Moja ya vitu ambavyo tukiviangalia tunaweza kujua kama kazi au biashara unayofanya itakuletea mafanikio au la, ni ule ufahari ulionao kwenye kazi au biashara hiyo.
Je unajisikia ufahari kwa kile unachofanya? Je upo tayari kusimama kifua mbele, mbele ya watu kuwaeleza kwamba hii ni kazi ambayo nimefanya mimi?
Je upo tayari kueleza na kutetea kile unachofanya kiasi kwamba mtu ambaye hata hajui anaanza kupata mwanga wa nini unachofanya?
Wote tunajua ya kwamba kipimo cha kwanza kabisa cha mafanikio ni kupenda kile ambacho unafanya. Kwa sababu unapopenda unaweza kujitoa na kufanya zaidi.
Sasa kupenda unachofanya kunaenda bega kwa bega na kujitoa kwa hatua ya ziada. Kuchukulia kile unachofanya kama kielelezo cha maisha yako, na kutaka kuacha alama ya kipekee kwenye kila unachogusa.
Unapokuwa tayari kuchukua ufahari kupitia kazi yako, unapokuwa tayari kuwaambia watu kwamba hili ni zao langu, ni dalili nzuri kwamba upo tayari kufanikiwa.
Hatari ya kuchukua ufahari kwenye kazi yako ni kuruhusu watu kukukosoa na hata wengine kukukejeli. Wengi watakosoa hata yasiyofaa kukosoa, wengine kwa namna watakavyokuona unaikubali kazi yako, watatafuta njia ya kukukejeli. Si unajua watu wengi hawapendi kazi wanazofanya, hivyo hawataki kuona wengine nao wakipenda kazi zao.
Hatari hizi zisikufanye uache kuchukua ufahari wa kazi yako, badala yake ziwe kichocheo kwako. Watu wanapokukosoa ndiyo urekebishe ili uwe bora zaidi. Wanapokukejeli ndiyo uwaoneshe kwamba hakuna wa kukuondoa kwenye kile unachofanya.
Na hapa haijalishi ni kazi gani unafanya, hata kama unafagia barabara, ifagie kwa ustadi mkubwa, kiasi kwamba utakuwa tayari kujivunia mbele ya wengine kwamba hiyo ni kazi ya mikono yako.
Kazi tunazofanya siyo tu zinatuingizia kipato na kutuletea mafanikio, lakini pia zinaleta maana kwenye maisha yako. Tunaanza kuwa na mchango kwenye maisha ya wengine badala ya kujiangalia sisi wenyewe.
Chukua ufahari kwenye kazi yako, jivunie kwa kile unachofanya na siku zote weka juhudi zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK