Kila mtu kuna biashara ambayo anaifanya kwenye maisha yako.
Iwe umeajiriwa au umejiajiri, kuna thamani ambayo unaitoa kwa wengine na wao kukulipa kwa thamani hii. Kila mmoja wetu kuna kitu anachouza kwa wengine ili kupata kipato. Kuna ambao wanauza muda wao, wengine wanauza utaalamu wao. Wapo wanaouza nguvu zao, wengine wanauza mawazo yao.
Kwa kuwa kila mmoja wetu yupo kwenye biashara, kuna kitu kimoja muhimu tunapaswa kukijua. Kitu hiki ni kwamba kila mmoja wetu ana biashara mbili ambazo anazo. Ni muhimu sana kuzijua biashara hizi mbili, maana mafanikio yapo kwenye biashara hizi mbili.
Biashara ya kwanza ni ile ambayo unaifanya sasa.
Kile ambacho unafanya sasa ili kuingiza kipato ndiyo biashara yako ya kwanza. Hii ni biashara ambayo unayo sasa, ambapo unahitaji kuweka juhudi ili kupata kipato cha kuendesha maisha yako. Pia unahitaji kutoa thamani kubwa kwa wengine.
Biashara ya pili ni ile ambayo unaiendea.
Hii ni ile biashara ambayo unaiendea, ile biashara ambayo unakua kutokana na namna unavyofanya biashara yako. Tunaweza kusema pia hii ni ile biashara ambayo unafikiria kuifikia. Unaweza kuwa na biashara sasa, lakini malengo na mipango yako ni kuwa na biashara kubwa kuliko uliyonayo sasa. Unakuwa na maono ya kuwa na biashara kubwa na yenye mafanikio zaidi.
Changamoto.
Sasa changamoto inaanzia hapa, watu huweka juhudi zao kwenye biashara moja na kusahau nyingine. Mara nyingi watu wamekuwa wakifikiria zaidi biashara wanayofanya sasa na kusahau ile biashara ambayo wanaiendea. Au wengine wamekuwa wanafikiria sana ile biashara wanayoiendea na kusahau biashara wanayofanya sasa.
Changamoto hii imekuwa na matatizo mawili, tatizo la kwanza ni kudumaa kwa biashara ambayo mtu anafanya. Miaka na miaka mtu anakuwa pale pale hakuna hatua kubwa anayopiga, hii ni kwa sababu anashindwa kufikiria biashara anayoiendea. Anaishia kufanya mambo kwa mazoea. Tatizo la pili ni mtu kushindwa kabisa kufanya biashara, hii ni kwa sababu anakuwa anafikiria biashara ile kubwa a kuona kuanza na ndogo ni kupoteza muda.
SOMA; BIASHARA LEO; Cross-Selling Na Up-Selling, Mbinu Mbili Za Kuongeza Mauzo Bila Kuongeza Wateja.
Suluhisho.
Popote ulipo, endesha na simamia vizuri biashara zako zote mbili. Kwa biashara unayofanya sasa hakikisha unaifanya kwa ubora wa hali ya juu, unawapa watu thamani. Lakini usijisahau na kubaki hapo, badala yake kila mara ifikirie ile biashara ambayo unaiendea, jua hatua za kuchukua kila siku ili uweze kufika kwenye kilele cha biashara ile unayoitaka wewe.
Ukienda vizuri na biashara hizi mbili, hutabaki hapo ulipo, hutafanya mambo kwa mazoea na muhimu zaidi mafanikio hayawezi kukukwepa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK