Hongera kwa siku nyingine nzuri sana ya leo rafiki yangu.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kile tunachofanya.
Ili kushika umiliki wa siku ya leo, ili kuitumia siku ya leo vizuri, ni muhimu ukaianza kwa kukiri hii ni siku bora kwako, hii ni siku ambayo unakwenda kuweka juhudi kubwa na utapata matokeo bora na makubwa. Unapokiri siku ya leo ni bora kwako, hakuna anayeweza kuiharibu kamwe. Miliki siku yako ya leo rafiki, kiri umiliki na ubora wa siku hii ya leo kwako.

img_20161112_091656

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu NJAA YA DUNIA,
Kama hujawahi kupata nafasi ya kusikia hili rafiki, basi sikia leo, dunia ina njaa kubwa sana.
Dunia ina njaa ya mawazo bora, mawazo ya kuifanya dunia kuwa sehemu salama kabisa ya kuishi na maisha yetu wote kuwa bora.
Ipo hadithi ambayo bado dunia haijasikia,
Lipo wazo ambalo dunia haijalipata bado na kulitumia kuwa bora zaidi.
Ipo bidhaa muhimu ambayo bado dunia haijapata.
Ipo huduma ambayo bado dunia haijapata.
Dunia ina njaa kubwa ya kazi zilizo bora.

Na uzuri ni kwamba, wewe ni mmoja wa wanaosababisha njaa hiinya dunia.
Kuna hadithi yako bado hatujaisikia,
Kuna uwezo wako mkubwa bado hatujauona.
Kuna huduma yako bado haijaingia kwenye maisha yako.

Hivyo rafiki yangu, acha kuidhulumu dunia, ipe kile ambacho umekuwa unafikiria kuipa muda mrefu lakini huanzi. Hebu tatua njaa hii ya dunia kwa kufanya kile ambacho unajua kweli unaweza kufanya, na kifanye kwa ubora wa hali ya juu.

Ishibishe dunia kwa kazi zilizo bora, hii ndiyo njaa kubwa ya dunia.

Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info