Tunaishi kwenye dunia ambayo ina kelele nyingi na za kila aina. Kila ambacho unakifanya kuna watu wengi ambao wanafanya pia.
Kama unafanya biashara, kuna wengi wanaofanya biashara kama yako. Kama umeajiriwa kuwa wengi wanaofanya kazi kama unayofanya wewe.
Kama unaandika kuna wengi wanaoandika kama wewe. Kama unaimba wapo wengi wanaoimba kama wewe. Kwa kifupi hakuna unachoweza kufanya wewe peke yako.
Hata kama utakuja na kitu kipya kabisa, utakapoanza kufanya na watu wakakuona, na wao pia wataanza kufanya. Ndiyo maana ni kawaida kuona sehemu haikuwa na biashara fulani, akaja mtu mmoja na kuanzisha biashara ya aina hiyo, baada ya muda ukashangaa kuona wengi wanafanya biashara kama ile kwenye eneo lile.
Ufanye nini?
Unaweza kuchukua hatua moja kati ya hatua hizi mbili;
Moja; piga kelele zaidi ya wengine.
Kwa sababu tayari kuna kelele, basi unaweza kuchagua kupiga kelele zaidi ya wengine. Kuhakikisha unapiga kelele mpaka kila mtu ajue na wewe upo. Unaweza kukazana kutangaza kwa kila mtu, kitu ambacho na wengine nao wanafanya.
Lakini tatizo la njia hii ni kama ilivyo kwenye tatizo la kupiga kelele, utachoka na kuumia na matokeo unayopata ni madogo. Utapiga kelele sana, lakini kwa sababu upo katikati ya kelele nyingi, utasikika na wachache mno. Nguvu nyingi matokeo kidogo. Faida ya kupiga kelele ni rahisi, huhitaji kujitoa zaidi, ni kelele tu.
Mbili; jitenge na kujitofautisha na kelele.
Hapa unaamua kujitoa kabisa kwenye kelele hizo, unajiweka pembeni, ambapo hakuna kelele kiasi kwamba huhitaji kutumia nguvu nyingi kuwafikia wale unaotaka kuwafikia.
Hapa unajitofautisha, unakuwa bora zaidi ya mtu mwingine yeyote ambaye amewahi kujaribu kufanya kile unachofanya wewe. Kwa kifupi unakuwa bora zaidi kwenye kile unachofanya, unatoa kitu ambacho watu hawajawahi kupata. Na kwa kuwa ukiwa bora watu wanaiga, basi ubora huu unautoa kila siku, kila siku.
Faida za kujitofautisha ni kwamba unajitengenezea watu wanaokwenda na wewe, huhitaji kupiga kelele ili kuwafikia watu, bali unawavutia watu wakufuate wao wenyewe. Unapata watu bora ambao pia watakuletea watu bora. Hasara yake ni kwamba ni vigumu kujitofautisha, unahitaji kujitoa na kuweka juhudi, unahitaji kufikiria tofauti na wengine, kitu ambacho ni kigumu kwa maisha yetu ya kawaida.
Nimalize kwa kusema, kufanya kilicho rahisi kunakuletea matokeo ya kawaida, matokeo ya hovyo. Kufanya kilicho kigumu kunakuletea matokeo bora kabisa. Chagua vyema, unataka kupiga kelele au unataka kuwa tofauti?
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK