Binadamu ni viumbe wa kijamii, tunajisikia salama pale ambapo tunakuwa kwenye jamii ambayo inafanya kile ambacho sisi pia tunafanya. Ndiyo maana unakuta kuna watu wanakunywa pombe siyo kwa sababu wanapenda, ila kwa sababu marafiki zao wanakunywa.
Sasa hii inakwenda mpaka kwenye hofu, hakuna mtu ambaye anapenda kuwa na hofu na wasiwasi yeye mwenyewe. Hivyo mtu anapokuwa na hofu au wasiwasi, hutafuta watu wengine ambao wana hofu hiyo au akawaambukize hofu hiyo.
Kwenye jamii zetu, mtu anaona afadhali pale ambapo hofu aliyonayo na wengine pia wanayo. Kwa mfano kama unakumbuka kipindi unasoma, mitihani inapokaribia unakuwa na hofu na wasiwasi. Unaona labda hujajiandaa vizuri, hivyo unawauliza wenzako, wakikujibu kwamba nao hawajajiandaa vizuri unajisikia afadhali kwamba siyo wewe mwenyewe, angalia hapo hujaondoa tatizo, ila umejisikia vizuri kwa kuwa wenzako nao wana tatizo kama lako.
Sasa leo rafiki yangu nataka kukushirikisha namna ya kuondokana na hofu hii ya kuambukizwa, kwa sababu kwa zama hizi tunazoishi, za mitandao ya kijamii, kila siku watu wanaambukiza wenzao hofu zilizowajaa. Mtu anaweza kutumia mtandao wake wa kijamii kuwajaza wenzake hofu ambazo anazo yeye.
SOMA; UKURASA WA 555; Hofu Inavyotumika Kukunyanyasa…
Ninachotaka kukuambia rafiki, usikubali kuambukizwa hofu za wengine. Taarifa nyingi za kutisha na kuogopesha unazopewa na watu, huwa zimeongezwa chumvi. Mara zote mambo siyo mabaya kama ambavyo yanasemwa na watu. Siku zote usiamini kitu juu juu pekee, badala yake chunguza kwa undani.
Kabla hujaingia kwenye mkumbo wa kuamini na kusambaza taarifa za hofu au wasiwasi, jiulize kama ni kitu kinachowezekana, na hata kikiwezekana kama siyo sasa basi huna haja yoyote ya kuhofia.
Usikubali kuambukizwa hofu, itulize akili yako, chukua hatua sahihi. Pia usiwe sehemu ya kusambaza hofu kupitia mitandao na mazungumzo yako na wengine.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)