Habari za jumapili ya leo rafiki yangu?
Karibu kwenye makala yetu nyingine ya NYEUSI NA NYEUPE, hapa tunauangalia ukweli wenyewe kama yulivyo, hatufuniki au kuficha chochote. Jembe tunaliita jembe na kijiko tunakiita kijiko, hata kama itakuumiza kwa namna yoyote ile. Kama ambavyo tunajua, kitu pekee kinachoweza kukuweka huru ni kuujua ukweli. Unaweza kuukataa ukweli, unaweza kuukwepa ukweli lakini hayo yote hayawezi kubadili ukweli.
Leo tunakwenda kuangalia eneo moja muhimu mno, eneo ambalo nimeona wengi wakilishangaa na wengine kujikuta kwenye mkumbo bila ya kujua wameingiaje, na mbaya zaidi hawajui watatokaje. Hili ni eneo muhimu kwa sababu kila siku tunakutana na mambo haya.

Nunua gazeti lolote kusoma na habari utakayokutana nayo ukurasa wa mbele ni habari hasi au inayokujaza hofu. Ukisoma vichwa vya mbele vya habari pekee, na ukaondoka bila ya kuangalia ndani, unaweza kusema dunia imefika mwisho kabisa, hakuna tena jambo zuri linaloweza kufanyika.
Fungulia habari yoyote kwenye televisheni au redio, na habari za kwanza unazokutana nazo ni habari ambazo ni hasi, habari ambazo zitakupa hofu kubwa. Utasikia mtu kajiua au kaua wenzake, utasikia mapigano ya watu au waasi na serkali. Utasikia kila aina ya habari ambayo itakufanya uone dunia inaisha kabisa.

Zamani mambo haya yalikuwa yanaishia kwenye magazeti, redio na tv, lakini sasa hivi kimekuja chombo kipya cha habari ambacho kinachochea moto wa habari hasi. Chombo hiki kimekuwa hatari sana kwa sababu kinawafikia watu wengi kwa haraka mno na kwa masaa yote 24 ya siku. chombo hiki ndiyo kimenifanya niandike leo kwa sababu naona namna watu wengi wakipotezwa na chombo hiki, bila ya kuja hatua za kuchukua.

Chombo ninachozungumzia hapa ni mitandao ya kijamii. Mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya kupashana habari kwa urahisi siku hizi. Huhitaji kusubiri mpaka muda wa taarifa ya habari, au usubiri mpaka magazeti yachapwe, mitandao ya kijamii itakupa habari pale pale inapotokea. Kwa mfano ikitokea ajali, mpaka uisikie kwenye habari ni usiku wakati wa taarifa za habari, au upewe kama habari mpasuko baada ya muda fulani kupita, chombo cha habari kijidhihirishie kwamba habari ni ya kweli, pia utasubiri mpaka kesho yake ndiyo usome kwenye magazeti. Lakini hali haipo hivyo kwenye mitandao ya kijamii, ajali imetokea sasa, kama kuna mwenye simu na mtandao upo basi dakika hiyo hiyo picha za ajali zipo kwenye mitandao.
Hivyo mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya kusambaza habari hasi na hofu kwa urahisi zaidi na kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja. Hii imeleta changamoto kwa wengine.

SOMA; MITANDAO YA KIJAMII; JE NI BARAKA AMA LAANA KWAKO?

Kabla sijaendelea nataka nikiri kwamba mitandao ya kijamii imekuwa na faida kubwa sana kwetu, imeweza kutuunganisha na hata kutuingizia kipato. Lakini kila chenye faida huja na kasoro zake. Na hapa tunaangalia kasoro moja ya mitandao hii, ambayo kila mtumiaji anapaswa kuijua ili kuweza kuiepuka.

Kwa nini habari hasi na zenye hofu zinapewa kipaumbele kikubwa?

Tuanze na mifano hai kabisa ya kila siku;
Kuna mambo mengi mazuri yanafanywa na watu, lakini hutaona watu wakiyapa kipaumbele, ila pale jambo moja baya linapofanywa, kila mtu atajua kuhusu jambo hilo.

Kuna tafiti nyingi sana ambazo zinafanywa kila siku na watafiti wa kijamii, kisayansi na kitabibu, lakini hutaona watu wakizijadili na kushadadia. Ila unapokuja utafiti kwamba katika kila watanzania wanne, mmoja wao ana matatizo ya akili, kila mtu ataijua na kujadili tafiti hiyo.

SOMA; Mambo 4 Yanayosababisha Uwe Na Fikra Hasi.

Kuna madaktari wengi wanafanya kazi zao kwa kujituma, wapo wanaokesha kwenye kazi zao kuhakikisha wagonjwa wao wanakuwa na afya njema, hutaona madaktari hawa wakiwa mjadala wa kitaifa. Ila anapotokea daktari mmoja akafanya makosa na mgonjwa akapata matatizo basi itakuwa habari ambayo kila mtu ataijua na kuijadili, watu watatoka kulaani vile wawezavyo.

Kuna walimu wengi wanafanya kazi zao kwa moyo wa kujitoa. Walimu hao wapo katika mazingira mabovu, lakini wanaendelea kuweka juhudi kuhakikisha wanatoa mchango bora kwa kujenga taifa letu, wanafanya mambo ambayo hata hawalipwi. Lakini hutasikia habari za walimu wa aina hii zikiwa gumzo la kitaifa, ili kuwapa moyo na kuwahamasisha wengine nao kuwa kama wao. Lakini inapotokea mwalimu mmoja amefanya kosa kwenye kazi yake, ambalo linapelekea hali ya elimu kutokuwa nzuri, kila mtu atajua, kila mtu atajadili, kila mtu atalaani. Hata asiye na habari za kutosha atakuwa na la kusema.
Kwa haya na mengine mengi yanayotokea kwenye maisha yetu ya kila siku, ni lazima tujiulize kwa nini habari hasi zinapewa kipaumbele kuliko habari chanya? Na hapa ndipo tunahitaji kuzama ndani, ili kuja na nyeusi na nyeupe kuhusu hali hii.

Sababu ya kwanza; tunaishi maisha ya miaka 3000 kabla ya kuja kwa Kristo (3000B.C)
Hii ina maana gani?
Hapo zamani sana, huenda mbali zaidi ya mwaka nilioandika hapo, maisha ya wanadamu yalikuwa hatarini. Binadamu walikuwa wakiishi kwenye mazingira ambayo siyo salama, walikuwa wakiishi maporini pamoja na wanyama. Hivyo wakati wowote mtu angeweza kuliwa na mnyama mkali, kudhuriwa na wadudu na hata kudhurika na mazingira hayo hatari.

Hivyo basi, wale wazee wetu wa enzi hizo wakajifunza namba ya kuhakikisha wanapona, na hivyo kujifunza namna ya kuiona hatari kabla hata haijatokea. Kwa hiyo kama yupo porini na kusikia kishindo inabidi aanze kukimbia hata kama hajui ni nini kimesababisha kishindo hiko. Huenda ni mnyama mkali anakuja, au huenda ni jiwe limeanguka. Kwa kukimbia kabla ya kuona kishindo kimesababishwa na nini, kulipelekea mtu kuokoa maisha yake. Kama kishindo ni cha mnyama, basi amepona kuliwa, na kama kishindo ni cha jiwe, basi hakuna ambacho amepoteza kwa kukimbia.

Kwa kifupi, risk ya kukimbia ilikuwa ndogo kiliko kukaa wakati hujui ni kipi kinakuja. Hivyo watu walijifunza kuangalia mambo hasi kwanza kwenye kila mazingira waliyopo. Hali hii waliirithishwa kwa vizazi vilivyofuata na mpaka sasa imefika kwetu. Akili zetu zinatoa kipaumbele kwa mambo hasi na ya hofu kuliko mambo chanya. Na miili yetu ina mfumo wa kuhakikisha tunapona kwenye mazingira hayo. Nafikiri umewahi kufukuzwa na mbwa na kujikuta unapanda ukuta ambao ukija kujaribu kuupanda tena huwezi, hivi ndivyo mwili ulivyojipanga kuhakikisha unakuwa salama.

SOMA; Dalili Sita(6) Kwamba Una Fikra Hasi Zinazokuzuia Kufikia Mafanikio Na Jinsi Ya Kuondokana Nazo.

Sababu ya pili; kuhakikisha siyo sisi au siyo watu tunaowajua.
Inapotokea hali fulani ambayo siyo nzuri, kwa mfano ajali, huwa tunapenda kujua wa kwanza ili kuhakikisha sisi hatuhusiki moja kwa moja, au wale ambao ni wa karibu kwetu hawahusiki. Hii pia ni zao la hofu ile ambayo tunaishi nayo kwamba mazingira siyo mazuri. Hivyo tunapendelea kujua habari hasi ili kujihakikishia kwamba sisi wenyewe na wale wa karibu yetu hawahusiki na wapo salama kabisa.

Sababu ya tatu; kuwa wa kwanza kutoa habari za ukombozi, za kishujaa.
Kwa sababu watu wengi wanapenda habari hasi, na wanazichukulia kwa uzito, hii inakuwa ni ufahari kwa yule ambaye atatoa habari hiyo kwa mara ya kwanza. Hivyo mtu anapopata habari hasi, kabla hata hajaielewa au kuijua vizuri, anakimbilia kuisambaza ili awe wa kwanza kutoa habari hiyo.
Kuna kiufahari fulani ambapo watu wanakipata pale wanapoona ni wa kwanza kutoa habari fulani ambayo watu wanajali sana. Hivyo hii inawasukuma watu kuhakikisha wanatoa habari hizo wa kwanza kabisa kabla wengine hawajazitoa. Ndiyo maana mara nyingi habari hasi zinazotolewa mwanzoni huwa ni za uongo.

Kwa mfano ajali imetokea, mtu aliyepo kwenye ajali, au aliyefika mapema, atatoa picha haraka na kusema ajali mbaya sana imetokea, watu wengi mno wamefariki. Hapa anasambaza habari yenye hofu kubwa kwa wengine. Maana unaposema watu wengi sana, ni watu wangapi. Kwa nini mtu kama huyu asingesubiri miili ikatolewa, ikahesabiwa wangapi wamefariki, wangapi majeruhi na kisha akawajulisha watu kwamba ajali imetokea na watu watano wamefariki. Wote tunajua sababu ni kwa nini, mpaka asubiri watu watolewe, atachelewa kutoa habari, atakuta wengine wameshaitoa. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa wale ambao wanapokea habari na kuzisambaza kwa wengine

Tufanye nini ili kuondoka kwenye mkumbo huu wa habari hasi na zenye hofu?
Kama ambavyo nimekuwa nakuahidi kupitia kipengele hiki cha nyeusi na nyeupe, sikuachi hivi hivi, bali nakupa hatua za kuchukua ili kuondokana na hali hii.

Moja; tambua kwamba maisha ni bora sana sasa kuliko siku zilizopita.
Haijalishi vyombo vya habari vinakuambia au kukuhubiria nini, maisha tunayoishi sasa ni bora kuliko ya siku zilizopita. Kwa kipimo chochote na kwa viwango vyovyote, maisha ni bora, ulinzi ni mzuri na mazingira ni rafiki kwa chochote unachotaka kufanya. Usipokee hofu na habari hasi kama zinavyotolewa.

Mbili; chunguza kila habari hasi au yenye hofu unayopokea.
Siwe tu mtu wa kupokea kila habari na kuichukua kama ilivyo na wewe kuisambaza. Badala yake ichunguze, hoji na dadisi. Jiulize habari hiyo imebeba ukweli kiasi gani. Je ina uhalisia kiasi gani. Na je ina msaada gani kwenye maisha ya wengine.

Tatu; usiwe mtu wa kusambaza habari hasi.
Unapopokea habari, usikimbilie kuisambaza. Ichunguze kwa makini na ona kama kuna manufaa yoyote, kama hakuna basi achana nayo, wala usiiseme kwa wengine. Usijijengee sifa ya kuwa mtu wa kutoa habari hasi na zenye hofu.

SOMA; Huyu Ndiye ‘STAA’ Muhimu Unayepaswa Kumfuatilia Kila Siku Kwenye Maisha Yako Ili Ufanikiwe.

Nne; jua biashara kuu ya habari ni kujenga hofu kwa watu.
Vyombo vya habari vinahitaji wasomaji na watazamaji ili kuingiza kipato, iwe ni kwa wao kulipa moja kwa moja au kupata matangazo. Hivyo kila chombo kinakazana kupata wasomaji wengi. Njia rahisi ya kufanya hivi ni kuwajaza watu hofu, ili wakae kwenye vyombo hivyo kupata habari lazima wawe na hofu kwamba kuna kitu wanakosa au kuna kitu lazima wakijue la sivyo maisha yao yatakuwa hovyo.

Tano; usisome habari za mbele za magazeti, usianze siku yako kwa kuangalia au kusikiliza habari na usiangalie habari kwenye tv.
Chagua aina ya habari unazotaka kupata, labda za biashara, afya, uchumi na nyingine kama hizo. Habari zisizoendana na hizo achana nazo. Hatujaikia mwisho wa dunia na hata tukifikia utasikia hata kwa wengine, siyo lazima uwe karibu na kila habari. Halafu hakuna kikubwa unachokosa kama hutafuatilia habari kila siku.

Hivyo ndivyo habari hasi na zenye hofu zinatumika na wengine kujitengenezea kipato huku zikiwafanya wanaozipokea kuona maisha siyo mazuri. Epuka kabisa habari hizi hasi na zenye hofu. Maisha ni bora sana sasa kuliko siku za nyuma.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK