Katika safari yako ya mafanikio, wapo watu wengi ambao watakupa maoni yao. Watakupa kila sababu kwa nini maoni yao ni sahihi na unapaswa kuyafuata. Watakuonesha na mifano, huku wakikupa ushahidi wa kweli kwamba wanachosema wao ndiyo sahihi.

Lakini unajua nini, hata waseme mambo mazuri kiasi gani, bado yale ni maoni yao. Na siku zote maoni siyo ukweli, bali ni maoni. Na kila mtu anaruhusiwa kuwa na maoni yake.

Ninachotaka kukuambia ni hiki rafiki, unapochagua safari ya mafanikio, na kujua kipi hasa unataka, weka juhudi kukipata. Kama kuna mtu yeyote anakuja kukuambia huwezi au haiwezekani, okoa muda wako kwa kutokumsikiliza. Kwa sababu hakujui vizuri na hakuna anayejua kesho italeta nafasi na fursa gani.

Wapo watu wengi walioishangaza dunia kwa makubwa waliyoweza kufanya licha ya watu kuwaambia hawawezi. Watu waliwapa mpaka ushahidi kwamba haiwezekani, lakini msukumo wa ndani yao uliwawezesha kupata kile walichotaka.

Je wewe ni kipi ambacho unakitaka kweli kutoka ndani ya moyo wako? Ni msukumo upi mkubwa ulipo ndani yako? Ni jambo gani unataka kukamilisha kwenye maisha yako?

Lolote unalotaka, usikate tamaa kwa maneno ya watu, au kwa kinachoendelea sasa. Badala yake weka juhudi, fanya kazi, jifunze, kuwa bora kila siku, na hakika utafanikiwa. Lolote linaweza kutokea kwa yeyote, na linaweza kutokea kwako pia. Usikate tamaa wala usiichie njiani, mafanikio yako yapo mikononi mwako.

Kwa mafanikio yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK