutokufanya. Hii ni kwa sababu unaposhindwa kwa kufanya, unakuwa umejifunza kitu kupitia hatua ulizochukua, kama ilikuwa biashara na ukapata hasara, angalau utakuwa umejifunza njia za kuepuka hasara kwenye biashara yako, au mambo ya kuzingatia ili kuepuka hasara.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; FAIL FORWARD (Hatua 15 Za Kufikia Mafanikio Kupitia Kushindwa).

Kama utashindwa kwa kutokufanya kabisa, hakuna chochote ambacho unakuwa umejifunza, badala yake unakuwa umetawaliwa na hofu, ambazo hazitakuachia ufanye jambo lolote kwenye maisha yako.

Nimalize kwa kusema hili rafiki yangu, kwa vyovyote vile fanya kitu, ukifanikiwa utakuwa umepata ulichotaka, na ukishindwa utakuwa umejifunza njia sahihi ya kupata kile unachotaka. Usisahau lakini, ya kwamba kwenye safari yetu ya mafanikio, ukishafanya tu, hakuna kushindwa, bali kuna kujifunza.

Uwe na siku njema sana leo rafiki yangu.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)