Moja ya hitaji kubwa sana la kuweza kuishi maisha bora na ya mafanikio, ni kupenda ukweli na kuishi ukweli. Tunapozungumza ukweli mara nyingi tunafikiria kutokusema uongo na vitu kama hivyo. Lakini huwa tunasahau kuhusu tabia zetu wenyewe.
Tumekuwa tunajidanganya sana kuhusu tabia zetu wenyewe. Kila mtu anapenda kutetea tabia yake na kuona ni nzuri, hata kama siyo sahihi. Watu wapo tayari kujitetea hata kama wamekosea ili waonekane kwamba hawajafanya makosa au makosa hayo yalikuwa nje ya uwezo wao. Wanafanikiwa kuwadanganya watu, lakini unajua nini kinatokea tena, wanarudia makosa yale yale kwa sababu wanajua siyo mbaya kufanya.
Nafikiri umewahi kuwa na watu wako wa karibu wawili ambao wamegombana, na kila mtu kwa wakati wake akaja kukueleza ugomvi ulivyokuwa. Kila mtu anakueleza ni jinsi gani mwenzake alivyofanya vibaya na jinsi gani yeye ameonewa. Hakuna atakayekiri kwamba yeye amekosea, na hata akikiri bado ataonesha kwamba hakuanza yeye kukosea.
Ni sawa na mtu anampiga mwenzake na kumuumiza, halafu ukimuuliza anakuambia alimtukana. Sawa kutukanwa ni kosa, lakini kumpiga mtu ni kosa pia, kosa halifuti kosa jingine, bali linafanya mambo yazidi kuwa mabaya.
SOMA; Hii Ndio sababu halisi kwa nini biashara nyingi zinashindwa.
Hivyo rafiki yangu leo nataka kukuambia hili, unapojikuta kwenye matatizo au changamoto yoyote ile, jua kuna namna ambavyo wewe mwenyewe umechagia kuwa pale ulipo. Jua kuna makosa umefanya, jua kuna namna ambavyo tabia yako haikuwa bora ndiyo maana umefika hapo ulipo.
Usijidanganye kwamba tabia yako wewe ni nzuri wakati wote, kuna mambo mengi unayofanya kwa kukosea, kubali ili uweze kujirekebisha na kutokurudia tena makosa hayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK