Habari mpendwa Rafiki na Msomaji wa mtandao wa AMKA MTANZANIA? Natumaini hujambo na unaendelea vyema katika shughuli zako za kila siku za kukupatia kipato na kugusa maisha ya watu wengine, yaani kuishi maisha ya maana hapa duniani.  Karibu mpendwa rafiki katika makala yetu ya leo tuweze kujifunza kwa pamoja. Natumaini rafiki yangu unajua kuwa kwa sasa tunaishi katika karni ya ishirini na moja (21) na tupo katika zama za taarifa ili ufanikiwe kwa sasa unahitaji taarifa sahihi na kwa wakati sahihi.  Na zama hizi za taarifa zinahitaji kila mtu awe na maarifa sahihi ili yaweze kumsaidia kuishi maisha ambayo ni sahihi na yenye maana kwa ujumla.

Mpendwa rafiki na msomaji wa AMKA MTANZANIA, karibu katika makala yetu ya leo ambapo tutajifunza falsafa moja kutoka kwa mwanafalsafa mkubwa aliyeishi na kuzaliwa kabla ya Yesu kuzaliwa na siyo mwingine bali ni mwanafalsafa Plato. Mwanafalsafa Plato aliwahi kusema, ‘’ a house that has a library in, it has a soul’’ akiwa na maana ya kwamba nyumba ambayo ina maktaba ndani ni nyumba ambayo ina roho. Kila mtu anaishi katika nyumba iwe ni nyumba yako uliojenga au uliopanga lakini unaishi katika nyumba. Je falsafa hii inagusa namna gani?

SOMA; Sehemu Kumi (10) Unazoweza Kupata Muda Wa Kujiongezea Maarifa Kupitia Kusoma Vitabu.

Ukweli ni kwamba nyumba nyingi wanazoishi watu hazina maktaba ndani. Nyumba nyingi ni mabingwa wa kuwa na makochi makubwa, flat screen tv nk. Jaribu kupita nyumba kumi katika jamii unayoishi halafu angalia ni nyumba gani wana maktaba au wana vitabu ndani. Wengi wanapenda kununua vitu kama cd za nyimbo, tamthilia mbalimbali na kukaa nazo kuliko kununua vitabu. Nyumba nyingi ni maskini wa vitabu na nyumba nyingi hazina roho na roho ya nyumba ni vitabu. Katika vitabu tunapata maarifa ambayo yanatusaidia kuishi maisha sahihi.

Maisha ya wanafalsafa wengi ni maisha mazuri sana yenye furaha, amani na mafanikio na kama ukifuatilia maisha ya mwanafalsafa hakika utaujua ukweli nayo kweli itakuweka huru. Yatupasa tuanze kuamka katika majumba yetu badala ya mgeni kuja kwako na kumfungulia tv aangalie mpe kitabu asome aonje roho ya nyumba yako. Akisoma hata ukurasa mmoja atakua ameongeza thamani katika maisha yake. Anza kununua vitabu na kuweka maktaba yako ndogo nyumbani. Katika nyumba yako hakikisha unaishi weka sehemu ya maktaba ambayo ndio roho ya nyumba yako.

Haitoshi kuwa na maktaba tu bali uhai wa maktaba ni wasomaji wa vitabu. Vitabu vinunuliwe na visomwe. Tukiwa tunajenga utamaduni wa kusoma vitabu kwa kila familia tutajenga jamii bora sana na tutafanya dunia kuwa sehemu salama ya kuuishi kwa kila mmoja wetu. Tuanze kwa kila familia kuwa na maktaba za vitabu kwetu. Tuache mambo ambayo hayana faida kubwa katika maisha yetu bali tujenge kizazi imara na jamii imara. Kila mtoto alelewe katika utamaduni wa kusoma vitabu kwani ndio njia sahihi ya kumfundisha mtoto kuvua samaki na siyo kumpa samaki.  Kama unaona ni fahari kumwachia mtoto aangalie sana tv bila kusoma vitabu ujue unamharibu mwenyewe mtoto wako.

SOMA; KITABU CHA APRIL; THE SEVEN HABITS OF HIGHLY EFFECTIVE PEOPLE (Tabia Saba Za Watu Wenye Ufanisi Wa Hali Ya Juu).

Mpendwa rafiki, mwanafalsafa na mwandishi  Jim rohn aliyezaliwa karni ya ishirini (20) na kufariki dunia karni ya ishirini NA moja ( Septemba 17,1930- Desemba 5, 2009) naye aliwahi kusema, ‘’ successful people have  big libraries. The rest have big flat screen Tvs in their home’’ akiwa na maana ya kwamba watu waliofanikiwa wamekuwa na maktaba katika nyumba zao na wengine waliobakia wamekuwa na tv kubwa za kisasa.  Hivyo basi, unaona mwanafalsafa huyu anavyotuambia ukweli kama alivyotuambia mwanafalsafa Plato. Plato yeye aliishi na kuzaliwa kabla hata ya Yesu lakini leo maneno yake yanadhihirika na mwanafalsafa aliyefariki katika karni hii 21 naye anatuambia ukweli huo huo.

Siku hizi katika nyumba nyingi fasheni ni kuweka flat screen ili naye aende na wakati kama wenzake wanavyoenda. Lakini ukiangalia katika upande wa roho ya nyumba hakuna kitu. Ukiwa na  maktaba ndani ndio unaonesha uhai wa nyumba yako kuliko kuwa na tv kubwa nyumbani. Tunatakiwa kuishi maisha ya kifalsafa yaani falsafa ni msingi wa maisha ya binadamu ambayo unaelezea ukweli kupitia uhalisia wa dunia. Jinsi unavyofikiria na unavyoishi unatumia falsafa bila ya wewe mwenyewe kujua.
Kila nyumba inatakiwa ianze leo kuwa na maktaba na kuanza kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu kila siku na kuachana na kutumia muda mwingi katika kuangalia luninga. Kuangalia luninga sana na kwa muda mrefu ni faida hasi kiafya lakini ukisoma vitabu sana ni faida chanya kiafya.  Kuwa balozi wa kuhamasisha jambo hili sehemu yoyote uliyopo. Tuna kazi kubwa kwa kila mmoja wetu kusaidiana ili kufuta ujinga. Taifa haliwezi kukua kama tukikaa na kushinda katika makochi na kuangalia tv taifa litakuwa kama watu wakifanya kazi kwa juhudi na maarifa.

SOMA; Hivi Ndivyo Tabia Ya Kupenda Kujisomea Ilivyoboresha Maisha Yangu. Inawezekana Hata Kwako Pia.

Sasa katika kufanya kazi kwa juhudi haitoshi bila kuwa na maarifa ya kutosha. Maarifa tunayapata katika vitabu vyetu vinavyopatikana katika maktaba zetu. Habari njema ni kwamba katika zama za taarifa unaweza kuwa na maktaba yako ndani ya simu yako imejaa vitabu, kompyuta, na nk. Unatakiwa kutembea na maktaba sehemu yoyote unayokwenda kuanzia leo.

Hatua ya kuchukua; anza leo kutembea na kitabu ukipata muda sehemu yoyote ile chukua kitabu soma. Katika simu yako kama umejaza vitabu ambavyo havina faida chanya futa weka vitabu, kama kwenye kompyuta yako umejaza nyimbo, movie za aina mbalimbali na sirizi (mpangilio wa matukio) mbalimbali futa na weka vitabu. Kama familia yako haina kitabu anza leo kutenga eneo la maktaba na muanze desturi ya kusoma kitabu. Karibu pia katika klabu yetu ya kusoma vitabu viwili kwa wiki. Katika kundi hili tunapokea watu makini ambao hawana sababu yaani excuses. Kujiunga na kikundi hiki tuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba +255717101505 ili uweze kujifunza kwa hamasa na kwa nidhamu bila kuahirisha.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com