Habari za leo rafiki?

Katibu kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Kupitia makala hizi tunashirikishana hatua mbalimbali za kuchukua kwa changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha yetu.

Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya watu kutumia mafanikio yako kukuadhibu. Yaani iko hivi, pale inapotokea wewe umefanikiwa kuliko wale wanaokuzunguka, hasa ndugu zako, wao wanachukulia kwamba ni jukumu lako wewe kuwapa chochote unachotaka. Na kama usipowapa basi watasema unaringa au huwajali. Kwa kuwa wewe una mafanikio kidogo kuliko wao, wanachofikiria ni kwamba muda wowote unaweza kuwasaidia na hivyo ukiwaambia huwezi wanaona umekataa tu au una roho mbaya.

Hili limekuwa changamoto kwa wengi ambao wamepata nafasi nzuri kidogo na kuzungukwa na watu ambao hawajapata nafasi kama hizo. Kupitia makala hii ya leo tutajifunza hatua sahihi za kuchukua ili kuondokana na changamoto hii na kuweza kufurahia maisha na mafanikio yako, badala ya mafanikio kuwa mzigo kwako.

SOMA; Hatua Za Kuchukua Pale Watu Wako Wa Karibu Wanapokukatisha Tamaa.

Kabla hatujaangalia ni hatua zipi za kuchukua, tupate alivyotuandikia msomaji mwenzetu ambaye anakabiliwa na changamoto hii.

Asante kocha wangu kwa ushauri wako mwingi ambao naona unanifungua kila siku ninapo soma Makala zako, na semina ya siku kumi iliyopita naona imenisaidia sana japo bado napambana.

CHANGAMOTO ZANGU NI KAMA IFUATAVYO:

1 . Wiki iliyopita nilipata changamoto kubwa sana, katika familia yetu tuko saba mimi angalau ndio naonekana kama nina kipato kikubwa kuliko wote, lakini kila mtu ana shughuli zake. nilipokea ombi mmoja anataka 200,000, mwingine 500,000, na mwingine 200,000 hii ni familia moja wote mzazi na watoto wote wanataka pesa wakati watoto ni wafanyakazi na mama ni mfanyabiashara. nikapokea ombi lingine mwingine anaomba 200,000 amlipie ada mtoto baada ya ada yake kumkopea mwingine na mwingine anaomba nimpe kadi yangu ya kura ili apate dhamana wapi sijui. Bahati nzuri sikuwa na pesa yoyote mkononi hivyo sikuweza hata mmoja kumpatia na wote hapo nina wafanyakazi pia. changamoto moja ni kubwa sana katika hao mwenye kuomba kadi yangu ya kupigia kura huwa anapenda kuiga saini yangu kutumia katika vitu vyake na hivyo baada ya kumnyima kadi hakuna mawasiliano tena naye. Nifanye nini kwa huyu ambaye anatumia signature yangu kwenye mambo yake na alitamka yeye mwenyewe, naomba msaada. Je kwa mtindo huo wa wote wanataka niwakopee ningekuwa na pesa ningefanyaje?

2. Mimi ni mfanyakazi lakini ni mwenyeji wa Mbeya kwa sasa nimehamishiwa Mtwara. Changamoto yangu kubwa ni kuwa nina miaka mitano tu ya kazi kwa sasa, nilikuwa nimejipanga kuanzisha bustani kubwa katika shamba la ekari tatu nikitaka nijue matokeo yake kabla sijamaliza muda wangu wa kazi kama inalipa. Kutokana na uhamisho huu naona kabisha siwezi kufanya tena hiyo biashara kwa sababu nilitaka niandae visima katika shamba hilo maana ni sehemu ya maji, pia nizungushie wigo kuzuia watu ambao hawaogopi kuvuna mali ya wenzao. Nifanyeje ili niweze kufanikiwa? NI MIMI MWANAMAFANIKIO, MSAADA WAKO NI MAFANIKIO YANGU UWE NA SIKU NJEMA. Lesther M.

Ndugu Lesther,

Kwenye changamoto ya kwanza, kama ambavyo nimeeleza kwenye utangulizi wa makala hii ya leo, wanachokifanya ndugu zako ni kutaka kukuadhibu kwa mafanikio kidogo uliyonayo. Kwa sababu haiwezekani watu wote hao kutaka fedha kwako kwa wakati mmoja. Hata kama una fedha nyingi kiasi gani, bado huwezi kugawa nyingi kiasi hicho kwa wakati mmoja. Utashindwa kufanya mambo mengine muhimu kwenye maisha.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kufanya Pale Ndugu Zako Wanapokuona Wewe Ni Mbaya(Mchawi) Kwa Sababu Una Mafanikio.

Hata kama wewe ndiye mwenye kipato kikubwa kuliko wengine wote, bado huwezi kugawa tu kama kila mtu anavyotaka mwenyewe, wewe pia una mahitaji yako muhimu kwa ajili ya kutengeneza uhuru wa kipato ambao utakunufaisha wewe na wengine pia.

Hivyo kama ambavyo tumejifunza kwenye makala zilizopita, ni muhimu uangalie njia bora zaidi ya kuwasaidia hao ndugu zako badala ya kuwapa fedha moja kwa moja. Angalia namna ambavyo unaweza kuwasaidia kutengeneza kipato zaidi ili waache kuwa tegemezi kwako moja kwa moja.

Na uzuri umesema kila mtu ana shughuli zake, basi unaweza kukaa chini na kila mtu na kumshauri njia bora za kuweka akiba na kukuza kipato kupitia shughuli wanazofanya. Kwa sababu unaweza kujikuta wewe unajinyima ili kufanya mambo makubwa, huku wenzako wanajiachia wakijua wakipata shida wewe upo na utawasaidia. Fuatilia hilo la kuwapa elimu zaidi ya namna wanaweza kutunza vipato vyao na kuongeza kipato zaidi.

SOMA; Kuwa Makini Na Fedha Zako, Ni Wewe Pekee Unayeweza Kuzilinda.

Kuhusu hilo la ndugu yako kutaka kitambulisho chako na kuiga sahihi yako ni jambo la ajabu sana nasikia kutoka kwako. Na kwa hili nazidi kupata picha kwamba ndugu zako hao wanatumia mafanikio yako kukuadhibu. Yaani wanachofanya ni wao kutaka chochote wanachotaka kwako na ukiwanyima basi unaringa au una roho mbaya kwa sababu umefanikiwa na hutaki wao wafanikiwe.

Sasa naomba nikuambie jambo moja, haijalishi watakuona una roho mbaya kiasi gani, haijalishi watakuona huwajali kiasi gani, kamwe usiruhusu mtu kutumia utambulisho wako kwa kitu chochote kile, hata kama ni kitu kizuri. Kama ana shida na utambulisho msaidie atengeneze utambulisho wake mwenyewe. Yaani kama ni kitambulisho hana, msaidie apate kitambulisho hata kama ni leseni ya udereva. Lakini kamwe usiruhusu mtu atumie kitambulisho chako kwa jambo lolote lile, hata kama unamwamini kiasi gani, kitambulisho ni chako wewe, lolote litakalotokea iwe ni kwa bahati mbaya, litakuhusu wewe moja kwa moja. Usikubali kabisa kuendekeza hilo, litakuja kukuingiza kwenye matatizo makubwa. Huyo ndugu yako anaweza kwenda kuomba mkopo mahali kwa jina lako, ukashangaa unakuja kukamatwa wewe ulipe mkopo.

Na kuhusu yeye kutumia sahihi yako, hilo nalo lifanyie kazi. Kwanza kaa naye chini yeye kumweleza ya kwamba aache kutumia sahihi yako, kwa sababu siyo vizuri na ni kosa kisheria. 

Kama ataamua kuendelea kutumia, basi chukua hatua zaidi, unaweza kulifikisha kwa wazee wa familia au ukoo na ukiona huko hupati msaada basi chukua hatua za kisheria. Wakati unafuatilia hilo hakikisha mtu huyo hapati picha zako kwa namna yoyote ile, maana anaweza kupata picha zako na kwenda kuchukua mkopo kwa jina lako au kufanya jambo jingine lolote ambalo litakuumiza wewe.

Kuhusu changamoto ya pili ya wewe kuhamishwa eneo la kazi na hivyo kushindwa kuendelea na mradi uliopanga kufanya mwanzo, huna namna inabidi uache mradi huo kwa sasa na kuangalia mradi mwingine unaoweza kufanya kwa lile eneo unalofanya kazi kwa sasa. Kwa sababu itakuwa vigumu sana kwako kuanzisha mradi mpya huku wewe ukiwa mbali na mradi huo. Kujaribu kufanya hivyo inaweza kukuingiza kwenye hasara kubwa.

Angalia kwa eneo ulilopo sasa, ni mradi gani unaweza kufanya, na anza kuufanya mapema kabla tena mabadiliko hayajatokea. Pia hilo lililotokea liwe msukumo kwako wa kuchukua hatua haraka ili kuondoka kwenye ajira. Kwa sababu ni jambo la kuumiza pale ambapo umeshaweka mipango ya maisha yako ya unataka uishi wapi na ufanye nini, na unalazimika kuacha yote hayo kwa sababu ya ajira.

Ile mipango yako ya mwanzo usiiue kabisa, bali isimamishe kwa sasa, tumia nafasi uliyopo sasa kuanza kitu kingine upya, kitakachowezekana kwa sasa, halafu baadaye ukishanunua uhuru wako, unaweza kurudi kwenye mipango yako ya awali. Usipoteze muda kufikiria mipango yako ya mwanzo, angalia sasa unaweza kuchukua hatua gani na chukua hatua hiyo.

Fanyia kazi haya ambayo tumeshauriana hapa, ili uweze kushika hatamu ya maisha yako na kufikia yale mafanikio ambayo unayaangalia.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.