USHAURI; Njia Ya Uhakika Ya Kuondokana Na Madeni Sugu Na Kufikia Uhuru Wa Kifedha Kwenye Maisha Yako.

Pesa, fedha, hela, au vyovyote unavyoiita wewe, ni moja ya mahitaji yetu muhimu sana kwenye maisha. Ukiondoa pumzi ambayo tunaivuta ili kuendelea kuwa hai, kitu kinachofuatia kwa umuhimu ni fedha. Bila ya fedha hakuna maisha, au maisha yatakuwa mabovu mno. Na ndiyo maana kila siku tunapambana, tunaamka asubuhi na mapema kwenda kwenye shughuli zetu, ili tuweze kutengeneza kipato.

 

Changamoto kubwa sana inayokuja kwenye swala la fedha ni kukosekana kwa elimu sahihi ya fedha. Elimu ya fedha, yaani jinsi ya kuipata, jinsi ya kuitumia na hata jinsi ya kuizalisha zaidi, haipo kwenye mtaala wa mfumo wetu wa elimu, na wala haipo kwenye taratibu zetu za kawaida kwenye maisha.

Yaani mtu atakaa chuoni miaka mitatu, minne au mitano akisomea fani fulani, atafundishwa kila kitu kuhusu fani hiyo, lakini hatofundishwa jinsi gani anaweza kutumia kipato chake vizuri, njia za kuziongeza ili maisha yake yaweze kuwa bora. Ukosefu huu wa elimu sahihi ya fedha ndiyo unafanya watu wengi wanajikuta kwenye changamoto za kifedha zinazotokana na makosa wanayoyafanya kila siku.

Makosa mengi kwenye matumizi ya fedha huwa yanapelekea kwenye madeni, na tabia ya madeni ni kwamba huwa yanakua. Kwa sababu mtu hana elimu ya fedha, anafanya makosa na kujikuta yupo kwenye madeni. Na kwa kuwa bado hana elimu ya fedha, madeni aliyonayo yanazidi kukua kadiri siku zinavyokwenda. Hii ndiyo hali inayopelekea baadhi ya watu kujikuta wakiishi maisha kama ya utumwa. Wanafanya kazi, wanapata fedha, wanakwenda kulipa madeni, halafu wanaanza kukopa tena.

SOMA; Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Madeni Mabaya.

Katika makala yetu ya leo ya USHAURI WA CHANGAMOTO ZINAZOTUZUIA KUFANIKIWA, tunakwenda kushauriana njia bora kabisa ya kuondoka kwenye madeni na kujijengea uhuru wa kifedha. Lakini kabla hatujaingia kujadili hayo, hebu tusome ujumbe wa msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili.

Habari, Changamoto ninayokutana nayo kwenye maisha yangu ni madeni makubwa ambayo ukilinganisha na kipato changu sioni jinsi ya kumaliza tatizo hili. Ninadaiwa benki ambapo kila mwezi nakatwa sh laki mbili na elfu ishirini, Ninadaiwa kwenye chama chetu cha akiba na mikopo kazini yaani saccos, kwa kifupi kila mwisho wa mwezi ninajikuta nina uhakika wa kupata shilingi laki tano tu. Mbali na madeni hayo yanayokatwa kwenye mshahara moja kwa moja vile vile nina madeni mengine kutoka kwa watu binafsi na vikundi vinavyokopesha kwa riba. Madeni haya yamekua ni mengi kiasi kwamba imefikia hatua nahisi kupoteza imani kwamba ninaweza kuyalipa. 

Kiukweli sikua na matumizi mazuri ya pesa na nimekuja kuligundua hilo baada ya kujikuta nabanwa kila kona kurejesha pesa za watu na mimi binafsi sioni hata pa kuanzia kuitafuta hiyo pesa. Sina biashara yoyote ninayofanya kwa sasa kwa sababu hata mtaji umekua shida kupatikana kwa sababu hiyo laki tano ninayoipata kila mwezi najaribu kupambana na madeni. 

Naomba ushauri wako nifanye nini, kwa hali ninayoiona kama nitaendelea kua hivi basi kuna hatari ya kupata magonjwa yanayosababishwa na msongo wa mawazo. R. F. Masami.

SOMA; Sababu 5 Zinazokufanya Wewe Kuishia Kukopa Kila Siku.

Kama ulivyosoma maelezo ya rafiki na msomaji mwenzetu hapo, umeshapata picha ya changamoto yake, umeshaona amekwama wapi kwa sasa. Huenda na wewe ni mmoja wa watu ambao wapo kwenye hali kama za rafiki yetu Masami, karibu tujifunze namna ya kuondoka kwenye madeni na kujijengea uhuru wa kifedha.

Rafiki yangu Masami, na marafiki wengine wote mnaosoma hapa, kuwa kwenye madeni siyo kitu cha bahati mbaya, bali ni kitu ambacho mtu unatengeneza iwe unajua au hujui. Na kanuni ya kuingia kwenye madeni ni rahisi, pale matumizi yanapokuwa makubwa kuliko mapato, lazima utaingia kwenye madeni. Na kama utaendelea kukuza matumizi yako, utaendelea kukuza madeni yako. Ni rahisi kama hivyo, huhitaji shahada ya uchumi na fedha kuelewa hilo.

Kwa hiyo, kwa kuanza ni kwamba, upo kwenye madeni kwa sababu umeruhusu matumizi yako yawe makubwa kuliko mapato yako. Hivyo kwa kuwa unataka kutumia zaidi ya ulichonacho, ukajikuta umeingia kwenye mtego wa madeni, na hapo ndipo umenasa mpaka sasa.

Sasa kitu kingine cha kushangaza kuhusu madeni ni hichi, ukishakopa mara moja, unajikuta unarudi kukopa tena, na kama ulipokopa mwanzo hapafai kukopa tena, unaenda kukopa kwingine na kwingine. Baada ya muda unajikuta unadaiwa na watu wengi na kuanza kuona maisha ni machungu.

Hii ndiyo njia ya uhakika ya kuondoka kwenye madeni.

Kama nilivyokushauri hapo juu, nitakupa njia ya uhakika ya kuondoka kwenye madeni ambayo upo sasa. Na ukifanyia njia hii kazi, basi utarudisha udhibiti wa maisha yako na mambo yako yataanza kwenda vizuri kama zamani.

SOMA; Mambo Kumi Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Matumizi Yako Ya Fedha Ili kuweza Kufiki Uhuru Wa Kifedha.

Njia ni hii, kwa sasa piga mahesabu yako sawa sawa, angalia kipato chako ni kiasi gani, halafu toa yale madeni ya msingi ambayo unakatwa moja kwa moja kwenye kipato chako kama ni mshahara. Halafu kile kipato kinachobaki kigawe kwenye mafungu matatu ambayo nitayaelezea vizuri hapo chini. Mafungu hayo utayagawa kwenye asilimia za kipato kinachosalia.

Mafungu matatu ni kama ifuatavyo,

Fungu la kwanza ni asilimia 10 ya kile kipato kilichobaki baada ya kuondoa makato yote, hili ni fungu ambalo unajilipa wewe kwanza. Hii ndiyo hazina yako, ndiyo kitakachokutoa hapo ulipo sasa na kukufikisha mbali zaidi.

Fungu la pili ni asilimia 20 ya kile kipato kilichosalia baada ya kuondoa makato. Fungu hili litumie kuanza kulipa madeni yako. Ongea vizuri na wale wanaokudai ambao hawakukati moja kwa moja, waoneshe nia ya kuwalipa kidogo kidogo. Wengi watakubali kwa sababu ni afadhali kulipwa kidogo kidogo kuliko kutolipwa kabisa.

Fungu la tatu ni asilimia 70 iliyobaki, hii ndiyo unayopaswa kuishi nayo. Yaani matumizi yako yote yasizidi fungu hilo ulilotenga. Hata kama ni kiasi kidogo cha fedha, ishi kwa kiasi hicho. Kama itakulazimu kula mchicha kila siku, kula, kama itakulazimu usinunue nguo tumia ulizonazo sasa. Ninachokushauri hapa ni uhakikishe unaishi kwenye kipato hicho pekee, usizidishe hata shilingi mia moja.

Wacha nikuoneshe kwa mfano ili tuelewane vizuri.

Tuchukulie labda kipato unachopokea baada ya yale makato ya msingi ni laki tano. Na hapa ukikatwa madeni ya moja kwa moja unabaki na laki tatu. Sasa hii laki tatu ndiyo unapaswa kuigawa kwenye mafungu matatu;

Fungu la kwanza ni asilimia 10, ambayo ni shilingi 30,000/= hii ni hazina yako, iweke mahali ambapo huwezi kuitumia kabisa. ni akiba ambayo baadaye utaiwekeza na kukuzalishia zaidi. Hii itaanza kukupa hisia za kuitawala fedha.

Fungu la pili ni asilimia 20, ambayo ni shilingi 60,000/= hii utaitumia kulipa yale madeni madogo madogo ambayo hukatwi moja kwa moja. Ongea na wote wanaokudai vizuri kuonesha nia ya kuwalipa na mpango wako. Watakubaliana na wewe.

Fungu la tatu ni asilimia 70 iliyobaki, ambayo ni shilingi 210,000/= hii ndiyo hela yako ya matumizi. Kwa namba yoyote ile hakikisha matumizi yako ya mwezi hayawi 211,000/= ukifika hapo tu jua umeshapoteza. Dhibiti kabisa matumizi yako. Ishi kwa msoto hasa, maana kuondoka kwenye madeni siyo zoezi rahisi kama ambavyo utakuwa unafikiria. Kama utakula mara moja kwa siku, sawa, kama utahitaji kutembea kwa miguu badala ya kutumia usafiri sawa, kama utahitaji kutokununua vocha za simu na vingine ambavyo siyo muhimu fanya hivyo.

Kwa sasa usianze kujifikiria mara mbili kwamba maisha yako, kama ungekuwa ni nchi tungesema upo kwenye STATE OF EMERGENCY, kama ni ugonjwa basi tungesema upo ICU. Kama umewahi kuona mtu aliyepo ICU, humkuti akila ugali au wali, kwa sababu hivyo vyote hawezi kuvitumia, anatumia vile laini laini kwa sababu ndiyo anaviweza kwa wakati huo.

Muhimu sana; kuanzia sasa, mpaka pale utakapokuwa umeondoka kwenye madeni haya, NI MARUFUKU KABISA KUKOPA. Ndiyo kwa namna yoyote ile usikope, hata kama ni dharura kubwa kiasi gani, angalia njia nyingine za kutatua dharura hiyo na utaziona tu.

Hii niliyokushirikisha hapa, ni njia ya uhakika ya kuondoka kwenye madeni na kuanza kutengeneza utajiri wako. Lakini nimekushirikisha nusu tu ya njia hii, kuna sehemu ya pili ambayo ni nzuri zaidi sijaiweka hapa. Hii ni kwa sababu najua wengi hawafanyii kazi hatua hii ya kwanza, wanakimbilia hatua ya pili na kuishi akuangukia pua.

Sasa wewe fanyia kazi hatua hii ya kwanza, halafu baada ya mwezi mmoja nitafute moja kwa moja kwa njia ya simu 0717 396 253 na nitakupa sehemu ya pili ya mpango huu wa kuondoka kwenye madeni na kufikia uhuru wa kifedha. Hii ni kwa yeyote ambaye anapitia hali kama hiyo, fanya zoezi hilo nililotoa hapo, kwa mwezi mmoja, ukishafanikiwa nitafute nikupe mpango kamili.

Kama utaona hii ni ngumu kwako, sina namna nyingine ya kukusaidia, ninachoweza kukuambia ni kwamba ukishafanya makosa, ni lazima utumikie adhabu. Ulifanya makosa kuingia kwenye madeni, unahitaji kutumikia adhabu ili kuondoka kwenye madeni hayo. Kama mtu atakushauri vingine, kwamba ipo njia rahisi zaidi ya kuondoka kwenye madeni yako, basi kimbia haraka sana usimsikilize, maana atakupoteza zaidi.

Fanya zoezi hilo kwa mwezi mmoja, halafu nitafute moja kwa moja kwenye simu yangu uingie rasmi kwenye mpango kabambe wa kushika hatamu ya maisha yako, chini ya usimamizi wangu.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya juma tatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: