Hupaswi kuwa na chuki kwenye maisha yako, kwa sababu chuki inaharibu mambo mengi kwenye maisha yako, hasa chuki hiyo inapokuwa juu ya wengine.

Lakini kuna vitu ambavyo tunapaswa kuvichukia, ili visiweze kukudhuru. Na kwa sisi wana mafanikio, sisi ambao tumekataa kuwa kawaida na kuamua kuwa bora zaidi, sisi ambao tunataka mafanikio ya kudumu kwenye maisha yetu na siyo ya kuja na kupotea, kuna vitu viwili tunapaswa kuvichukia.

Vitu hivi viwili vimebeba sumu kubwa ambayo inaweza kutuondoa kabisa kwenye safari hii ya mafanikio. Ni wajibu wetu kujua vitu hivi na kuviepuka haraka iwezekanavyo.

Kitu cha kwanza; maisha rahisi.

Maisha rahisi ni sumu kubwa ya mafanikio, ndiyo tunapenda maisha yawe rahisi, lakini kama maisha yataenda hivi, bila ya changamoto, kila tunachotaka tunapata na tunapata kirahisi, ni hatari kubwa. Hii ni kwa sababu binadamu tuna tabia ya kujisahau hivyo mambo yanapokuwa rahisi, tunajiona tayari sisi ni wa ngazi nyingine, tunaona tumeshaweza kula kitu na hivyo kuanza kufanya kwa mazoea. Na hapa ndipo anguko kuu linapotokea.

Wewe mwenyewe ni shahidi, kwa watu ambao wamepitia maisha rahisi na baadaye mambo yakabadilika sana kwao. Mpaka watu wanajiuliza imekuwaje.

Kitu cha pili; mafanikio makubwa ya haraka.

Hii ni sumu nyingine ambayo inaingia kirahisi kwenye akili zetu na kutuharibu kabisa. Kuna watu ambao wamekutana na fursa za kipekee kwa wakati ambao wengine hawajaona fursa hizo. Kwa kupata fursa hizi zinawapa nafasi ya kupata mafanikio makubwa sana ndani ya muda mfupi. Baada ya mafanikio haya, wengi hujikuta wakiwa vibaya kuliko hata walivyokuwa kabla ya mafanikio hayo ya haraka.

Mafanikio makubwa na ya haraka yamekuwa yanawaharibu watu kwa sababu watu wanakuwa hawajajiandaa kiakili na kimtazamo. Unajua unapoenda na mafanikio yanayokua kwa kiwango fulani, na wewe unaendelea kukua, hivyo unajifunza namna ya kwenda na mafanikio yako. Ila mafanikio yanapotokea kama mafuriko, ni changamoto kubwa kwa sababu mtu anakuwa hana maandalizi, anajikuta akifanya maamuzi ambayo siyo bora kwake.

Kwa vyovyote vile, usitamani maisha yawe rahisi, na wala usiombe mafanikio makubwa na ya haraka. Furahia safari yako ya mafanikio, kwa kufanyia kazi changamoto unazokutana nazo, na kupiga hatua moja kwa wakati.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK