Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Ni imani yangu kwamba upo vizuri na unaendelea kuweka juhudi kubwa ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Kumbuka kwamba falsafa ni sehemu muhimu ya maisha yetu ya kila siku, jijengee falsafa imara itakayokusaidia kufanya maamuzi bora ya maisha yako.

Ipo kanuni ya Dhahabu (GOLDEN RULE), ambayo ndiyo kanuni kuu inayotupa maadili ya kuishi vyema kwenye jamii zetu. Dini zote zinafundisha kanuni hii, jamii zote zilizostaarabika zinafundisha kanuni hii. Ni kanuni muhimu, ambayo kwa kuijua na kuiishi, maisha yako yanakuwa bora. Na siyo maisha yako pekee, bali hata ya wale wanaokuzunguka yanakuwa bora sana.

Kanuni hii ya dhahabu ina tafsiri tofauti kulingana na jamii au dini ambayo unaifuata. Lakini msingi wa kanuni hii ni huu; WAFANYIE WENGINE KILE AMBACHO UNGEPENDA WAKUFANYIE. Ni kanuni rahisi, inayoeleweka na ambayo tukiweza kuiishi, maisha yatakuwa bora na dunia kuwa sehemu salama kabisa ya kila mtu kuishi.

Kanuni ya dhahabu inatutaka kutokujiangalia sisi wenyewe pekee, bali tuwaangalie na wale ambao wanatuzunguka. Kama kuna kitu ambacho sisi tunakipenda, basi tujue na wengine pia wanapenda kitu hicho. Na kama kipo kitu ambacho sisi hatupendi, basi na wenzetu pia hawakipendi. Kwa kanuni hii, inatupasa tutoe mchango mzuri kwa wengine na kuepuka kuwaumiza wengine.

Kanuni hii ya dhahabu ipo wazi kwa kila mtu, haijalishi rangi, kabila au hata dini. Bali ni kanuni ambayo inamfaa kila mtu na inahakikisha tunakuwa na jamii bora ambayo ina ushirikiano na ukuaji wa pamoja.

Kwa kuiishi kanuni hii tunakubali ya kwamba sisi wote ni kitu kimoja, na tatizo linapompata mmoja wetu ni tatizo letu. Kama kuna mtu hafanyiwi sawa, basi hilo litatuathiri sisi wote. Ni lazima tuwajali wengine kama ambavyo tunajijali sisi wenyewe.

Kanuni ya dhahabu ndiyo kanuni ya mafanikio makubwa kwenye maisha.

Kanuni hii ya dhahabu haiishii tu kwenye maadili na kuwa na jamii bora, bali tunaweza kuitumia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Kanuni hii ya dhahabu ni nzuri kwenye kujenga jamii bora na zenye ushirikiano, ila ni nzuri zaidi kwenye kujenga mafanikio makubwa na yanayodumu.

Kanuni ya dhahabu inasema kwamba watendee wengine kile ambacho ungependa wakutendee wewe, au usiwatendee wengine kile ambacho usingependa wao wakutendee. Hivyo hapa kuna kiungo kimoja muhimu sana ambacho ni kupenda kitu fulani. Wote tuna vitu ambavyo tunapenda kufanya, na pia tunapenda kufanyiwa. Sasa hivi ndiyo vitu ambavyo kama tukiweza kuvitumia vizuri, tunaweza kujijengea mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Hatua ya kwanza kabisa ya mafanikio kwa kutumia kanuni ya dhahabu ni kuwafanyia wengine kile ambacho unapenda kufanyiwa wewe. Na kuepuka kuwafanyia wengine kile ambacho hupendi kufanyiwa. Hivyo itumie kanuni hii kuvaa viatu vya wengine, jiweke kwenye nafasi za wengine na ona kama unatoa kile ambacho wewe ungependa kupata kutoka kwa wengine.

Tuangalie mifano michache;

Matumizi ya kanuni ya dhahabu kwenye ajira.

Kama umeajiriwa, unaweza kutumia kanuni ya dhahabu kuhakikisha unatoa mchango bora kabisa kwenye kazi hiyo. Hapa jiweke kwenye nafasi ya mwajiri wako na yule anayetegemea huduma zako.

Kwenye nafasi ya mwajiri wako jiulize kwa kazi unayofanya, je kama wewe ndiyo ungekuwa mwajiri na kuna mfanyakazi kama wewe, ungemchukuliaje? Je ungemwona kama ni mfanyakazi mwenye mchango kwenye kazi yako au mzigo? Je ungekuwa tayari kumpa nafasi kubwa zaidi na kumwongezea kipato kutokana na mchango wake au ungekuwa tayari kumpunguza kazi pale nafasi inapotokea? Majibu ya maswali yako yote tayari unayo, na unaweza kuyatumia kuhakikisha unakuwa bora zaidi.

Kwenye nafasi ya anayepokea huduma, jiulize kama wewe ndiye uliyekuwa unapokea kile unachotoa, je ungejisikiaje? Kwa mfano kama wewe ni daktari, na unatoa huduma kwa mgonjwa, jiulize je kama mimi ndiyo ningekuwa mgonjwa, na nikaenda kwa daktari akanipa huduma kama hii, je nitakuwa tayari kurudi tena kwake? Je nitakuwa tayari kuwaambia wengine nao waende kwa daktari huyu? Jiulize kwa kila unachofanya, iwe ni msanii, mwalimu, mwandishi. Chochote unachofanya, jiweke kwenye nafasi ya yule anayepokea, na ona kama ni kitu bora amepokea. Boresha zaidi ili kuweza kutoa huduma bora.

Matumizi ya kanuni ya dhahabu kwenye mafanikio ya biashara.

Unaweza kutumia kanuni hii ya dhahabu kwenye mafanikio ya biashara yako. Na hapa unajiweka kwenye nafasi za wengine, unavaa viatu vyao.

Kwa kila mtu unayehusiana naye kupitia biashara yako, jiulize kama wewe ndiye ungekuwa unapata wanachopata wao kutoka kwako kama ungeridhika na kuendelea kuwepo kwenye biashara hiyo.

Kama ni wateja jiulize kama kweli wanaridhika kama ambavyo wewe ungependa kuridhika unaponunua bidhaa au huduma unayotoa. Kama ni washirika wa kibiashara jiulize kama wanapata ushirikiano bora kutoka kwako.

Matumizi ya kanuni ya dhahabu kwenye mahusiano yako.

Kanuni hii ya dhahabu inatumika kwenye kila eneo la maisha yako. Unaweza kuitumia kwenye mahusiano yako ya kimaisha, na kukuwezesha kuwa na mahusiano bora kabisa na wengine.

Chochote unachowafanyia wengine, jiulize je kama wao ndiyo wangekuwa wamekufanyia wewe, ungejisikiaje, je ungeendelea kuwa na mahusiano mazuri na watu hao. Kwa kujiuliza swali hili kila mara utaweza kujirekebisha pale unapokosea na kuboresha zaidi yale mazuri unayofanya kwa ajili ya wengine.

Tuitumie kanuni ya dhahabu tunayofundishwa kila siku, kujijengea mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Mafanikio ya aina hii yanadumu kwa sababu yamejengwa kwenye msingi imara unaowajali wengine pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK