UCHAMBUZI WA KITABU; What Winners Do To Win (Mbinu Hamsini (50) Wanazotumia Washindi Kushinda).Kuna jambo moja muhimu sana unapaswa kulielewa kwenye maisha yako, jambo hili ni kwamba hakuna kitu chochote kinachotokea kwa bahati, iwe ni mbaya au nzuri. Kila kitu kinachotokea kwenye maisha kimesababishwa. Kama maisha yako ni mazuri kuna mambo umefanya ambayo yamepelekea uwe na maisha mazuri. Kadhalika kama maisha yako ni mabaya, basi hayo ni matokeo ya mambo mabaya uliyofanya, au mazuri ambayo hukufanya.

 

Watu waliofanikiwa, na watu wanaoshinda kila siku kwenye maisha yao, kuna mambo wanayofanya, ambayo yanawaletea matokeo ya ushindi. Mambo haya siyo siri, wala hayahitaji elimu au uwezo mkubwa kuweza kuyafanya wewe pia.
Kwa bahati nzuri sana kwetu, mwandishi Nicki Joy, ametuchambulia yale mambo muhimu ambayo washindi wanayafanya na hivyo kuwa na maisha ya ushindi kila siku. Kazi ni kwako kujifunza mambo haya na kuyafanyia kazi kila siku kwenye maisha yako.
Mwandishi amezungumzia mengi mno, mimi hapa nimekuchambulia 50 kati ya hayo mengi, jifunze, fanyia kazi na maisha yako yatakuwa bora sana.

1. Ushindi unamaanisha vitu tofauti kwa watu tofauti. Kile ambacho wengine wanaona ni ushindi kwao, kinaweza kisiwe ushindi kwako. Hivyo hatua ya kwanza jua maana ya ushindi kwako.

2. Kila mtu anapenda kushinda, kila mtu anapenda zile hisia za ushindi. Hata wale wanaoshindwa, kwa ndani wanajua namna gani wanautaka ushindi. Usiubanie moyo wako, tafuta ushindi.

3. Ili kushinda, kitu muhimu ni kuja sheria za mchezo. Kila mchezo una sheria zake, na kwenye huu mchezo ambao wote tunaoucheza, ambao unaitwa MAISHA, una sheria zake, zijue na kuziheshimu na mambo yako yataenda vizuri. Zipuuze na hutaweza kushinda kamwe.

4. Ukishazijua sheria za mchezo, hatua inayofuata ni kutengeneza mkakati wa ushindi. Ushindi hauji kwa bahati, ushindi unakuja kwa mikakati bora inayofanyiwa kazi. Mkakati wako wa ushindi unahusisha mtazamo wako, juhudi unazoweka na namna ya kutumia sheria za mchezo kwenda vizuri.

5. Kutaka kuwa bora ni moja ya mitazamo unayopaswa kuwa nayo ili kufanikiwa.

6. Lazima uingie uwanjani ili kushinda. Ukishajua ushindi kwako ni nini, ukazijua sheria za mchezo, kisha ukatengeneza mbinu zako za ushindi, bado ushindi huwezi kuupata kama hutaingia uwanjani na kucheza. Kuwa mtu wa kuchukua hatua kwa lolote unalotaka kupata.

SOMA; Hizi Ndio Mbinu Anazutumia Mwajiri Wako Kuhakikisha Unaendelea Kuwa Mtumwa Wake.

7. Washindi wanajua ya kwamba ukomavu ni muhimu kuliko umri. Ukomavu hauhusiki na umri, bali ni uwezo wa mtu kukubali majukumu yake, kuchukua hatua na kukubali makosa yake.

8. Wakati wa furaha kwenye maisha yetu, ni ule wakati ambao tunakuwa na mawazo ya hamasa, mawazo bora na yanayoleta matunda mazuri. Mara zote hakikisha unakuwa na mawazo haya.

9. Kipimo cha ukomavu kinahusisha vigezo hivi tisa muhimu;
Moja; uwezo wa kufanya kazi bila kusimamiwa.
Mbili; uwezo wa kumaliza kazi ambayo mtu ameianza, bila ya kuahirisha.
Tatu; uwezo wa kutembea na hela mfukoni bila ya kuitumia.
Nne; uwezo wa kutokulipiza kisasi hata kama umefanyiwa mabaya.
Tano; uwezo wa kutegemea mambo bora zaidi baadaye.
Sita; uwezo wa kuwa na busara, kujizuia usiseme kila kitu hata kama unasukumwa kusema.
Saba; uwezo wa kufikiria kuhusu madhara ya hatua unazochukua au unazoshindwa kuchukua.
Nane; uwezo wa kukubali kupokea lawama za wengine.
Tisa; uwezo wa kujifunza kutokana na uzoefu.

SOMA; Hizi Ndizo Aina Tatu (3) Za Kushindwa Katika Maisha Na Kazi.

10. Ushindi unaanza na hamu ya mafanikio. Unapowaona na kujifunza kutoka kwa wengine ambao wamefanikiwa, na wewe unapata hamu na shauku ya kufanikiwa pia. Unaona kama wao wameweza, basi hata wewe unaweza.

11. Hamasa ya kweli inatoka ndani yako mwenyewe. Hamasa ya nje inaweza kukusaidia, ila haidumu. Hamasa ya ndani ndiyo hamasa ya kweli, inakupa msukumo mkubwa na inadumu kwa muda mrefu.

12. Kwenye huu mchezo unaoitwa MAISHA, kuna wakati utaonewa, kuna wakati utanyimwa kile ambacho unastahili, kuna wakati utafanya kila kitu, halafu wengine wananufaika kuliko wewe. Ni muhimu uweze kuvuka nyakati kama hizi bila ya kukata tamaa.

13. Hamasa ya mafanikio ni kitu unachopaswa kuchoche akila siku, hufanyi mara moja halafu ikawa imetoka, kila siku unahitaji kuendelea kujihamasisha.

14. Washindi wanajua ili kuona mafanikio, lazima waamini kwanza kwamba watafanikiwa. Kwa kifupi unaona na kupata kile ambacho unaamini. Kama hufanikiwi, hebu anza kuchunguza imani yako, ni kipi unaamini?

SOMA; Tumia Kanuni Hizi Tatu(3) Za Muhimu Sana Ili Uweze Kumfanya Mteja Asikukimbie Kwenye Biashara Yako

15. Imani yako ndiyo ufunguo wa hazina yako. Huu ndiyo ufunguo unaokupeleka kwenye mafanikio au kushindwa. Imani yako ndiyo inatawala maisha yako. Kama unaamini utashinda, basi utavuka vikwazo vyote na kushinda. Kama unaamini utashindwa, hata njia iwe rahisi kiasi gani, utaona vikwazo.

16. Washindi wanajua kwamba chochote wanachoamini sasa, wametengeneza wao wenyewe. Washindi wanajua na wapo tayari kuvunja imani hasi wanazojengewa na wengine. Wanapoambiwa hawawezi kufanya kitu fulani, ndiyo wanapata hamasa ya kukifanya.

17. Washindi wanapigana kila siku kuhakikisha wanaondoa imani zisizoendana na ushindi kwenye maisha yao. Wanafanya hivyo kwa kuepuka kutumia kauli zinazotumwa na wengi, ambazo ni hasi. Kauli kama hatuwezi, haiwezekani huwezi kuzisikia kwa washindi.

18. Washindi wanachukua hatari ambazo ni hatari, nafasi ambazo wengine wanahofia kabisa kuzichukua. Washindi wanajua ya kwamba hatari namba moja kwenye dunia hii ni kutokuchukua hatari kabisa.

19. Kuna watu wanajua muda mzuri na muda mbaya, kuna watu wanajua wakati sahihi na ambao siyo sahihi kufanya kitu. Lakini washindi wanajua kitu hiki kimoja, muda wowote kwao ni muda mzuri na sahihi kuchukua hatua. Hawasubiri muda.

20. Washindi wanajua kitu pekee ambacho kina thamani kubwa ni muda. Wanajua huwezi kudhibiti muda, bali unaweza kudhibiti matumizi yako kwenye muda, na wanafanya hivyo, kwa kuwa na vipaumbele sahihi kwao.

21. Washindi wanajua muda hautafutwi, bali muda umetengwa. Wakati wengine wanasema wakipata muda watafanya, washindi wanapanga muda na kufanya. Kama unasubiri upate muda, utasubiri milele.

22. Washindi wana orodha mbili, orodha ya kwanza ni ya vitu ambavyo watavifanya (TO DO LIST), na orodha ya pili ni ya vitu ambavyo hawatavifanya (NOT TO DO LIST). Orodha ya pili ni muhimu sana kwa washindi kwa sababu inawaepushia kupoteza muda.

23. Washindi wote wana misingi imara wanayasimamia, ili kuepuka kupelekwa na matukio ya kila siku. washindi wanajua hakuna kinachopoteza muda kama kuhangaika na matukio ya kila siku.

24. Washindi wanajua matumizi mazuri ya muda hayaanzi na saa, bali yanaanza na kupanga, kusimamia na kuweka vipaumbele vizuri. Usihangaike kuangalia saa, angalia ni nini unafanya na kina matokeo gani kwako.

25. Washindi wanajua wao wenyewe hawawezi kitu, wanajua wanahitaji msaada na ushirikiano kutoka kwa wengine. Hivyo wanajenga mahusiano bora na wengine, na kuwasaidia pia.

26. Washindi wanajua, kitu kigumu katika kufanya kazi na wengine, ni kufanya kazi na wengine. Kwa kifupi binadamu ni kiumbe mgumu sana kufanya naye kazi, hivyo unahitaji kuwa na uelewa sahihi ili kuweza kwenda vizuri na wengine.

27. Washindi wanajua kuwajaza wengine hofu hakuwasaidii kufikia malengo yao. Wanajua wale walio chini yao, wanahitaji kupewa hamasa ili wafanye kazi zao vizuri, kuwapa vitisho kunawahamasisha kwa muda mfupi, baada ya hapo wanazoea na haileti matokeo mazuri.

28. Washindi wanajua kuwahamasisha watu kufanya kazi zao kwa kuwapa zawadi pia haileti matokeo ya kudumu. Inaleta matokeo ya muda mfupi, baada ya hapo watu wanazoea na haiongezi uzalishaji au ufanisi.

29. Washindi wanajua kwamba kitu pekee kinachowahamasisha watu kufanya kazi kwa juhudi, kwa ufanisi na uzalishaji wa hali ya juu ni mazingira mazuri ya kazi. Na mazingira haya ni ya kisaikolojia kama kazi kuwa na maana kwa watu hao, ushirikiano, kutambulika na kuheshimika kwa wanachofanya.

30. Washindi wana haja kubwa ya kuchukua hatua. Pale jambo muhimu linapokuja mbele yao, huwa hawasiti wala kusubiri kwa muda mrefu. Badala yake wanachukua hatua mara moja, hali hii inawawezesha kuzitumia vizuri fursa zinazowajia.

31. Unaweza kuwa na akili sana, ukawa na ujuzi wa kutosha, lakini kama hutakuwa mtu wa kuchukua hatua haraka, utaishia kuwa wa kawaida.

32. Katika dunia ya sasa, unahitaji kuwa kasi kuliko washindani wako. Watu wa sasa hawana tena utulivu, wanataka kitu na wanakitaka sasa. Kama wewe huwezi kuwapa kwa kasi wanayotaka, watatafuta pengine wanapoweza kupata kwa kasi hiyo.

33. Hakuna mtu aliyeweza kufanya makubwa kwa kusubiri mpaka awe tayari. Washindi wote wanaanza hata kabla hawajawa tayari, na wanajifunza huku wakiendelea kufanya.

34. Washindi wameweza kuwajenga wateja wao hali ya kuchukua hatua haraka. Mteja anapowaambia akiwa tayari atawatafuta, washindi hawamwambii sawa, ukiwa tayari tutafute. Badala yake wanamuuliza utakuwa tayari lini, kesho au juma tatu ijayo? Kwa hali hii wanawaambukiza wateja haja ya kuchukua hatua haraka na hivyo kuweza kukamilisha kazi zao.

35. Jipange. Kila siku kabla hujaondoka eneo lako la kazi, panga vitu vyako vizuri, safisha eneo ulilofanyia kazi. Tafiti zinaonesha kwamba, kuanza kazi kwenye eneo safi na lililopangiliwa vizuri, kunaleta hamasa ya kuweza kufanya kazi vizuri.

36. Washindi kwa kweli siyo watu wavivu, uvivu ni sumu kubwa ya mafanikio na ushindi. Kama wewe ni mvivu, jua kabisa kwamba unapishana na ushindi.

37. Kama umekuwa na uvivu basi angalia chanzo chake ni nini. Kila uvivu una chanzo ndani yako. Vyanzo vya uvivu ni aina ya chakula mtu anapata, kukosa mazoezi, kukosa muda wa kutosha wa kulala na kupumzika, dawa ambazo mtu anaweza kuwa anatumia, aina ya marafiki wanaokuzunguka. Angalia chanzo kwako ni nini na kifanyie.

38. Washindi wanajua kuwa na mtizamo chanya ni hatua muhimu, lakini siyo kila kitu. Wanajua mtazamo chanya pekee hautoshi, bali mtizamo chanya lazima uende pamoja na matendo chanya.

39. Kuna namna ambavyo washindi wanaiweka miili yao, ambao unawafanya wengine kuwaamini. Washindi husimama wima, mabega juu, uso wanaangalia mbele, miguu imeachana, mikono kwenye mapaja. Kwa mkao wa aina hii wanaonekana ni watu wanaojua kile wanakifanya na hivyo kuaminika na wengi.

40. Kuchukua hatua ndiyo kitu pekee kinachowatofautisha washindi na wengine. Na cha kushangaza sasa siyo kwamba washindi wanachukua hatua kubwa sana, bali wanachukua hatua ndogo ndogo sana, zile ambazo wengine wanazipuuza. Baadaye hatua hizi ndogo zinawanufaisha sana.

41. Washindi wanajua tofauti ya kujiamini na kujivuna. Wanajua kujiamini ni muhimu ili kushinda, ila hawatumii ushindi wao kujivuna kwa wengine. Wanajua kushinda kwao siyo kitu cha kuwafanya wadharau wengine.

42. Washindi pia wanajua japo wanaamini wanaweza, siyo kwamba wanaweza kufanya kila kitu bora kuliko wanavyofanya wengine. Wanaoshindwa huamini wanaweza kufanya kwa ubora zaidi ya wengine, hivyo hawawaheshimu wengine na hivyo kukosa ushirikiano na wengine.

43. Washindi wanajua utu wao na wa wengine siyo sehemu ya ushindi. Hata washinde kiasi gani, bado hawajioni wao ndiyo wao na wengine ni mafisi. Wanawaheshimu wengine, hata kama hawajashinda kama wao.

44. Washindi wanajua umuhimu wa mambo ya kawaida kwenye ushindi wao. Hata siku moja hawachukulii mambo kirahisi, au kudharau mambo kwa sababu ni ya kawaida. Wanaheshimu na kufanya kila wanachopaswa kufanya, hata kama ni kidogo kiasi gani.

45. Watu wengi wamekuwa wakiangalia yale makubwa na kusahau madogo ambayo yanakuja kuwa makubwa sana baadaye. Washindi hawaruhusu hili litokee kwao, wanafanya kila jambo kwa wakati wake.

46. Washindi wanaishi kwa falsafa kwamba kila mtu anastahili kuheshimiwa mpaka pale watakapoamua wenyewe kutokuheshimiwa. Hivyo huwachukulia watu wote kwa usawa, na hivyo kuweza kutoa huduma bora sana kwa watu wote.

47. Baadhi ya mambo madogo madogo muhimu sana kuzingatia ili kujenga mahusiano bora na wengine;
Moja; simama wakati wa kutambulishwa na kujitambulisha kwa wengine.
Mbili; sema TAFADHALI, sema ASANTE, sema Karibu.
Tatu; waangalie wengine machoni wanapoongea na unapoongea.
Nne; angalia njia ya kufanya tendo la wema.
Tano; wafungulie wengine mlango, wape wengine nafasi.

48. Washindi wanajua kuna tiketi moja muhimu ya kuwaingiza kwenye mioyo ya wengine. Tiketi hiyo ni uso wenye tabasamu. Unapotabasamu watu wanakuamini na kuvutiwa kuwa karibu na wewe. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wale wanaotabasamu wana mambo mazuri yanayoendelea kwenye maisha yao. Tabasamu mara zote, hata kama huna mambo mazuri 
yanayoendelea kwenye maisha yako.

49. Washindi wanafanya mambo ya kawaida kwa namna ambayo siyo kawaida. Siyo kwamba washindi wanafanya mambo ya tofauti sana na wengine, wanafanya yale yale wanayofanya wengine, ila wanayafanya kwa utofauti mkubwa. Wanaweza kuuza kile ambacho kila mtu anakiuza, lakini wao wakakiuza kwa ubora zaidi.

50. Washindi wana kopi mbinu za mafanikio kutoka kwa wale ambao wamefanikiwa. Washindi wanajua hawahitaji kuja na mbinu zao mpya za mafanikio, badala yake wanaangalia wale waliofanikiwa wanafanya nini, na wao wanafanya hivyo. Hawaigi kile wanachofanya, bali wanaiga tabia na mitazamo yao, ambayo inawapelekea kuwa na mafanikio makubwa.

Je wewe unataka kuwa mshindi, je unataka mafanikio makubwa kwenye maisha yako? Fanya mambo haya 50 tuliyojifunza kupitia kitabu hiki cha WHAT WINNERS DO TO WIN.
Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

One thought on “UCHAMBUZI WA KITABU; What Winners Do To Win (Mbinu Hamsini (50) Wanazotumia Washindi Kushinda).

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: