Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.

Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tutaweza kufika popote tunapotaka kufika.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu THAMANI YAKO NA MAWAZO YA WENGINE.
Moja ya njia ambazo watu wamekuwa wanatumia kubaribu maisha yao, ni kuchukua thamani yao kutokana na mawazo ya wengine juu yao.
Yaani mtu anajiona wa thamani pale wengine wanapomfikiria hivyo, na kujidharau pale wengine wanapomchukulia wa kawaida tu.
Hii ni njia mbaya sana ya kuharibu maisha yako, kwa sababi huwezi kumlazimisha mtu akufikirie kama unavyotaka wewe.
Mtu atachagua kukufikiria vile anavyotaka yeye, kutokana pia na matatizo na changamoto zako.
Kutumia fikra za wengine kupima thamani yako, ni kujidharau na kujikatisha tamaa.
Popote ulipo, kumbuka wewe ni wa thamani na fanya yale ambayo ni ya thamani.
Ukisubiri mpaka wengine wakufikirie ni wa thamani, utachelewa sana, na huenda usijione wa thamani kabisa kwa sababu kila mtu ana maoni yake binafsi juu yako wewe.
Wewe ni wa thamani, hapo ulipo sasa. Toa thamani zaidi kwa lolote unalofanya, na wengine wanavyokufikiria na kukuchukulia hiyo ni juu yao. Wewe fanya lile ambalo ni sahihi, mara zote.
Nakutakia siku njema sana.
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,
#KochaMakirita