Mara kwa mara nimekuwa nasema tunachopata kwenye maisha ni kile ambacho tunakitafuta, kile ambacho tunafanyia kazi. Na hii ndiyo maana wale wanaofanya kazi za kawaida wanapata matokeo ya kawaida. Wale wanaofanya kazi za tofauti wanapata matokeo ya tofauti. Pia kadiri mtu anaweka juhudi ndivyo matokeo yake yanakuwa bora.
Lakini swali linabaki hili, kwa nini wengine wawe tayari kuweka juhudi kubwa na wengine wasiwe tayari kufanya hivyo? Kwa nini wengine wakubali kufanya kazi za kawaida wakati wengine wanatafuta kazi za tofauti? Na hapa ndipo nimepata jibu kubwa sana.
Jibu hili ni kwamba tunachopata kwenye maisha yetu, ni kile tunachovumilia, kile tunachokubaliana nacho. Kama kazi tuliyonayo sasa tunaweza kuivumilia, hata kama haitupi kipato cha kutosha, tutaendelea na kazi hiyo. Lakini inapofikia hatua kwamba hatuwezi kuivumilia tena kazi hiyo, tunabadilika na matokeo yetu pia yanabadilika.
Na hii inaeleza vizuri sana kwa nini unakuwa watu wamekaa kwenye kazi moja kwa muda mrefu bila maendeleo, halafu inatokea wamefukuzwa kazi au hawawezi tena kuwa kwenye kazi ile na maisha yao yanabadilika kabisa. Wanapata kazi nyingine bora na kipato chao kinakuwa kizuri. Kilichokuwa kinawafanya wabaki kwenye kazi ile licha ya kwamba haikuwa inawanufaisha ni kwa sababu waliweza kuivumilia.
Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye biashara, unakuta mtu anafanya biashara ndogo eneo fulani, hakui wala haendelei, yuko pale pale miaka yote. Hii ni kwa sababu ameshakubaliana na hali ile na anaweza kuivumilia. Inapotokea hali ambayo inamfanya ashindwe kuvumilia biashara hiyo, lazima atabadilika.
Kama kipato chako ni milioni moja kwa mwezi, siyo kwa sababu ndiyo uwezo wako, bali ni kwa sababu unaweza kuvumilia kupata milioni moja kwa mwezi. Kama ungekuwa huwezi kuvumilia, ungeshafanya jambo la ziada kuongeza kipato hicho. Ni kwa sababu umeshakubali kipato hicho na kuyafanya maisha yako yaendane na kipato hiko. Kama ungekuwa hujakubaliana nacho, ungepambana mpaka upate zaidi ya hapo.
Huu ndiyo ukweli, tunapata kile tunachovumilia, kile ambacho tumekubaliana nacho.
Tufanye nini sasa rafiki yangu ili tutoke hapa tulipo?
Kwanza kabisa tuweke msingi wa maisha yetu, ni kipi ambacho tutakikubali na kukivumilia. Tuweke viwango vya juu ambavyo vinaendana na malengo ya maisha yetu, kisha tuweke juhudi ili kuishi viwango hivi. Tukishatengeneza kipi tunaweza kukivumilia, tutafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK