Wote tunajua ya kwamba, kwenye maisha tunapata kile ambacho tunakitaka. Kile ambacho tunakifikiria muda mrefu kwenye akili zetu, na kukitafuta kwa bidii ndiyo tunachopata kwenye maisha yetu. Tunapata kile ambacho kimetawala akili zetu muda mwingi kwa sababu akili zetu zina uwezo mkubwa wa kuumba na kutusogeza karibu na mazingira yenye kila tunachotaka.

Lakini pia tunapata kile ambacho tunavumilia. Kile ambacho tunakubaliana na cho, kile ambacho hatukipingi ndiyo tunachoendelea kupata kwenye maisha yetu. Kama kipato ulichonacho sasa unakubaliana nacho, utaendelea kupata kiasi hicho kwenye maisha yako. Kama watu waliokuzunguka unakubaliana nao, utaendelea kuzungukwa na watu wa aina hiyo kwenye maisha yako.

Chochote unachovumilia utaendelea kukipata, chochote unachokubaliana nacho kitaendelea kuwepo kwenye maisha yako.

Kwa mfano kama mtu anakutukana na wewe unakubaliana naye, au unavumilia, huthubutu kumwambia ukweli kwamba hupendi maneno kama anayoyatoa, ataendelea kutoa maneno hayo. Na mbaya zaidi wale wanaokuzunguka wakiona unakubaliana na maneno ya matusi unayopewa na wengine, na wao wanajifunza kwamba unakubaliana na maneno hayo, nao wataanza kukupa maneno hayo.

Kama kipato unachoingiza sasa kupitia kazi yako au biashara yako unakubaliana nacho, utaendelea kupata kipato hicho siku zote. Utapokea kipato hicho na kuendelea kufanya kile unachofanya na kwa njia unazotumia kufanya sasa, hutaweka makubwa na hutaweza kupata matokeo tofauti. Hata akija mtu mpya, atajifunza kupitia kile unachopata sasa na yeye atakulipa kiasi hicho hicho kwa sababu unaweza kukivumilia.

Ukiangalia vizuri, sehemu kubwa ya hivi tunavyovivumilia ni vitu ambavyo hatuvitaki kwenye maisha yetu, lakini hatuna njia ya kuondokana navyo. Siyo vitu tunavyopenda na kufurahia, lakini tunajikuta kama tumenasa na hatujui tunachomokaje.

Ufanye nini ili uweze kupata unachotaka?

Kama kuna kitu ambacho hukipendi kwenye maisha yako, usikivumilie, usikipe nafasi kabisa. Kama ni matendo ya watu huyapendi, waambie wazi ya kwamba hupendezwi na matendo yao. Usiogope kama watakasirika au kukuchukuliaje, ukichukua hatua ya kuwaambia ukweli watakuheshimu.

Kama kipato chako cha sasa hakikutoshelezi, usikubaliane nacho, chukua hatua za kuongeza kipato chako. Usikae na kujidanganya kwamba siku moja mambo yatakuwa mazuri, mambo hayawi mazuri yenyewe, mambo yanafanywa kuwa mazuri. Ni lazima uchukue hatua wewe ya kuhakikisha unapata kipato bora zaidi ya ulichonacho sasa.

Yote haya yanatupeleka kwenye kuchukua hatua, na kauli kwamba maisha ni kile unachochagua, inabaki kuwa sahihi. Usichague kuvumilia yale ambayo huyataki, maisha ni yako na uchaguzi ni wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK