Kuna kauli ya wahenga kwamba kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza

Hii ni kauli ambayo ina uhalisia mkubwa kwenye maisha yetu ya kila siku. na kwenye uendeshaji na ukuzaji wa biashara zetu, ina ukweli nusu na uongo nusu.

Kila siku watu wamekuwa wanajifunza na kushauriwa mbinu mbalimbali za kukuza biashara zao ili kufanikiwa. Zipo mbinu ambazo zinawasaidia, na nyingi zinawapotezea muda.

Leo nataka nikushirikishe misingi mikuu miwili ya kukuza biashara yoyote ile. Uzuri wa misingi ni kwamba inafanya kazi popote inapotumiwa kwa usahihi.

Ukuaji wa biashara yoyote unaanzia kwenye mauzo, kama hakuna mauzo biashara haiwezi kukua kwa namna yoyote ile. Hakuna kitu kinachotokea kwenye biashara mpaka pale unapofanikiwa kumuuzia mtu kitu, unapoweza kumshawishi mtu akatoa fedha yake kununua unachouza.

Msingi wa kwanza; hakikisha una bidhaa au huduma bora kabisa.

Watu wana shinda,

Watu wana mahitaji,

Watu wana maumivu…

Je bidhaa au huduma unayotoa, inayaboreshaje maisha ya watu kuwa bora zaidi.

Hatua ya kwanza hakikisha una bidhaa au huduma bora kabisa, yenye thamani kubwa na inayoweza kuwafanya wengine kuwa na maisha bora.

Hapa ndipo nusu ya ukweli wa kauli ile ya wahenga kuhusu kizuri, ni lazima uwe na kizuri kweli.

Msingi wa pili; jifunze kuuza bidhaa au huduma yako, na iuze kweli.

Kuwa na bidhaa au huduma bora, haimaanishi kwamba watu watajipanga kuja kuinunua, ni mpaka wajue kama kweli ipo na uweze kuwashawishi kununua.

Ni lazima uweze kuipigia debe bidhaa au huduma wako, ni lazima uweze kuwashawishi watu waache matumizi mengine ya fedha zao na wakupe wewe fedha hizo. Hii ni kazi ambayo unahitaji kuifanya ili uweze kuuza na hatimaye kukuza biashara yako.

Hapa ndipo uongo wa kauli ya kizuri chajiuza, unahitaji kuwa na kitu kizuri, lakini hakitajiuza chenyewe unahitaji kukiuza wewe. Hii ni kwa sababu wapo wengi wanaofanya kile unachofanya wewe, hivyo wateja wako wanakutana na kelele nyingi, lazima wewe uweze kuvuka kelele hizo na kuwapa kile hasa wanachotaka.

Hii ndiyo misingi miwili, itumie kwenye biashara yoyote unayofanya, uone kama hutafanikiwa kupitia biashara hiyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK