Kuna imani ambazo zinakaribisha fedha na hivyo kuleta utajiri na pia kuna imani ambazo zinafukuza kabisa fedha. Ndani ya jamii zetu, imani kubwa zilizotawala ni zile za kufukuza fedha.

Moja ya imani ambayo inafukuza fedha na kuwafanya wengi kubaki kwenye umasikini ni imani ya UHABA.

Jamii na watu wanaokuzunguka wanakufanya uamini kwamba duniani kuna uhaba wa fedha. Kuna uhaba wa vitu vizuri na hivyo kukufanya uone wewe huwezi au hustahili kupata vitu hivyo.

Kwa imani hii ya uhaba wa fedha na vitu vizuri, watu wanajikuta wakisukumwa kushindana na kupigania vile vichache vinavyoonekana. Ambacho watu hawa hawajui ni kwamba kuna fursa nyingi zaidi za kutengeneza fedha tofauti na zile chache ambazo kila mtu anaziangalia.

Dunia haina uhaba wa fedha, dunia haina uhaba wa vitu vizuri, bali dunia ina uhaba wa mawazo bora ya kuwezesha kuongeza thamani na kuongeza fedha. Yaani ni kwamba, fedha zipo nyingi iwezekanavyo, kama yatakuwepo mawazo bora yanayoweza kuongeza thamani inayoendana na fedha zinazohitajika.

Hebu chukulia dunia ya miaka 100 iliyopita, hakukuwa na kompyuta, wala mtandao wa intaneti wala vitu vingi tunavyofurahia sasa. Hivyo hakuna mtu aliyetafuta fedha ili kununua kompyuta, au simu nzuri au kulipia mtandao wa intaneti. Lakini vitu hivi tunavyo sasa na tunatafuta fedha za kuwa navyo kila siku. Hii ina maana kwamba waliokuja na mawazo ya kuleta vitu hivi, wameongeza thamani kwenye dunia na dunia imewalipa kulingana na thamani kubwa waliyoleta.

Hivyo na wewe hapo ulipo, unaweza kuongeza kipato chako utakavyo, kama utaweza kuongeza thamani kwenye dunia. Jua na amini ya kwamba hakuna uhaba wa fedha, bali upo uhaba wa thamani. Ongeza thamani na fedha zitaongezeka vile utakavyo.

Fedha zipo, na unastahili kabisa kupata fedha unazotaka. Hakuna wa kukuzuia bali wewe mwenyewe. Vuka imani zinazokuweka kwenye umasikini na beba imani za utele na zikuwezeshe kupata kila unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK