Habari rafiki?
Kama ambavyo wote tunajua, safari ya mafanikio siyo safari rahisi, ina changamoto na vikwazo vingi. Watu wengi wanaanza safari hii lakini hawafiki mbali. Matumaini makubwa waliyokuwa nayo yanazima kabisa pale wanapokutana na magumu na changamoto. Hili ndiyo limekuwa linatokea kwa wengi na hivyo kushindwa kupiga hatua kwenye maisha yao.

Leo tunakwenda kuangalia swali moja muhimu la kujiuliza kila siku ili kupata hamasa ya kuendelea na safari yako ya mafanikio. Kupitia swali hili utaweza kuvuka kila changamoto unayokutana nayo, hata kama itakuwa changamoto kubwa kiasi gani.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Swali ambalo unapaswa kujiuliza kila siku kwenye safari yako ya mafanikio ni hili; JE NI KITU GANI KINANISUKUMA KUFANYA HIKI NINACHOFANYA? Kwa lugha nyingine ni kwa nini unafanya kile ambacho umechagua kufanya? Unapokuwa na sababu ambayo inakusukuma na sababu hii ikawa kubwa, hakuna kikwazo au changamoto inayoweza kukuzuia wewe kufikia mafanikio makubwa.

Sasa jibu la swali hili linaweza kuwa jibu rahisi au jibu halisi.

Jibu rahisi ni lile jibu la juu juu ambalo haliwezi kukuvisha wakati wa changamoto. Kwa mfano kama jibu ni unafanya ili upate fedha, kama utafanya lakini ukakosa fedha, moja kwa moja hutaweza kuendelea kufanya. Kwa sababu lile kusudi ulilonalo unaona halitimii. Au kama jibu lako ni unafanya kwa sababu kila mtu anafanya, au unataka uonekane na wewe unafanya, ni rahisi kuishia njiani, kwa sababu majibu haya hayana uzito wa kushindana na changamoto utakazokutana nazo.

Jibu halisi ni lile ambalo umelitambua baada ya kutafakari kwa kina, pale ambapo umeweka tamaa zako pembeni na kuangalia kwa uhalisia kile hasa unachofanya. Kwa mfano unapoangalia mchango unaotoa kwa wengine kupitia kile unachofanya, unapata hamasa kubwa ya kuendelea hata kama unakutana na changamoto. Kwa sababu unajua wapo watu ambao wananufaika kupitia kile ambacho unafanya. Au unapofanya kitu ili kutumia uwezo mkubwa ambao upo ndani yako, kwa sababu unajua unaweza, basi hutakatishwa tamaa na changamoto utakazokutana nazo.

Ili uweze kufikia jibu halisi la kwa nini unafanya kile unachofanya, ni lazima ujijue wewe mwenyewe, ni lazima ujitambue unataka nini kwenye maisha yako, na upo tayari kutoa nini ili upate kile ambacho unakitaka. Zifuatazo ni hatua muhimu za kuzingatia;

Moja; jitambue wewe ni nani.

Jitambue wewe ni nani na umekuja kufanya nini hapa duniani, jua ni maeneo gani ambayo uko vizuri na jua ni maeneo yapi ambayo una udhaifu. Kwa kujua haya, utaweza kuweka nguvu kubwa kwenye yale maeneo ambayo uko vizuri na kuachana na yale ambayo upo dhaifu. Pia jua ni mambo gani ambayo unapendelea kwenye maisha yako. Changamoto kubwa ambayo inafanya watu wanakuwa na maisha magumu, ni kufanya kazi au biashara ambazo hawazipendi, wanakuwa wanafanya kwa sababu tu wanataka fedha au kwa sababu kila mtu anawategemea wafanye. Unahitaji kuvuka hatua hii.

Mbili; jua ni kipi upo tayari kutoa ili kupata kile unachotaka.

Wote tunajua, na kama ulikuwa hujui jua leo, hakuna kitu cha bure, kila kitu unachotaka na kupata kwenye maisha yako kina gharama yake. Ni lazima uwe tayari kulipa gharama ili kupata kile unachotaka. Na kadiri unavyotaka vitu vikubwa, ndivyo gharama ya kulipa inakuwa kubwa. Jua gharama na kuwa tayari kuilipa, kuwa tayari kuweka juhudi kubwa, kuwa tayari kutoa mchango mkubwa kwenye maisha ya wengine, na ndipo utakapoweza kupata kile unachotaka kufanya.

Kauli moja ninayotaka ujikumbushe ni hii rafiki; huwezi kufanikiwa kama hujawawezesha wengine kufanikiwa. Je wewe ni watu gani umejitoa kuwawezesha kufanikiwa? Wajue na chukua jukumu hilo haraka.
Tatu; kuwa tayari kujifunza na kubadilika.

Hakuna njia moja ambayo ukipita lazima ufike kwenye mafanikio, kila mtu ana njia yake ya kipekee, hivyo hata kama watu watakushauri vitu vya kufanya, bado ni wewe mwenyewe utakayejua njia halisi kwako. Na hii ni changamoto kwa sababu hatuzaliwi na kitabu cha maelekezo ya kile ambacho tunatakiwa kufanya. Hiki ni kitu tunachopaswa kukijua wenyewe, na tunakijua baada ya kujaribu vitu vingi. Ili uweze kufikia kile hasa ambacho ni maalumu kwako, ni lazima ujaribu vitu vingi tofauti tofauti. Katika kujaribu vitu hivi, kuna ambavyo utavipenda sana na utakuwa tayari kuvifanya hata kama ni vigumu. Ili ufikie hatua hii ni lazima uwe tayari kujifunza na kubadilika.

Mtazamo sahihi na chanya juu ya kile unachotaka, ni hitaji muhimu mno kwenye safari ya mafanikio. Hii ni kwa sababu ya ugumu wa safari hii na hivyo kuhitaji kitu cha kukupa hamasa kwenye kila hatua unayopiga. Jua kwa nini hasa unataka kile ambacho unataka, na hakuna kitakachoweza kukurudisha nyuma.
Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)