Siku za hivi karibuni kumekuwa na matangazo mengi ya vyeti kupotea. Kila chapisho la gazeti lina zaidi ya ukurasa mzima wenye matangazo ya kupotea kwa vyeti.

Kikubwa cha kushangaza ni kwamba sehemu kubwa ya vyeti vinavyotangazwa kupotea, vimepotea miaka mingi iliyopita. Vipo vyeti vinatangazwa kupotea miaka 10 mpaka 20 iliyopita.

Najua wote tunajua kwa nini kumekuwa na ongezeko la watu kutangaza kupotelewa na vyeti, hicho siyo ninachotaka tujadili leo. Leo tutajadili jinsi unavyoweza kupata cheti ambacho hakiwezi kupotea, cheti ambacho utadumu nacho milele na kitakuwa a manufaa makubwa kwako.

Hatua ya kwanza;

Jamii zetu zimeweka thamani kubwa sana kwenye makaratasi, ambayo yameandikwa maksi ambazo tulipata wakati tunasoma. Makaratasi haya yamepewa kipaumbele kikubwa kuliko thamani ambayo tunaweza kuitoa. Na hii ndiyo sababu vyeti vinaonekana ni muhimu sana.

Lakini cheti ambacho ulikipata miaka 20 iliyopita, unafikiri kina uhalisia gani leo? Ndiyo miaka 20 iliyopita uliweza kufaulu masomo uliyopimwa kwa kipindi hicho, je kujibu maswali miaka 20 iliyopita bado kunaleta uhalisia wa leo?

Hatua ya pili;

Tengeneza cheti chako mwenyewe. Cheti hiki unachopewa kwenye mfumo wa elimu ni muhimu, lakini cheti muhimu zaidi ni kile unachotengeneza wewe mwenyewe. Hiki ni cheti ambacho hakiwezi kupotea, kwa sababu cheti hicho ni wewe mwenyewe.

Cheti chako unakitengeneza kwa kuchagua kufanya kitu kwa wengine, ambacho kinawaongezea thamani na kufanya maisha yao kuwa bora zaidi. Toa thamani kwa wengine, na wao watakuchukulia wewe kama mtu wa muhimu kwao, watakutegemea kwa kile unachowapa, na hiki ndiyo cheti ambacho huwezi kukipoteza.

Ukishakuwa na kitu ambacho wengine wanakutegemea, wanajua wakija kwako lazima wapate kile wanachotaka, hiki ni cheti cha kudumu kwenye maisha yako.

Hatua ya tatu;

Safisha cheti chako, kiboreshe zaidi kila siku. Kama ambavyo watu wanafanya kwa vyeti vyao vya darasani, kuviboresha kwa kuongeza viwango vyao vya elimu, wewe pia boresha cheti chako. Boresha cheti chako kwa kuongeza thamani unayotoa kila siku. kile ambacho umechagua kufanya, chagua kuwa bora zaidi kila siku. Usifanye kwa mazoea, bali kila siku angalia namna unavyoweza kuboresha zaidi. Angalia mahitaji ya watu na wapatie, angalia hata yale ambayo bado wao hawajayajua.

Hitimisho;

Hivi ndivyo unavyotengeneza cheti chako mwenyewe, cheti kitakachokupa kazi popote utakapokwenda, na cheti ambacho hakiwezi kupotea kamwe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK