Kuna swali moja muhimu sana la kujiliza kama unataka kuongeza kipato chako. Ni swali muhimu na sahihi ambalo litakupa jibu sahihi la hatua unazoweza kuchukua wewe ili kupata ile fedha unayotaka kupata.
Kwa mfano, kama unataka kujenga nyumba, au kununua gari, au kununua chochote ambacho ni muhimu kwako, utaanza kujiuliza nitapata wapi fedha? Si ndiyo, hili ni swali la msingi kabisa. Wengine wataenda moja kwa moja kwamba haiwezekani kwa wao kupata fedha hizo, wengine watafikiria njia mbalimbali za kupata fedha hizo.
Njia hiyo inaweza kusaidia, lakini ipo njia nyingine ambayo ina uhakika zaidi wa kukuwezesha kupata kile unachotaka.
Njia hiyo inaanza na kujiuliza swali hili muhimu, nani mwenye fedha zangu? Unajua ya kwamba fedha yoyote unayotaka sasa, lazima itatoka kwa mtu mwingine. Unajua huwezi kujitengenezea fedha zako wewe mwenyewe. Badala yake lazima utoe bidhaa au huduma kwa mtu, na yeye akulipe kulingana na thamani uliyompa. Sasa huyu ndiye mtu ambaye ana fedha zako.
Unapotaka kupata fedha ya kununua kitu fulani, jiulize ni nani ana fedha zako hizo kwa sasa. Na hapa anza kuangalia ni namna gani utamshawishi mtu huyo akupe fedha yako hiyo ambao anayo kwa sasa. Kwa njia hii utajiuliza maswali bora zaidi, mfano mtu huyu anataka bidhaa au huduma gani ili aweze kunipa fedha yangu hiyo.
Kwa swali hili utahakikisha unatoa huduma bora kabisa kwa yule ambaye unajua ana fedha yako, na yeye kwa kupata thamani hiyo unayotoa, atakuwa tayari kukupa fedha yako ambayo alikuwa nayo yeye.
Fedha yoyote unayotaka sasa, ipo kwenye mifuko ya wengine. Hawajakupa bado kwa sababu hakuna thamani ambayo umeshawapatia. Hebu anza kuwapa thamani sasa na uone watakavyokupa ile fedha unayotaka.
Hii unaweza kuitumia popote, iwe ni kwenye ajira au hata biashara. Unapotaka fedha zaidi, angalia ni thamani gani unayoweza kutoa kwa wengine, na wao wawe tayari kukulipa fedha. Usije ukatumia dhana hii kinyume, kwa kuangalia nani mwenye fedha halafu ukamwibia, hiyo haifanyi kazi, itakupoteza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK