USHAURI; Jinsi Ya Kuondokana Na Uteja (Ulevi) Wa Michezo, Kamari Na Mitandao Ya Kijamii.

Rafiki, karibu kwenye makala yetu ya leo ya USHAURI WA CHANGAMOTO mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Kama ambavyo wote tunajua, changamoto ni sehemu ya maisha yetu, hivyo maisha bora siyo yale ambayo hayana changamoto, bali yale ambayo tunaweza kuzitatua changamoto zetu. Kwa sababu unapotatua changamoto, unajifunza zaidi na hivyo kuweza kuwa bora zaidi.

 

Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya uteja au ulevi wa michezo, kamari na hata mitandao ya kijamii. Vitu hivi vimekuwa changamoto kubwa kwa wengi na kuwazuia kuweza kufanikiwa. Kuna watu ambao hawawezi kabisa kukaa muda bila ya kucheza michezo ya aina fulani. Wengine hawawezi kabisa kukaa muda mrefu bila ya kuingia kwenye mitandao ya kijamii.

Ulevi mbaya sana ambao sasa unashika kasi ni huu wa kamari. Kuna hii kamari ambayo imehalalishwa sasa inaitwa betting, ambapo mtu anatabiri matokeo ya mpira na akipatia anapewa fedha. Wengi wamekuwa wakishiriki michezo hii na kupoteza fedha, lakini hawaachi kwa sababu unakuta wamekosea kidogo tu. Pia wanapata taarifa za wengine ambao wameweka fedha kidogo na kupata matokeo makubwa, tamaa yao inakuwa kubwa na kujikuta hawawezi kuacha. 

Kwa njia hii wanakuwa wateja na kushindwa kujizuia kucheza kamari.
Kabla hatujaangalia unawezaje kuondokana na ulevi wowote ambao unao sasa, hebu tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;

Wazazi wangu wanajitahidi sana kunipa mtaji lakini tatizo napenda sana kucheza pool table nimejitahidi kuacha lakini inashindikana na sina kilevi kingine kila siku naliwa elfu 20, 10 nakuendelea, na zaidi kuacha imeshindikana. Ezron Charles Kaje

Kama tunavyoona kwa rafiki yetu Ezron hapo juu, tayari ameshaingia kwenye ulevi kiasi kwamba hawezi tena kujizuia. Sasa hivi akili yake imeshakuwa kwenye utumwa wa mchezo huo, hana tena nguvu ya kujidhibiti.

Yafuatayo ni mambo muhimu kufanya ili kuondokana na ulevi wa michezo, kamari na hata mitandao ya kijamii.

1. Kubali kwamba una tatizo.
Hatua ya kwanza kabisa ya kutatua tatizo hili la ulevi ni kukubali kwamba una tatizo. Kwa sababu usipokubali una tatizo, huwezi kukubali msaada wowote. Kubali kwamba kuna vitu ambavyo umekuwa unafanya kwa muda mrefu ambavyo vimekuwa havina msaada wowote kwako. Kubali kwamba matumizi yako ya mitandao ya kijamii yamevuka kiasi.

Kwa upande wa Ezron, yeye ameshakubali ana tatizo mpaka akaomba ushauri, yupo kwenye nafasi nzuri ya kubadilika.

2. Badili marafiki.
Ukiangalia kwa makini, utagundua marafiki zako nao ni wateja wa kile ambacho na wewe umeshakuwa mteja. Hii ina maana kwamba unapokutana na marafiki zako, wote mnawaza kitu kimoja, ambacho ni ule ulevi wenu. Unahitaji kubadili marafiki ulionao, au kupunguza muda na marafiki ambao unao. Hii itakupa nafasi ya kuweza kukaa mbali na kile ambacho tayari umeshakuwa na ulevi nacho.

SOMA; Jinsi Ya Kuondokana Na Matumizi Mabaya Ya Mtandao Wa Intaneti Na Kutumia Vizuri Muda Wako Kujiongezea Kipato.

3. Tafuta kitu kingine ambacho kitakuweka ‘bize’.
Unapotaka kuacha ulevi wowote ulionao sasa, ni vyema ukapata kitu ambacho kitakuweka bize. Kama utaacha halafu ukawa huna kitu kingine cha kufanya, itakuwa rahisi kwako kurudi kwenye tabia uliyoacha. Unapopata kitu kingine cha kufanya, akili na mawazo yako yote yanakuwa kwenye kitu hicho kipya na hivyo kuwa rahisi kusahau ule ulevi wako.

Tafuta kitu ambacho unapenda kufanya, ambacho kitakuondoa kwenye ulevi ulionao sasa. Inawezekana ikawa kujifunza, au kazi fulani unayoipenda sana. Kila unapopata mawazo ya kwenda kufanya kile ambacho una ulevi nacho, fanya kile ulichopanga kufanya.

4. Epuka vishawishi vya kurudia ulevi unaotaka kuachana nao.
Mara nyingi unaweza kujipanga vizuri kuacha kitu fulani, lakini vishawishi vikawa vingi na kujikuta unarudia kile unachotaka kuacha. Moja ya vishawishi ni marafiki, ambao tumeshawazungumzia hapo juu.

Vishawishi vingine ni mazingira, kama upo kwenye mazingira ambayo yanahamasisha tabia fulani, inakuwa vigumu kwako kuiacha. Kama upo kwenye mtaa ambao kila mtu anacheza mchezo fulani unaotaka kuacha, itakuwa vigumu kwako. Kama simu yako ina mitandao ya kijamii ni vigumu kwako kuondokana na ulevi huu.
Badili mazingira yako ili yakuweke mbali na vilevi vyovyote unavyotaka kuachana navyo.

5. Pata msaada wa kuweza kuondokana na ulevi wowote ulionao.
Kama njia zote hapo juu hazitakusaidia, basi ipo njia ya uhakika ya kukuwezesha kuachana na ulevi wowote unaokusumbua. Njia hii ni kupata msaada wa wengine. Kupata msaada kupo kwa aina mbili.

Aina ya kwanza ni kujiunga na vikundi vya watu ambao wanataka kuachana na ulevi ambao na wewe unataka kuachana nao. Kwa kuwa kwenye vikundi hivi mara kwa mara mnakutana na kujadili changamoto mbalimbali na njia bora ya kufikia malengo yenu.
Aina ya pili ni kuwa na mshauri ambaye atakuwa anakusimamia katika hilo unalofanya. Mtu huyu atakufuatilia kwa karibu kuhakikisha kweli umeachana na tabia hiyo ambayo siyo nzuri kwako.
Maisha bora na yenye mafanikio ni yale maisha ambayo yana uhuru wa mwili na akili. 

Unapokuwa na ulevi wa kitu chochote, tayari unakuwa umepoteza uhuru wako, maisha yako hayawezi kuwa bora na huwezi kuwa na mafanikio. Kama kuna ulevi wowote ambao unakusumbua kwa sasa, hakikisha unaondokana nao. Utajuaje kitu ni ulevi kwako? Kama unashindwa kujizuia kufanya, basi umeshakuwa mlevi.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya juma tatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.
Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s