Linapokuja swala la fedha, kila mtu anataka kuwa na fedha za kumtosha kuweza kuendesha maisha yake bila ya kuwa na wasiwasi wowote. Kila mtu anataka kuwa na uhuru wa kifedha ambapo ana uhakika wa kupata huduma zote muhimu kwake, hata kama hafanyi kazi moja kwa moja. Kwa kifupi kila mmoja wetu anapenda utajiri.
Lakini kama tunavyojua, kupenda utajiri na kuupata utajiri ni vitu viwili tofauti kabisa. Wengi wanaupenda utajiri, ila ni wachache sana ambao wanaupata utajiri huo kweli. Sababu inayopelekea hali hii ni wengi kutokujua njia sahihi zakupata utajiri.
Kosa moja ambalo linapelekea watu wengi kuwa masikini ni kufikiri ya kwamba kipato chao ndiyo kinawaletea utajiri. Wanakazana kuongeza kipato wakifikiri ya kwamba wakifikia kiasi fulani cha kipato basi watakuwa matajiri.
Na hii ni kwa wote, walioajiriwa, waliojiajiri na wanaofanya biashara. Wanakazana kuongeza kipato, lakini wanasahau siri moja kuu ya utajiri ambayo haianzii na kipato.
Iko hivi rafiki, kipato hakiwezi kukuletea utajiri, kwa sababu kadiri kipao kinaongezeka, na matumizi nayo yanaongezeka. Nafikiri wewe mwenyewe utakuwa umelishuhudia hili mara nyingi, ulipokuwa na kipato kidogo, matumizi yako yalikuwa madogo, kipato kilipoongezeka matumizi nayo yakaongezeka. Hata kama utayadhibiti kiasi gani, bado kuna ambayo yataongezeka.
Pia kipato hakiwezi kukufanya tajiri kwa sababu kuendelea kutegemea kipato muda wote ili kupata fedha ya kuendesha maisha, ni umasikini mkubwa. Hii ni kwa sababu kama kipato hicho kitakauka leo, haijalishi kilikuwa kikubwa kiasi gani, maisha yako yataathirika.
Kama kipato hakikuletei utajiri, ni kitu gani basi kinaleta utajiri?
Najua utakuwa umeshaanza kujua, hasa kama umekuwa mfuatiliaji wa elimu ya fedha kwa muda.
Kinacholeta utajiri ni uwekezaji. Pale unapoifanya fedha yako ikufanyie kazi wewe, na kuanza kuvuna faida, hapo ndipo unapoanza kuhesabu utajiri wako. Pale ambapo unaingiza kipato bila ya wewe mwenyewe kufanya kazi moja kwa moja, hapo ndipo unakuwa na utajiri.
Ufanye nini?
Bila ya kuangalia kipato ulichonacho sasa, hakikisha unawekeza. Wekeza ili baadaye uwekezaji wako uweze kukuzalishia kipato bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja. Anza kuwekeza mapema, wekeza hata kidogo kidogo. Kwenye uwekezaji muda ni muhimu kuliko kiasi. Anayewekeza kidogo kidogo kwa miaka mingi, anapata faida kubwa kuliko anayewekeza kiasi kikubwa kwa mara moja.
Wekeza rafiki, maeneo gani uwekeze tutaendelea kujifunza kupitia KISIMA CHA MAARIFA.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK