Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Ni siku nyingine mzuri sana ambayo tumeianza. Ni ile siku ambayo kuna mambo ulijiambia nitafanya kesho. Nataka nikukumbushe tu rafiki yangu kwamba kesho yenyewe ndiyo imeshafika sasa. Usipeleke tena kwenye kesho nyingine zaidi ya leo.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KUPOTEA, kuliko kubaki hapo ulipo.
Rafiki, leo sitaki tubembelezane, nataka nikuambie ukweli kama ulivyo.
Najua unajua kwamba kutokuchukua hatua ni kujihakikishia kwamba utaendelea kubaki hapo ulipo sasa.
Lakini pia najua unajiona bado hujawa tayari kuchukua hatua fulani, unaona bado kuna vitu hujakamilisha, na hivyo kuendelea kubaki hapo ulipo sasa.
Sasa leo nataka nikuambie kitu muhimu rafiki,
Ni bora upotee kuliko kubaki hapo ulipo sasa.,
Ni bora ufanye kitu ukosee kuliko kutofanya kabisa.
Ni bora uanze biashara upate hasara kuliko kutokuingia kwenye biashara kabisa.
Unajua kwa nini nakuambia ni bora rafiki?
Kwa sababu ukishapotea utaitafuta njia sahihi, na mjanja yeyote huwa hapotei mara mbili. Wanasema unapotea wakati wa kwenda, siyo na wakati wa kurudi. Hivyo kama utapotea, utaijua njia sahihi na hutapotea tena.
Ukianza biashara na kupata hasara, utajifunza mengi mengi mengi mno ambayo usingeweza kujifunza kabla hujaingia kwenye biashara. Utajua mambo gani yanapelekea kushindwa kwenye biashara, utajua njia za kufuata na njia za kuepuka.
Kwa kifupi, kufanya na kukosea ni darasa kubwa kubwa kubwa mno kuliko kutokufanya kabisa. Anza kufanya na jifunze kupitia makosa utakayofanya. Jaribu kitu kipya leo, kikifanikiwa itakuwa poa, kikishindwa utakuwa umejifunza.
Nakutakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
http://www.makirita.info